Kanda ya Kaskazini inavyotunza fedha zaidi kuliko kutoa

Ukizungumzia masuala ya fedha hapa nchini, kila eneo lina dhana inayoliruhusu. Kwa mikoa ya Kaskazini ni rahisi kusikia neno wabahili hao, wanaijua pesa au wachakarikaji (watafutaji) wazuri wa pesa.

Hata ripoti ya utafiti wa Finscope mwaka 2023 inayoangazia uzoefu wa wateja, inaonyesha uhalisia huo. Inasema watu wa ukanda huo ni wawekaji wazuri wa fedha benki na kwenye taasisi za fedha kuliko wanavyozitoa, ukilinganisha na maeneo mengine.

Kwa ujumla, asilimia 22 ya Watanzania wenye miaka zaidi ya 16 wanatumia huduma za kibenki kwa sasa na kiwango hicho kimeongezeka kutoka asilimia 17 mwaka 2017.
Ripoti ya mwenendo wa uchumi wa kanda ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inaonyesha kuwa jumla ya amana zote zilizowekwa benki mwaka 2022/2023, zilikuwa ni Sh31.14 trilioni, kati ya hizo, Dar es Salaam iliweka Sh19.22 trilioni, sawa na asilimia 61.7, ikifuatiwa na Kanda ya Kaskazini.

Kwenye Kanda ya Kaskazini ambayo ndani yake kuna mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Tanga na Manyara, thamani ya fedha zilizowekwa benki zilikuwa Sh3.88 trilioni, sawa na asilimia 12.5 huku mikoa ya Kusini Mashariki (Ruvuma, Pwani, Lindi na Mtwara) ikiwa na amana kidogo zaidi ambayo ni Sh914.1 bilioni, sawa na asilimia 2.9.

Ripoti hiyo ya BoT inaonyesha kuwa kwa nchi nzima, miamala iliyofanywa kupitia huduma za benki wakala kwa mwaka 2022/2023 iliongezeka kwa asilimia 26.6, sambamba na thamani yake iliyoongezeka kwa asilimia 46.

Jumla ya miamala 81,646,098 ya kuweka fedha iliyofanyika kupitia huduma ya wakala wa benki ilikuwa na thamani ya Sh66.4 trilioni. Miamala ya kutoa ilikuwa 45,998,973 yenye thamani ya Sh20.44 trilioni.

Takwimu hizo zinaonyesha kuwa watu wengi hutumia zaidi huduma za uwakala kufanya miamala kuliko kufika benki ana kwa ana, lakini pia wengi wanaweka fedha kuliko kutoa.

Katika miamala iliyofanywa kupitia wakala wa benki Kanda ya Kaskazini ilikuwa 12,366,464 ya kuweka yenye thamani ya Sh9.46 trilioni na ya kutoa ikiwa ni 6,634,866 yenye thamani ya Sh2.62 trilioni; ukiwa ndiyo ukanda unaotoa fedha kidogo zaidi benki baada ya Kanda ya Kusini Mashariki iliyotoa Sh1.8 trilioni.

Kwa upande wa kuweka fedha Kanda ya Kaskazini ni ya tatu kwa thamani ya miamala ya kuweka nyuma ya Dar es Salaam na Kanda ya Ziwa. Kwa mwaka 2022/2023 kanda hiyo iliweka Sh9.4 trilioni, Dar es Salaam Sh18.82 trilioni na Kanda ya Ziwa Sh16.60 trilioni.

Hata hivyo, kanda ya Kaskazini inachangia asilimia 10 tu ya mikopo yenye thamani ya Sh25.79 trilioni, iliyotolewa na benki za biashara mwaka 2022/2023, Dar es Salaam iliongoza kwa asilimia 56.7, ikifuatiwa na Kanda ya Ziwa kwa asilimia 13.3 na Kanda ya Kati (Dodoma, Morogoro, Singida na Tabora) kwa asilimia 11.4.

Hali halisi mtaani

Hali ya matumizi makubwa ya huduma za kifedha inajidhihirisha katika mji wa Moshi ambao unakadiriwa kuwa na watu zaidi ya 160,000 (sensa ya 2022) ukiwa na matawi ya benki tofauti zaidi ya 16.

Benki ambazo matawi yake yanapatikana Moshi ni NBC, CRDB, DTB, Exim, Posta, KCBL, KCB, Azania, Equity, ABSA, Mwanga Community, Uchumi Commericial, BOA, NMB, Akiba Commercial, Stanbic na Mkombozi.

