Kamati ya Seneti ya Marekani yapitisha muswada wa kupitia upya uhusiano na Tanzania
Muktasari:
- Kamati ya Mahusiano ya Nje ya Seneti ya Marekani imepitisha muswada wa kupitia upya uhusiano na Tanzania katika hoja 24 za sheria, hatua inayofungua ukurasa mpya wa uangalizi wa kisera kati ya mataifa hayo mawili.
Dar es Salaam. Kamati ya Uhusiano wa Kigeni ya Seneti ya Marekani imepitisha jumla ya hoja 24 vya muswada wa sheria unaolenga kuimarisha usalama wa taifa la Marekani, kulinda masilahi yake duniani na kupitia upya uhusiano ya nchi hiyo na mataifa washirika duniani, ikiwemo Tanzania.
Hatua hiyo imebainishwa katika taarifa ya pamoja iliyotolewa Jumatano, Juni 17, 2026 na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Seneta Jim Risch akishirikiana na Seneta Jeanne Shaheen, mara baada ya wajumbe wa kamati hiyo kukamilisha kikao kazi na kupitisha muswada huo kwa makubaliano ya vyama vyote viwili.
Miongoni mwa sheria zilizopitishwa na kamati hiyo ni pamoja na muswada wa S.4577 wa "Sheria ya Kupitia Upya Uhusiano wa Pande Mbili kati ya Marekani na Tanzania", uliowasilishwa na maseneta Ted Cruz na Jeanne Shaheen.
“Tunafarijika kuona miswada hii ya vyama vyote ikipiga hatua mbele na kusogea hatua moja katika kulinda vyema masilahi ya Marekani kote ulimwenguni," ilieleza taarifa hiyo ya pamoja.
Baada ya hatua hiyo, muswada huo sasa unakwenda kwenye Bunge la Seneti kupigiwa kura na endapo utapitishwa utakwenda kutiwa saini na Rais wa Marekani.
Mbali na muswada huo unaoigusa Tanzania, kamati hiyo imepitisha sheria nyingine ikiwemo ile ya usalama nchini Sudan, sheria ya kulinda uhuru wa kidini duniani, kupambana na ukiukwaji wa haki za binadamu nchini China, pamoja na wa kuimarisha ushirikiano wa kiteknolojia na kiulinzi katika ukanda wa Indo-Pacific na Taiwan, ili kulinda masilahi ya nchi hiyo duniani.
Muswada unaoihusu Tanzania uliwasilishwa Mei 20, 2026, ukihusishwa na matukio ya uchaguzi mkuu wa Tanzania wa Oktoba 29, 2025, ambapo Marekani ilieleza wasiwasi kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu na kudhoofika kwa misingi ya kidemokrasia.
Katika toleo lake la awali, muswada ulipendekeza tathmini ya kina ya uhusiano wa Marekani na Tanzania katika diplomasia, usalama, biashara na misaada ya maendeleo.
Pia, ulipendekeza kusitishwa kwa baadhi ya misaada ya usalama na maendeleo pamoja na kupitia upya ushirikiano wa kibiashara kupitia taasisi kama Millennium Challenge Corporation (MCC).
Aidha, ulifungua uwezekano wa vikwazo vya viza na kufungia mali kwa watu watakaobainika kuhusika na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu, pamoja na kuhitaji tathmini ya uhusiano wa Tanzania na China na Russia.
Vipengele vyapunguzwa
Hata hivyo, kabla ya kupitishwa, Seneta Shaheen aliwasilisha marekebisho yaliyopunguza ukali wa baadhi ya vipengele, ikiwamo kuondolewa kwa pendekezo la kusitisha ushirikiano wa kijeshi kati ya Marekani na Tanzania.
Pia, marekebisho mapya yaliondoa masharti yaliyohusu misaada ya usalama yakibakiza vikwazo vinavyohusu ufadhili wa maendeleo.
Muswada huo, uliorekebishwa unaendelea kupendekeza kuzuiwa kwa ufadhili wa Shirika la Millennium Challenge Corporation (MCC) kwa Tanzania, hadi masharti maalumu yaliyowekwa yatakapotekelezwa.
Mabadiliko mengine kabla ya muswaha huo kupigiwa kura kwenye bunge la Seneti, ni kuingizwa kwa kifungu kinachoruhusu msamaha kwa kuzingatia masilahi ya taifa la Marekani.
Chini ya marekebisho hayo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani atakuwa na mamlaka ya kuondoa au kusamehe vikwazo vya misaada na uwekezaji, ikiwa ataona hatua hiyo inalinda masilahi ya Marekani. Kifungu hicho hakikuwepo katika muswada wa awali.
Aidha, marekebisho hayo yamebadilisha mfumo wa vikwazo uliopendekezwa. Badala ya kuanzisha mfumo mpya wa vikwazo, muswada huo sasa unapendekeza matumizi ya sheria iliyopo ya Global Magnitsky, kuwachukulia hatua watu binafsi watakaobainika kuhusika na ukiukwaji wa haki za binadamu au vitendo vya rushwa.
Msimamo wa Serikali
Akitoa msimamo wa Serikali bungeni baada ya muswada huo kupelekwa kwenye kamati hiyo, Waziri Kombo alisema: Serikali itachukua njia za kidiplomasia katika kukabiliana na misukosuko inayoibuka ili kulinda mahusiano ya Tanzania na mataifa ya nje.
