Kamati ya Bunge yapigania madeni taasisi za serikali, Waziri Nape ajibu

Muktasari:

  • Serikali imetakiwa kuhakikisha taasisi zilizochini ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ikiwemo Shirika la Posta, Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), kulipwa madeni yao ya muda mrefu ziweze kujisimamia na kujiendesha kibiashara.

Dar es Salaam. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeitaka Serikali kuhakikisha taasisi zilizochini ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari zinalipwa madeni yao ya muda mrefu ziweze kujisimamia na kujiendesha kibiashara.

Baadhi ya taasisi hizo ni Shirika la Posta, Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).

Maelekezo hayo yametolewa leo Jumapili, Machi 19, 2023 jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Seleman Kakoso ambapo amesema ni vyema Serikali kuhakikisha inasimamia madeni hayo ili mashirika hayo yaweze kukopesheka na kujiendesha kibiashara.

Kakoso pia ameishauri Serikali ihakikishe mkongo wa taifa unaosimamiwa na TTCL unajiendesha kibiashara ili kusababisha mapinduzi katika sekta ya mawasiliano.

Akijibu hoja hiyo, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema Serikali ina mpango wa kuhakikisha madeni yote yanalipwa na tayari wameanza uhakiki wa madeni yanayoweza kulipwa yalipwe na yanayoweza kugeuzwa kuwa mtaji wafanye hivyo.

Pia, wamefanya mabadiliko ya sheria ya posta ili kuwafanya waweze kujiendesha kibiashara sambamba na kuwataka kuwa na ubia na taasisi mbalimbali.

Vilevile alielekeza TTCL na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuweka miundombinu ya mkongo wa taifa kwenye nguzo za za umeme badala ya kufukia ardhini jambo ambalo linaongeza usalama.

"Tumepokea maelekezo ya kamati ya Bunge ya kuharakisha mchakato wa taasisi hizo zijisimamie kibiashara. Kuhusu upatikanaji wa huduma za redio mipakani, tumeelekeza TTCL kushirikiana na watoa huduma za redio kuongeza kasi ya upatikanaji wa masafa ya ndani," amesema Waziri Nape.

Nape amesema mchakato wa kuzifanya taasisi hizo kujiendesha kibiashara unaendelea na ndio maana wamewapa TTCL  mkongo na kituo cha data wasimamie na kujiendesha na   wamefanya mabadiliko ya sheria ya posta ili kuwafanya waweze kujiendesha kibiashara sambamba na kuwataka kuwa na ubia na taasisi mbalimbali.