Kakakuona hatarini kutoweka, jitihada za makusudi zahitajika

Muktasari:

 Huko Marekani, soko la kakakuona linazidi kukua kwa sababu ya mahitaji ya ngozi yake inayotumika kutengenezea mikanda, mabegi na viatu

Kasi ya uvunaji wa kakakuona duniani inatishia kutoweka kwa kiumbepori huyo kutokana na kuongezeka kwa mahitaji yake katika mataifa yanayomtumia kama chanzo cha malighafi za kutengenezea bidhaa tofauti na pia kitoweo kwa baadhi ya jamii.

Mataifa mbalimbali yameshuhudia kukamatwa kwa kakakuona akisafirishwa kwa njia haramu au viungo vyake, jambo linalotokana na vita kali ya kupambana na biashara ya mnyama huyo mdogo.

Tayari kakakuona ameadimika katika nchi za Asia na sasa wengi wanavunwa Bara la Afrika na kusafirishwa kwenda Asia na Marekani ambako kuna mahitaji makubwa na soko la mnyama huyo.

Mnyama huyo mwenye magamba magumu mwilini mwake amekuwa akiwindwa kwa ajili kupata magamba hayo ambayo yanatumika kiimani kama dawa na jamii nyingine duniani wanapenda zaidi nyama yake.

Soko kubwa la kakakuona liko Asia anakotumika kama kitoweo na magamba yake kama dawa.

Matumizi yake yanazidi kuongezeka pia barani Afrika.

 Huko Marekani, soko lake linazidi kukua kwa sababu ya mahitaji ya ngozi yake inayotumika kutengenezea mikanda, mabegi na viatu.

Jitihada mbalimbali za kimataifa zinafanyika kuhakikisha mnyama huyo analindwa ili aendelee kuwepo. Hamasa kubwa inatolewa kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa kuripoti matukio ya uvunaji wa mnyama huyo ili hatua za kisheria zichukuliwe.

Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira (JET) kinachotekeleza mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili, kimewakutanisha waandishi wa habari na wataalamu wa masuala ya uhifadhi nchini kuwapa elimu kuhusu viumbe walio hatarini kutoweka na usafirishaji wa viumbepori.

Mratibu wa Usimamizi wa Sera ya Maliasili kutoka Mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili, Allen Mgaza anasema mwenendo wa ukamataji wa magamba ya kakakuona unazidi kuongezeka dunia kutokana na jitihada za mataifa.

Anatolea mfano tukio la hivi karibuni la tani sita za magamba ya kakamuona zilikazomatwa huko Malaysia zikipelekwa sokoni.

 Sio Malaysia pekee, hata Tanzania baadhi ya watu wamekamatwa kwa kukutwa na magamba ya mnyama huyo wakijaribu kuyasafirisha.

“Hivi unadhani hadi kufikisha tani sita za magamba ya kakakuona, ni kakakuona wangapi watakuwa wameuawa ukiangalia size (ukubwa) ya kiumbe yule, ni wangapi watakuwa wameuawa?

“Hii biashara ikifanyika kwa miaka minne au mitano, hakutakuwa na wanyamapori, hawa kakakuona watapotea na sicho kitu tunachotamani kukiona,” anasema Mgaza wakati akimzungumzia mnyama huyo.

Katika jitihada za kumlinda mnyama huyo, anasema Tanzania imesaini mkataba wa Cites wa kimataifa unaodhibiti biashara ya kimataifa ya viumbepori walio hatarini kutoweka, pia anasema imeboresha sheria ili kuakisi makubaliano na mikataba ya kimataifa.

“Nadhani kutoa elimu ni muhimu, lakini usimamizi wa hizi sheria ni muhimu. Kuwa na sheria nzuri ni jambo moja lakini kuhakikisha hizi sheria zinasimamiwa vizuri kuhakikisha kwamba uelewa ni mkubwa na kuviwezesha vyombo vya usimamizi na utekelezaji wa sheria,” anasema Mgaza.

Mtaalamu huyo anasema biashara haramu ya viumbepori ni tatizo la kimataifa na limekuwa na athari nyingi za kiuchumi na kijamii.

Anasema biashara hiyo imetajwa kuwa namba nne kati ya biashara haramu zinazofanyika duniani ikitanguliwa na biashara haramu za usafirishaji wa dawa za kulevya, binadamu na wa bidhaa bandia.

Mgaza anasisitiza kwamba, biashara ikiwa inahusisha watu wengi kama hizo, lazima kuwe na ushirikiano mkubwa wa kitaasisi na jamii kuungana na vyombo vya dola katika kuhakikisha kwamba wanatokomeza biashara hiyo.

