Kalage aacha kazi Hakielimu, asema…

Muktasari:
- Amehudumu katika nafasi ya ukurugenzi wa shirika hilo kwa miaka 10, nafasi yake inakaimiwa na Godfrey Boniventur
Dar es Salaam. Uongozi wa Dk John Kalage katika Shirika la Hakielimu umetamatika baada ya mwanataaluma huyo kutupa karata yake kwenye ulingo wa siasa.
Taarifa ya kuondoka Kalage imetolewa na Mwenyekiti wa Bodi wa Shirika hilo, Sylvester Orao akieleza mabadiliko ya uongozi wa taasisi hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa ya Orao kwa umma aliyoitoa leo Alhamisi, Julai 3, 2025, amesema katika kipindi ambacho anatafutwa mkurugenzi mtendaji mwingine nafasi hiyo itakaimiwa na mkuu wa miradi wa shirika hilo, Godfrey Boniventure.
Orao amesema Kalage ameachia nafasi hiyo ili kupata fursa ya kujihusisha na siasa akiwa ni miongoni mwa wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) waliotia nia ya kugombea ubunge katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 2025.
“Hakielimu ni shirika huru lisiloegemea upande wowote wa kisiasa. Tunasisitiza wafanyakazi wake wote wanapaswa kutojihusisha na siasa wanapozitumikia nafasi zao au kuwa na uhusiano wowote wa kisiasa.
“Tunaheshimu uamuzi wa Kalage na tunamshukuru kwa mchango wake, katika kipindi hiki ambacho tunaendelea na mchakato wa kumpata mkurugenzi nafasi yake itachukuliwa na Godfrey Boniventure,” amesema Orao.
Mwananchi imezungumza na Dk Kalage ambaye amekiri kuacha kazi kwenye shirika hilo akieleza ilikuwa ni uamuzi wake wa muda mrefu ili apate fursa nzuri ya kuingia kwenye siasa.
Amesema tayari ameomba ridhaa ya CCM kugombea Jimbo la Korogwe Vijijini na matarajio yake ni kwenda kuyatekeleza kwa vitendo mengi ambayo yamekuwa yakishauriwa na wadau wa elimu.
“Ni kweli nataka kugeukia upande mwingine, nikipata ridhaa hiyo nitakwenda kuyasukuma yale yote ambayo tumekuwa tukishauri tukiwa nje lakini kwa namna moja au nyingine hayakutekelezwa.
“Tunahitaji kuwa na Bunge lenye wataalamu ili kusukuma gurudumu la maendeleo, nami nimeona naweza kuwa sehemu ya maendeleo hayo. Naona pia mwaka huu wataalamu wengi wameonesha nia ya kutaka kuingia bungeni, endapo watafanikiwa itakuwa nafasi nzuri kwao kutoa mchango kwa maendeleo ya taifa,” amesema Kalage.
Kiongozi huyo ameeleza anajivunia miaka 10 ya uongozi wake katika shirika hilo kwani limekuwa na mchango mkubwa kwenye sekta ya elimu.
“Katika kipindi cha uongozi wangu tumejitahidi kushirikiana na Serikali, wadau na mamlaka za uamuzi, tuliwashirikisha kila tulichoona kinafaa kwa mustakabali wa elimu nchini.
“Hatukuwa na mivutano, mara zote tulikaa mezani na kushauri yale ambayo tuliona yanafaa na mengi ilikuwa ni matokeo ya tafiti na mapendekezo ya wadau wa sekta ya elimu ambayo kimsingi yamekuwa na tija kwa elimu ya nchi hii,” amesema.
Akitolea mfano wa hilo amesema shirika hilo lilikuwa taasisi ya kwanza iliyofanya utafiti na kubaini upungufu kwenye Sera ya Elimu ya mwaka 2014 ikiwa ni miezi michache baada ya kuzinduliwa.
“Tulifanya utafiti na kueleza mapungufu, tulionekana watu wa ajabu sera haina hata muda mrefu halafu tumeanza kuipigia kelele, lakini kadiri siku zilivyozidi kwenda kelele ziliongezeka na hoja yetu ikapata mashiko.
“Alipoingia madarani Rais Samia Suluhu Hassan akaelekeza wizara ya elimu ifanye mapitio ya sera hiyo na tumeona kazi iliyofanyika hadi kuipata Sera ya elimu ya mwaka 2014 toleo la mwaka 2023,” amesema Kalage.