Tanzania yagundua aina nne za kahawa ya Arabika

Muktasari:

  • Taasisi ya Utafiti wa Kawaha nchini (TaCRI) imegundua aina nne za mbegu ya kahawa aina ya Arabika ambayo inavumilia hali ya ukame, ikiwa ni moja ya mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuongeza uzalishaji wa zao hilo.

Moshi. Taasisi ya Utafiti wa Kawaha nchini (TaCRI) imegundua aina nne za mbegu ya kahawa aina ya Arabika ambayo inavumilia hali ya ukame, ikiwa ni moja ya mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuongeza uzalishaji wa zao hilo.

Hayo yamebainishwa na mtaalamu wa kitengo cha uboreshaji wa zao hilo kutoka TaCRI, Nuhu Aman wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Moshi, ambapo amesema taasisi hiyo tayari imekamilisha utafiti na michakato yote na mbegu hiyo inatarajiwa kutoka mwaka huu 2023/2024.

Aman amesema kwa sasa mamlaka ya udhibiti wa ubora wa mbegu Tanzania (Tosci) inaendelea na hatua za kufanya tathimini na uhakiki wa mbegu hizo na baada ya hapo zitatolewa ili ziweze kuwafikia wakulima na kutumika katika maeneo ambayo yameathiriwa na changamoto ya ukame.

"Kama kitengo cha uboreshaji wa zao la kahawa tuneshatoa aina 23 za kahawa bora ambazo zinaendelea kufanya vizuri na kuklmuondolea mkulima gharama za uzalishaji na zimeendelea kuwa na ukinzani wa magonjwa, lakini kwa sasa tuna changamoto ya upungufu wa mvua hivyo tunakuja na aina ambayo inastahimilivu hali ya ukame,"amesema Nuhu na kuongeza kuwa

 "Kwa sasa zipo aina nne ambazo zipo kwenye mchakato wa kutolewa, kwa upande wetu tumeshamaliza mchakato na sasa tumewaachia Mamlaka ya Udhibiti wa Ubora wa Mbegu Tanzania (Tosci) na tunatazamia mwaka huu wa 2023/2024 zitawafikia wakulima,....na aina hizi zinaenda kuwanufaisha wakulima katika maeneo ambayo wamepata changamoto ya ukame na mabadiliko ya tabianchi,".

"Hivyo wakulima waliopo maeneo yenye ukame kwa sasa hiyo haitakuwa tena changamoto baada ya kutoka aina hizi, ataweza kuzalisha kahawa na kupata kipato, hatua ambayo itawawezesha kuboresha maisha yao kwa ujumla"

Akizungumza Mtaalamu wa maabara kutoka Taasisi hiyo, Ephafra Mosi amewataka wakulima wa kahawa kuhakikisha wanapima udongo kabla ya kuwekeza kwenye kilimo hicho ili kufahamu aina na kiasi cha mbolea kinachohitajika.

Amesema matumizi ya mbolea pasipo kujua upungufu wa virutubisho vilivyopo kwenye ardhi husababisha wakulima kupata mavuno kidogo, kwa sababu hutumia mbolea kwa kukisia, hivyo ni vyema kila mmoja akapuma udongo wa shamba lake ili kujihakikishia kilimo chenye tija.

"Imeonekana hali ya rutuba ya udongo nchini imekuwa inadorora mwaka hadi mwaka hivyo tumekuwa tukishauri wakulima kabla ya kuwekeza kwenye kahawa ni lazima wahakikishe wanapata taarifa za udongo ili kujua ni mbolea gani inahitajika na kiasi gani," amesema Mosi

Monica Matemu mkazi wa Rombo mmoja wa wakulima wa Kahawa amesema ugunduzi wa mbegu hizo za kahawa zinayovumilia ukame zitachochea ongezeko la kilimo cha zao hilo nchini.

"Ukame umekuwa ni changamoto kubwa katika maeneo mengi nchini kwa sasa, hivyo endapo zitapatikana mbegu za kahawa zinazovumilia ukame, itawezesha kilimo hiki kukua na kuongeza uzalishaji mkubwa na wenye kuleta tija kwa wakulima," amesema Matemu.