Kamati ya Bunge yaitaka Serikali kuchochea mauzo nje

Muktasari:

  • Kamati ya Bunge  Kudumu ya Bajeti imechambua na kutoa maoni yake kuhusu kuhusu mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na mapendekezo ya mwongozo wa maandalizi ya mpango wa  bajeti kwa mwaka 2024/25.

Dodoma. Uchambuzi wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Bajeti umebaini kwamba uwiano wa ulipaji wa deni kwa mauzo ya nchi unakaribia ukomo wa asilimia 15 ambapo hadi Juni, 2023 uwiano huu ulikuwa asilimia 14.1.

Hayo yamesemwa leo Jumatatu Novemba 6, 2023 na Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Omary Kigua kuhusu mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na mapendekezo ya mwongozo wa maandalizi ya mpango wa  bajeti kwa mwaka 2024/25.

Kigua amesema mwenendo huo una athari kwenye akiba ya fedha za kigeni ukizingatia kwamba takribani asilimia 58.71 ya deni la Serikali ni deni la nje ambalo hulipwa kwa fedha za kigeni.

Hata hivyo, amesema endapo mauzo ya nchi hayawezi kukidhi malipo ya deni basi italazimika kutumia akiba ya fedha za kigeni kulipa deni na hivyo kupunguza uwezo wa nchi kuagiza bidhaa na huduma nje.

“Kamati inaishauri Serikali kuchukua hatua za makusudi za kuchochea mauzo ya nje kwa kuongeza mauzo ya mazao ya kibiashara yalioongezewa thamani, kuchochea uzalishaji wa bidhaa za viwandani, kukuza sekta ya utalii pamoja na huduma ili kuimarisha akiba ya fedha za kigeni,”amesema.

Kwa upande wa mkakati wa kuongeza fedha za kigeni, Kigua amesema kamati imebaini mikakati ya Serikali wa kuongeza fedha za kigeni nchini, hauendi sanjari na mkakati wa kupunguza matumizi ya fedha za kigeni kwa wizara, idara, wakala na taasisi za Serikali.

“Hivyo, kamati inaishauri Serikali kuweka sharti la lazima, kwa maofisa masuuli wote kuhakikisha ununuzi wa bidhaa na huduma kuanzia mwaka wa fedha 2024/25, kipaumbele kiwe kwa bidhaa na huduma zinazozalishwa na kupatikana nchini kabla ya kuagiza au kununua bidhaa na huduma nje ya nchi,”amesema.

Aidha, Kigua amesema miradi ya kilelezo ya muda mrefu ambayo haijakamilika.

Amesema kamati imefanya uchambuzi wa miradi ya kielelezo ambayo imekuwa haitekelezwi kwa muda mrefu ili kubaini changamoto zinazoikabili.

Ametaja miradi hiyo ni Mradi wa Magadi Soda Engaruka, Makaa ya Mawe Mchuchuma na Chuma Liganga, Eneo Maalumu la Uwekezaji Bagamoyo na mradi wa kufua umeme wa maji wa Rumakali (MW 222).

Mingine ni miradi wa kufua umeme wa maji wa Ruhudji (MW 358) na miradi ya kuendeleza maeneo huru ya kuongeza mauzo nje.

Amesema miongoni mwa sababu za changamoto hizo ni kukosekana kwa fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi hiyo.