Serikali kubuni mbinu mpya kuongeza unywaji wa kahawa

Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Kisare Makori akizungumza na wadau wa kahawa nchini wakati wa kufunga tamasha la kahawa (Kahawa Festival)  mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Muktasari:

  • Serikali ipo mbioni kubuni mbinu mpya kuongeza unywaji wa kahawa nchini kuimarisha soko la ndani.

Moshi. Serikali imeitaka Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) kushirikiana na wadau wengine wa  zao la kahawa nchini, kuja na ubunifu na mbinu mpya za kuhamasisha unywaji wa kahawa ili kukuza soko la ndani la zao hilo na kuondokana na utegemezi wa soko la nje ya nchi.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na TCB, Tanzania inatumia asilimia 7 ya kahawa inayozalishwa nchini, huku asilimia 93 ikitegemea masoko ya nje ya nchi.

Akizungumza wakati akifunga tamasha la kitaifa la kahawa lililofanyika kwa siku tatu Mjini Moshi mkoani Kilimanjaro, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Kisare Makori amesema kwa sasa zinahitajika jitihada za makusudi na ubunifu ili kuweza kuchochea ukuaji wa soko la ndani la kahawa, hatua ambayo pia itasaidia kuimarika kwa soko la zao hilo. 

"Kahawa ni kinywaji kinachotumika kwa wingi sana duniani baada ya maji, ambapo kwa siku hunywewa vikombe bilioni 3 duniani kote, lakini pamoja na umaarufu wa kinywaji hiki duniani, hapa nchini bado unywaji ni mdogo na nimeelezwa ni asilimia 7 na hivyo asilimia 93 ya kahawa tunayozalisha tunategemea masoko ya nje," amesema Makori.

"Kiwango hiki cha chini cha unywaji kahawa kinachangiwa na sababu mbalimbali ikiwemo imani potofu za kuhusisha kinywaji hiki na matatizo ya kiafya hivyo kufanya watu wengi kuogopa kukitumia...Wito wangu kwa Bodi ya Kahawa na wadau wote wa kahawa nchini ni kuja na ubunifu na njia mpya za kuhamasisha wananchi na kutoa elimu juu ya faida za unywaji kahawa ili kukuza juhudi za kuongeza thamani ya soko la ndani."

Aidha amesema zao la kahawa ni moja ya mazao ya kimkakati nchini ambayo yanatakiwa kusimamiwa vizuri ili kuweza kutoa mchango katika jitihada za serikali za kutatua tatizo la ajira na kuchangia katika ukuaji wa uchumi na ujenzi wa viwanda, hivyo bodi na wadau wanapaswa kuhakikisha sekta ya kahawa inakuwa na kufikia malengo yaliyowekwa na serikali.

"Wadau wa kahawa tuna jukumu kubwa la kuhakikisha kuwa lengo la Serikali linafikiwa kwa kuhakikisha sekta ya kahawa inabadilika kwa kuongeza ufanisi kwa yale yanayotekelezwa hususani kujikita kwenye juhudi za kuongeza thamani na kuja na mbinu na mipango mipya itakayotoa ufumbuzi wa changamoto kuu zinazoikabili sekta ya kahawa, ikiwa ni pamoja na masuala yanayohusiana na masoko ya bidhaa za zinazotokana na zao hili," amesema.

Amesema, "Lakini pia kumuongezea mkulima maarifa na kumuwezesha kuongeza tija katika uzalishaji wa Kahawa, na kutatua changamoto ya bei ndogo ili kuamsha ari ya kilimo cha kahawa"

Akizungumza Mkurugenzi wa TCB, Primus Kimaryo amesema sekta ya kahawa bado ni himilivu na kwamba wanaendelea na jitihada za kuhamasisha unywaji wa kahawa nchini, ili kukuza soko la ndani kutoka asilima 7 hadi kufikia asilimia 15 ifikapo mwaka 2025/2026.

"Sekta ya kahawa ni sekta himilivu, inapitia mambo mengi, bei zinapanda na kushuka, uzalishaji unapanda na kushuka na ubora unapanda na kushuka, lakini wakulima wetu wameendelea kujishika na zao hili na tunaendelea kusisitiza kwamba, Kahawa inalipa lakini inapaswa kufuata taratibu zote za kilimo na uandaaji wa kahawa bora," amesema.

Kimaryo amesema, "Jukumu kubwa ambalo liko mikononi mwetu ni kuendelea kuhimzana Watanzania kunywa kahawa yetu wenyewe, kwani tunapokunywa kahawa yetu, basi utegemezi wa soko la nje unakua ni kidogo na tunaongeza ajira kwa vijana wetu lakini pia tunaimarisha bei yetu kwa wakulima," amesema.

Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya tamasha hilo, Dennis Mahulu amesema wameendesha mashindano mbalimbali ikiwemo ya uonjaji wa kahawa, uandaaji wa kahawa bora pamoja na uzalishaji bora wa kahawa.

"Tumejikita katika kushirikisha wadau ambapo tulikuwa pia na mashindano lengo likiwa ni kuongeza uelewa na kutambua mchango wa wakulima katika zao la kahawa. Pia kulitolewa mafunzo mbalimbali ambapo watu wameelimishwa kuhusu faida za kahawa kiafya, pia imetolewa elimu ya masoko ya kahawa, utafiti, mabadiliko ya tabianchi na mambo mengine mengi yahusuyo zao hili ili kuimarisha sekta ya kahawa nchini," amesema.