Kamati ya Bunge yaagiza wauza samaki Kamanga waondolewe

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Miundombinu, Selemani Kakoso akizungumza wakati kamati hiyo ilipotembelea na kukagua mradi wa upanuzi wa Bandari ya Mwanza Kaskazini jijini Mwanza. Picha na Mgongo Kaitira
Muktasari:
Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa ameagizwa kukutana na Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni ili kujadiliana na kupata muafaka wa kuondolewa jengo hilo
Mwanza. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeagiza kuondolewa kwa jengo la Kituo Kikuu cha Polisi Mwanza na wafanyabiashara wanaouza samaki eneo la Kamanga ili kupisha upanuzi wa gati la Bandari ya Mwanza Kusini.
Maagizo hayo yametolewa jana Jumamosi Machi 16, 2024 na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Selemani Kakoso, wakati kamati hiyo ilipotembelea na kukagua mradi wa upanuzi wa bandari hiyo unaogharimu Sh18.6 bilioni ili kuiwezesha kupokea meli kubwa ikiwamo MV Mwanza 'Hapa Kazi Tu' yenye kimo cha ghorofa nne, urefu wa mita 92.6, upana wa mita 17 na uzito wa tani 3,500.
Kakoso amemuagiza Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa kukutana na Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni ili kujadiliana na kupata muafaka wa kuondolewa jengo hilo huku akiwataka wauzaji wa samaki Soko la Kamanga kupisha eneo hilo kwa hiari ili kuruhusu utekelezaji wa mradi huo.
“Kwenye maeneo ambayo ni milki za Serikali wananchi kama wanayatumia ndivyo sivyo wapishe ili mradi uweze kuendelea kufanya kazi. Mradi huu ni wa kimkakati ambao Serikali imewekeza fedha nyingi.
“Maeneo yote ambayo wanatakiwa kupisha ni pamoja na eneo la Jeshi la Polisi kwa kuwa Jeshi la Polisi na bandari ni mali ya Serikali, Waziri wa Uchukuzi na Waziri wa Mambo ya Ndani watakaa ili kuhakikisha maeneo haya yanapishwa ili mradi wa upanuzi wa bandari uweze kufanya kazi vizuri,” amesema Kakoso.
Meneja wa Bandari za Ziwa Victoria, Erasto Lugenge amesema utekelezaji wa mradi huo ulioanza Mei 3, 2023, kwa mkataba wa miezi 18 umefikia asilimia 30 huku ukijumuisha ujenzi wa maegesho, barabara ya sakafu ngumu, jengo la abiria na ujenzi wa uzio wa bandari hiyo.
Lugenge amesema mradi huo unaotekelezwa na Kampuni ya China Fifteen Group Bureau ya nchini China, utahusisha uhamishaji wa mifereji ya maji, kingo za Mto Mirongo eneo linalogusa bandari, kuhamisha miundombinu ya reli na uwekaji wa miundombinu ya umeme katika bandari hiyo.
“Maendeleo ya jumla yamefikia asilimia 30 kwa kipindi cha miezi 11 tangu mradi kuanza hadi kufikia jana. Mkandarasi amelipwa Sh2.4 bilioni pamoja na kodi ya ongezeko la thamani (VAT) ambayo ni sawa na asilimia 13 ya gharama mradi wote,” amesema.
“Kulingana na mpango wa utekelezaji mradi ulitakiwa kuwa umefikia asilimia 46.5 mpaka sasa ukilinganisha na asilimia 30 hivyo maendeleo ya utejkelezaji wa mradi yako nyuma kwa asilimia 16.5, hata hivyo mkandarasi ametakiwa kuongeza vifaa na wafanyakazi na kufanya kazi kwa Saa 24 ili ukamilike kwa wakati,” amesema.
Hata hivyo, Katibu Tawala Msaidizi (Miundombinu) Mwanza, Chagu Nghoma amesema:“Kuna jengo linaloonekana limechakaa hapo kituoni mpaka sasa, Wizara ya Mambo ya Ndani wana hati yake, bandari (TPA) nao wanasema lilikuwa la kwao kwamba lilikuwa linatumiwa na askari wa bandari hapo awali.
“Hili suala lililetwa kwa katibu tawala mkoa na nilikabidhiwa mimi, tukaleta watu wa ardhi wakapima na kuna sehemu ambayo polisi wameshaiachia kwa ajili ya njia ambayo jengo lao mojawapo ni hilo lililochakaa hapo na makubaliano ni kwamba jengo lao lifidiwe na hilo limeshakubalika, kwa hiyo njia itapatikana na kuingia na kutoka bandarini,” amesema Nghoma.
Mwenyekiti wa wauza samaki Kamanga jijini humo, Raphael Magambo amesema amepokea maelekezo hayo kwa utayari.
Huku akidokeza hawapingani na uamuzi huo, amesema wafanyabiashara zaidi ya 400 wanatarajiwa kuhamia eneo hilo la Tampere huku akiiomba Serikali kuboresha miundombinu ikiwamo kujenga mabanda katika eneo jipya wanalotarajia kuhamia ili kuendelea na biashara yao.
“Tumepokea uamuzi huo vizuri tu, halmashauri imeshatuonyesha eneo lenyewe ni zuri tu na tayari maandalizi yameshaanza. Hatuwezi kukataa kuhama kwa sababu wanatuboreshea miundombinu maana bandari ikikamilika tutakuwa wanufaika kwanza, kwa hiyo tuko tayari kuondoka,” amesema Magambo.