"Tunawaahidi na mimi nawaahidi… wanaotaka kutumia udhaifu wetu mdogo uliotokezea kuonea, kuinyanyasa, kuikandamiza nchi, tutakwenda nao kwa jibu hili zuri sana la kidiplomasia," alisema.
Alitaja juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan kujenga mridhiano, falsafa ya R4 na uhuru wa kuabudu kama hatua muhimu iliyovutia mataifa mbalimbali kushirikiana na Tanzania katika nyanja mbalimbali.
Kuhusu muswada huo wa maseneta wa Marekani, Kombo alisema wizara itachukua hatua stahiki huku akitoa wito kwa wanaoituhumu Tanzania kwa maovu ya ubaguzi, uonevu kuja Tanzania ili kushuhudia hali ilivyo.
"Kule wanasema tunachinjana, wote wawili hawajawahi kufika Tanzania. Tumeshatuma barua ya kuwaalika waje, tutawalipia sisi gharama zote hadi malazi, waje Tanzania waweze kuona wapi tunachinjana, wapi tunapigana, waone watu wanavyokutana kwenye matatizo, Watanzania tunavyoishi. Tumeshawalika," alisema.
Alisisitiza umuhimu wa kujibu hoja kwa hoja na kuwa Tanzania itaendelea kutumia njia ya kidiplomasia katika kushughulikia matatizo ya kimataifa.
Kombo alisema tayari wamemwelekeza Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Dk Elsie Sia Kanza kufanyia kazi hoja za maseneta hao.
Hata hivyo, alisema kiutaratibu hoja zilizotolewa maseneta hao ndani ya Bunge lao zinatakiwa zijibiwe na wabunge wa Tanzania kama ilivyofanyika.
Kombo alitoa msimamo huo, kufuatia mjadala ulioibuliwa na wabunge wasisitiza uhuru wa nchi kuheshimiwa.
Msimamo huo unaendana na kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyosisitiza Desemba 2025 kuhusu msimamo wa nchi na mamlaka yake.
“Kama nchi isiyofungamana na upande wowote, Tanzania iko wazi kushirikiana na wote wanaoheshimu uhuru wetu na masilahi yetu," alisema Rais Samia.
Aidha, Juni 7, 2026 akiwa nchini Russia, Rais Samia alieleza kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na wadau wote duniani kwa misingi ya manufaa ya pamoja na kuheshimiana.
Walichotaka wabunge
Baadhi wa wabunge ndani ya Bunge la Tanzania wakijadili hoja ya maseneta Jeanne na Ted Cruz, wakitaka heshima kwa uhuru na mamlaka ya nchi kupewa kipaumbele.
Mbunge wa Mtama, Nape Nauye alisema; "Tulipopitia matatizo Rais Samia amesimama imara, ameonyesha uzalendo na hili limepeleka salamu duniani kuwa hata tunapopitia matatizo bado tunaweza kutatua wenyewe changamoto zetu.
"Niiombe wizara, mara kadhaa tuwakumbushe marafiki zetu, tupo tayari kusaidiana nao kama marafiki, lakini nchi hii ipo huru, hatukupewa uhuru wetu kama zawadi, tulipambana tukapata uhuru wetu.
“Tupo huru, tunathamini mchango wao, lakini muhimu wakumbuke, wasitumie changamoto tulizonazo kutuumiza, kutunyanyasa, kutukandamiza, kutudhalilisha; watumie fursa tunayowapa kufanya nao kazi kwa heshima na upendo," amesema.
Mbali na Nape, Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya, alisema Tanzania ina uhusiano wa kihistoria na Marekani hivyo ijitahidi kumaliza tatizo hilo kwa kuheshimu uhuru wa nchi.
"Wasitumie kigezo hicho kutukandamiza kujinufaisha kisiasa. Tulitarajia wenzetu wangewasiliana na kamati yetu ya Bunge kabla ya kuandaa muswada huo ambao unataka kufuta viza kwa viongozi wa Chama cha Mapinduzi ambao wengine ni wahanga, viongozi wetu wa ulinzi ambao hawajapewa nafasi ya kusikilizwa, ni jambo linalokwenda kuharibu uhusiano wetu," amesema.
Naye Elibariki Kingu, mbunge wa Singida Magharibi, alisema Tanzania ni Taifa lisilofungamana na upande wowote akisisitiza kuwa Taifa limejikita kulinda uhuru na mamlaka yake.
"Huo muswada na mimi nimebahatika kuuona... Tusije tukaruhusu heshima ya Rais wetu na nchi yetu ikachezewa na viongozi wetu wakawa wanyonge," amesema.
Hata hivyo, Mbunge wa Tunduru Kaskazini (ACT-Wazalendo), Addo Shaibu alionya kuwa sera ya kutofungamana na upande wowote isitumike kufumbia macho hoja za haki, uwajibikaji na kupinga ukandamizaji duniani.
Shaibu amesema sera ya nchi ya kutofungamana na upande wowote isifanye jamii kukaa kimya kwenye ukandamizaji wa haki.
Aliitaka Serikali kusimama katika kusimamia haki na uwajibikaji, ikipinga dhuluma na uonevu wa mataifa makubwa.