Kamati kufuatilia Hakimiliki yatakiwa kuwa huru

Muktasari:

  • Kamati ya kuratibu namna bora ya kusimamia Hakimiliki nchini imetakiwa kuwa huru ili kukusanya mapendekezo yatakayoisadia Serikali kusimamia eneo hilo kwa njia iliyo bora.

Dar es Salaam. Kamati ya kuratibu namna bora ya kusimamia Hakimiliki nchini imetakiwa kuwa huru ili kukusanya mapendekezo yatakayoisadia Serikali kusimamia eneo hilo kwa njia iliyo bora.

Wito huo umetolewa leo Ijumaa Juni 8, 2022 na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Said Yakub katika uzinduzi wa kamati hiyo.

Siku sita zilizopita Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa iliteua kamati kufuatia kuwepo kwa malalamiko kutoka kwa wadau hasa wa sekta ya sanaa kuhusiana na namna mirabaha inavyokusanywa na kugawanywa na kuwepo kwa vitendo vya uharamia katika kazi hizo.

Sakata hili lilifika hadi kwenye vikao vya bunge la Bajeti lililomalizika hivi karibuni ambapo Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki, Hamisi Taletale, alilalamikia moja ya wasanii wake kuambulia Sh50,000 katika mgao huo.  

Akizungumza katika uzinduzi huoYakub amesema kuna wakati inaweza kutokea kukawa na mjadala mkali katika vikao vya kamati lakini lengo ni kupata majibu ya utatuzi wa masuala ya hakimiliki nchini.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Pauline Gekul amesema pamoja na mmbo mengine amesema kamati hiyo inatarajiwa kuratibu mjadala wa namna bora zaidi ya kusimamia Hakimiliki nchini.

"Mjadala huu tungependa ufanyike baada ya siku 30 kuanzia sasa na kamati muhakikisha mnashirikisha kila mdau kwa kutumia nyenzo zote ili kuepuka malalamiko kuwa kuna aliyeachwa kwa kuwa mawazo yao tunayahitaji sana katika kuliboresha hili " amesema Waziri Gekul.

Hata hivyo Waziri huyo ametaja majukumu ya kamati hiyo kuwa ni pamoja na kupendekeza mifumo bora ya kukusanya na kugawa mirabaha inayoshahabina na mifumo inayotumika kwingine duniani.

Jingine ni kupendekeza njia ya kupambana na uharamia na kupendekeza mfumo bora wa uendeshaji wa Cosota kisha kuwasilisha taarifa yake kwa Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Victor Tesha ameahidi kuwa na wenzake watafanya kazi kwa weledi na ubunifu ili kuhakikisha wanatoa mapendekezo yenye tija.

Wajumbe wa kamati hiyo ni pamoja na Mbunge wa Muheza, Hamis Mwinjuma 'Mwana FA', Dk Omar Mohamed, Paul Mattysse, Safina Kimbokota, Torriano Saramba na Gabriel Kitua.

Wengine ni Twiza Mbarouk, Asha Salum Mshana, Saudin Mwakaje na Demesh Mawi.