Changamoto nane zinazoikabili sekta ya kahawa

Mwenyekiti wa bodi ya kahawa Tanzania (TCB), Profesa Aurelia Kamuzora akizungumza wakati wa uzinduzi wa Tamasha la kahawa linalofanyika mjini Moshi

Moshi. Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB), imetaja changamoto nane zinazoikabili sekta ya kahawa nchini, huku ikijikita kuboresha miundombinu, kusimamia ubora na kuimarisha soko la ndani la zao hilo, ili kuhakikisha bei inayopatikana haimuumizi mkulima.

Changamoto hizo ni pamoja na ukosefu wa pembejeo za uhakika, magonjwa yanayoathiri zao hilo, miti ya kahawa yenye umri mkubwa, kushuka kwa rutuba ya udongo kwa baadhi ya mikoa, vijana kukimbia kilimo hicho pamoja na mabadiliko ya tabianchi na kwamba, bodi hiyo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, inaendelea kushughulikia changamoto hizo, ili kuongeza uzalishaji na kuimarisha sekta ya kahawa nchini.

Kwa mujibu wa takwimu za uzalishaji wa zao la kahawa nchini, uzalishaji umeongezeka kutoka wastani wa tani 50,000 hadi kufikia tani 85,000 za kahawa kwa mwaka jana na  malengo ni kufikia uzalishaji wa tani 300,000 ifikapo mwaka 2025/26.

Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa TCB, Profesa Aurelia Kamuzora, wakati wa ufunguzi wa tamasha la kahawa kitaifa linalofanyika jana katika eneo la Coffee Curing Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro likiwa na lengo la kuonyesha uhalisia wa uzalishaji wa kahawa, masoko na mnyororo wote wa thamani.

Profesa Kamuzora amesema bodi hiyo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, inaendelea kushughulikia changamoto na matatizo yanayoikabili sekta ya kahawa hapa nchini ili kuimarisha sekta hiyo na kuongeza mapato yatokanayo na zao hilo.

"Bodi kwa kushirikiana na wadau inajitahidi kuyatatua matatizo na changamoto zinazoikabili sekta hii ya kahawa kwani matatizo yaliyopo sasa ni pamoja na kupanda na kushuka kwa bei ya kahawa, kwani bei ya kahawa haipandi kwa pamoja, siku nyingine iko juu, siku nyingine ipo chini, na bei inaposhuka inamfanya mkulima akate tamaa, lakini hili tunalifanyia kazi ikiwa ni pamoja na kuimarisha soko la ndani ili kupunguza utegemezi wa soko la nje," amesema Profesa Kamuzora na kuongeza kuwa;

"Lakini katika tatizo la ukosefu wa pembejeo za uhakika...sasa hivi dunia imebadilika, ni kwamba mlaji anajiuliza ni pembejeo gani imetumika kwenye kilimo ili aweze kununua kahawa yako. Na tumeona ujio wa 'organic cofee' kahawa ambayo inazalishwa bila kutumia kemikali, bei yake inakuwa kubwa kuliko  zile zinazotumia kemikali, hivyo na hili tunaliangalia ili kuona namna ya kuboresha na kusaidia wakulima kulima kilimo chenye tija".

Profesa Kamuzora amesema  "Mnyororo wa thamani wa kahawa una maeneo mengi, kwa hiyo wadau  tunatakiwa kulifanyia kazi hili la vijana kujiingiza kwenye mnyororo wa kahawa, lakini  tunaomba wakulima washirikiane na wadau wote ili tuongeze tija kwenye zao hili, kwani soko la kahawa  ni kubwa endapo tutakuwa tumejipanga na kuhakikisha kahawa inayozalishwa inakuwa bora,"

Mwenyekiti huyo wa bodi amewataka wadau wa kahawa hapa nchini kutumia tamasha  linaloendelea mkoani hapa kutathmini changamoto zinazoikabili  sekta ya kahawa ili kuona ni hatua gani za kuchukuliwa ili kulinusuru zao hilo.
Kaimu Mkurugenzi TCB, Francis Kajiru amesema wataendelea kuhakikisha uzalisha wa zao la kahawa unakuwa na wakulima  wanalima kwa  tija na kwa ubora unaotakiwa kwenye soko la dunia.

"Tunasherekea mafanikio yetu kwamba kwa miaka mitatu iliyopita sekta ya kahawa imeanza kukuwa na kuonyesha mafanikio kwa hiyo sisi kama wadau wa kahawa tutaendelea kufanya vizuri zaidi na matarajio yetu ni kwamba  hapa kuna wataalamu wazuri wa kahawa, tutajifunza vizuri kuhusu kahawa,  upatikanaji wake ikiwa ni pamoja na kuzingatia ubora.

Naye, Mwenyekiti wa jukwaa la wadau wa kahawa nchini, Denis Mahulu amesema wataendelea kuhamasisha unywaji wa kahawa nchini ili kukuza soko la ndani ambapo kwa sasa linatumia asilimia 7 pekee ya kahawa yote inayozalishwa nchini.
Pamoja na mambo mengine amesema watahakikisha kahawa inayonyweka mtaani na kwenye vijiwe inakuwa na viwango vya ubora vinavyokidhi vigezo.