“Ni muhimu kuelimisha jamii kwamba kujihusisha kwako na makundi yanayofanya biashara haramu ya viumbepori, umeliangusha Taifa lako kwa sababu biashara ikifanyika haramu hatupati kipato na tunawapoteza hawa viumbe.

“Kwa muda mrefu viumbe hivi vinawindwa, mwisho wa siku vitapotea. Sitamani ifike kipindi tuwaonyeshe watoto wetu, wajukuu wetu picha za wanyama kwamba zamani kulikuwa na mnyama anaitwa kakakuona, kuna mnyama alikuwa anaitwa tembo,” anasema Mgaza.

Viumbe wengine hatarini

Mgaza anabainisha kwamba viumbe wengine walio hatarini kutoweka kutokana na kasi kubwa ya uvunaji ni tembo wanaouawa kwa sababu ya biashara ya meno ya tembo iliyoshamiri katika mataifa ya Asia.

“Kwa mujibu wa mkataba wa Cites, kuna viumbe ambao wakifanyiwa biashara na biashara hiyo isipodhibitiwa, viko kwenye hatari ya kutoweka, kwa mfano kakakuona, tembo na kima wa aina tofauti tofauti.

“Siyo lazima awe mnyama mzima, bali hata sehemu za miili yao kama vile ngozi, magamba, kucha, nyama au mifupa yao, vyote hivyo vinapaswa kudhibitiwa kwani biashara ikiendelea viumbe hivi vitatoweka,” anasema Mgaza.

Sio wanyama pekee, hata mimea mingine pia iko hatarini kutoweka kutokana na uvunaji wake.

 Mkataba wa Cites unatambua na kuweka udhibiti wa biashara ya baadhi ya mimea ambayo iko hatarini kutoweka kabisa.

Ofisa Uhifadhi kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Reuben Magandi anabainisha kwamba mimea iliyohatarini kutoweka ni miti jamii ya mninga, msandali na mpingo.

“Miti hii imeorodheshwa na Cites kama mimea iliyo hatarini kutoweka, hivyo tunafanya jitihada mbalimbali kuhakikisha tunailinda na kuhamasisha jamii kupanda miti mingine hasa ya matunda kwenye maeneo yao.

“Kila mtu anatamani kulalia kitanda cha mninga, mwingine anataka milango ya mninga. Sasa ukiachia hivi tu, miaka ijayo tutakuwa hatuna mti huo wa asili. Mpingo pia unatumika kuchongea vinyago, msandali wanatengenezea pafyumu, hayo yote ni mahitaji yanayochochea ukataji wake,” anasema Magandi.

Kuhusu hatua wanazochukua, Magandi anasema wameimarisha ukaguzi na udhibiti wa usafirishaji wa bidhaa za misitu kwenda nje ya nchi na pia wanagawa miche ya miti kwa wananchi na shule mbalimbali ili kuhamasisha utunzaji wa mazingira.

Hatua zinachukuliwa

Februari 2023, Kamishna Mwandamizi kutoka Mamlaka ya Wanyamapori (Tawa), Mlage Kabange alisema Tawa kwa kushirikiana na Taasisi ya Wanyamapori Afrika (AWF) walianzisha kikosi cha mbwa wanusao mwaka 2015 kwa lengo la kupambana na ujangili.

Katika makubaliano hayo, Wizara (Maliasili na Utalii) kupitia Tawa ilikuwa na jukumu lka kutoa askari na AWF walikuwa na jukumu la kutoa mafunzo, mbwa, magari na kugharamia matunzo ya mbwa ikiwamo chakula na matibabu.

Kabange alisema awali kikosi hicho kilikuwa na mbwa wane na askari sita, lakini kufikia mwaka jana walifikisha askari 13 wa kikosi cha mbwa na mbwa wanane.

“Katika kipindi kuanzia mwaka 2015 hadi 2023, doria za kikosi cha mbwa kimefanikiwa kukamatwa kwa watuhumiwa wa ujangili 108, mengo ya tembo, magamba ya kakakuona, nyamapori mbichi, meno ya kiboko na meno ya simba,” alisema.

Wakati jitihada hizo zikifanyika, kesi mbalimbali zinaendelea katika Mahakama za Tanzania kwa watu mbalimbali waliokutwa na nyara za Taifa yakiwamo magamba ya kakakuona anayeaminika kuwa chanzo cha bahati na utabiri.