KALAMU HURU:Vijembe vinapunguza uwajibikaji wa Bunge

Wednesday December 23 2020
VIJEMBEPIC
By Peter Elias

Bunge ni moja ya mihimili ya dola likiwa na wajibu wa kuisimamia Serikali katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo na bajeti.

Mbali na jukumu la kutunga sheria na kupitisha bajeti, Bunge pia lina kazi ya kuisimamia mihimili mingine ambayo ni Serikali na Mahakama bila kuingilia utendaji wao.

Mihimili yote ina wajibu huo na inatakiwa kufanya kazi kwa kutizama kama mhimili mwingine unatimiza wajibu wake.

Katika Bunge lililopita, kulikuwa na mnyukano mkali kati ya wabunge wa kambi rasmi ya upinzani hasa wa Chadema na wale wa chama tawala wanaoitetea Serikali wakati wote.

Hayo yote sio hoja kubwa, tatizo ni pale wabunge wanapoacha kujielekeza kwenye hoja inayojadiliwa halafu wakarushiana vijembe kwa maslahi yao binafsi ya kisiasa au vyama vyao.

Hilo siyo jambo sahihi kwa sababu linawafanya wasiifanye kazi yao kikamilifu. Wananchi waliwachagua ili kuwasemea kero na mahitaji yao bungeni na Serikali isikie na kutekeleza kadri bajeti inavyoruhusu katika mwaka husika.

Advertisement

Kunapokuwa na vita vya maneno baina ya wabunge, dhima ya Bunge kuisimamia Serikali inapungua. Mjadala unageuka kuwa wa vijembe na zogo badala ya kutoa suluhisho kwa kero za wananchi.

Wakati fulani, Spika Job Ndugai naye alikuwa akiingia kwenye mtego huo kwa kuwarushia vijembe wabunge wa Chadema jambo lililokuwa likichukua nafasi kubwa kwenye vyombo vya habari na kufunika hoja iliyokuwa ikijadiliwa bungeni.

Hatuwezi kupata maendeleo kama sisi wenyewe tumegawanyika. Upinzani siyo uadui bali ni mawazo mbadala ambayo yanaweza kuchukuliwa na kufanyiwa kazi kwa maslahi ya Taifa.

Upinzani pia siyo kupinga kila kitu hata kama ni bora, upinzani ni kuja na mawazo mbadala ya kujenga badala ya kutukana au kukosoa bila kuonyesha njia. Dhana hizo zikifahamika vizuri na kutekelezwa, zitapunguza vijembe bungeni.

Hata hivyo, mzizi wa hayo yote unaanzia kwenye kokasi za vyama ambazo zinawataka wabunge hao kuzungumza mambo yenye maslahi kwa chama wakati wote wanapochangia hoja bungeni.

Natambua wabunge wanawajibika kwa vyama vyao lakini hilo haliwapi kibali cha kudhoofisha wajibu wa Bunge kwa Taifa. Heshima na wajibu wa Bunge unapaswa kulindwa na wabunge wote bila kujali tofauti zao za kiitikadi.

Kwa kuwa Bunge jipya limezinduliwa, natoa rai kwa wabunge waliochaguliwa kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 28 kutambua kwamba hicho ni chombo muhimu kwa maendeleo ya Taifa hili.

Bila kuwa na wabunge wenye uchungu na Taifa lao, hatuwezi kupata maendeleo tunayoyatarajia. Serikali inajitahidi kuleta maendeleo kwa kujenga miundombinu, ni vizuri wabunge pia wakaungana kutekeleza wajibu wao.

Wabunge wazingatie maslahi ya Taifa wawapo bungeni au kwenye vikao vya vyama vyao. Hiyo itakuwa njia bora ya kuliwezesha Bunge kutimiza wajibu wake wa kikatiba.

Hata kama Bunge halirushwi mubashara, wananchi tunataka kuona kila mbunge anatoa hoja zinazotugusa wananchi badala ya kujadili mambo binafsi ya mbunge mfano mikopo yake benki au mahala pengine popote.

Bunge liibane Serikali kutekeleza mikakati iliyowekwa kuondoa kero mtaani.

Advertisement