Dickson Kavishe, mfanyabiashara wa Mji wa Moshi, anasema uwepo wa benki hizo umekuwa ni msaada mkubwa kwao kutokana na urahisi wa upatikanaji wa huduma za benki na ukaribu pale wanapohitaji huduma hizo.

Miongoni mwa sababu zinazotajwa mji huo kuwa na benki zaidi ya 16 ni wananchi wa mkoa huo kuendesha maisha yao kwa shughuli za ujasiriamali ambazo zinapelekea baadhi ya taasisi za kifedha, zikiwemo benki kuwekeza, zikifuata fursa za wafanyabiashara.

Pamoja na shughuli za kijasiriamali ambazo zinatajwa kuvutia taasisi hizo za fedha, ni uwepo wa mashirika ya kidini, baadhi yake yakimiliki hoteli na taasisi za elimu na hivyo kuwa kichocheo cha benki hizo kuwekeza kwa wingi katika mkoa huo.

Akizungumza na Mwananchi, mdau wa maendeleo kutoka taasisi ya Kilimanjaro Community Achievement, Mwalimu Isaki Ara alisema utamaduni wa wenyeji wa mkoa huo, hasa Wachaga, maisha yao yamekuwa yakijikita katika ujasiriamali na kwamba suala la biashara kwao ni utamaduni, ndiyo sababu inayovutia taasisi za fedha kuwekeza katika mji huo.

"Suala la biashara (Wachaga) hawalazimishwi, wanaona ni sehemu ya maisha, hivyo shughuli za kiuchumi ambazo ni biashara inaweza ikawa ni sababu kubwa inayovutia taasisi za fedha kwa sababu biashara hutegemea fedha na fedha zinahitajika pale uzalishaji unapofanyika," anasema Ara.

Anasema sababu nyingine ni kwamba wenyeji wa mkoa wa Kilimanjaro ambao wameenea maeneo mbalimbali duniani, wanazalisha sana na hivyo wakati mwingine taasisi za fedha zikaona Kilimanjaro iwe sehemu ya uwekezaji.

Anaongeza kuwa wakati wa sikukuu za mwisho na mwanzo wa mwaka ambapo ni kipindi cha Wachaga kurudi nyumbani kusherehekea sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya, ni kipindi ambacho fedha hutumika sana, kwa hiyo kuwepo kwa benki husaidia urahisi wa fedha kupatikana.

Kwa upande mwingine, anasema uwepo wa taasisi za dini, elimu mkoani hapa hasa katika Mji wa Moshi kwa namna moja ama nyingine zinavutia taasisi za fedha kuwekeza katika mji huo.

"Hapa Moshi, kuna taasisi nyingi za dini na kuna madhehebu makubwa ambayo asili yake ni hapa Kilimanjaro, asilimia kubwa hizi taasisi za dini zina miradi mikubwa, unakuta kuna madhehebu ambayo yanamiliki hoteli, taasisi za elimu na miradi mingine mingi ambayo husaidia sana fedha kuzunguka na ndiyo sababu kubwa ya taasisi za fedha kuwekeza hapa," alisema.

Kwa upande wake Dk Meda Mrimi, mtaalamu wa masuala ya uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MUCo), anasema miongoni mwa sababu za mji wa Moshi kuwa na taasisi nyingi za fedha ni za kijiografia.

Mji huo upo jirani na Kenya, hivyo kumekuwa na shughuli nyingi za kibiashara zinazoendelea kufanyika, zipo biashara halali na zisizo halali, zikihusisha magendo na nyinginezo, hivyo hizo zote zinachangia katika mzunguko wa fedha katika mkoa huo.

Sababu nyingine, anasema mkoa huo ni moja ya mikoa ambayo ilikuwa ikizalisha kahawa kwa wingi kwa takribani miongo mitano au sita, na kahawa ilikuwa ikipata bei nzuri kitaifa na kimataifa iliyosababisha mkoa huo kuwa na mzunguko wa fedha kwa nyakati zote.

Wazawa wengi wa Kilimanjaro wako nje ya mkoa wao hata nje ya nchi, wakifanya shughuli za ujasiriamali na nyinginezo na wana mwamko wa kuwekeza nyumbani, hivyo mali nyingi wanazozipata kutoka sehemu mbalimbali waliko, wanazileta nyumbani kwa ajili ya uwekezaji.

Benki nyingine zimekuwa zikitumika hasa kwenye kusafirisha fedha, mfano benki za KCB na ABSA, na hii ni kwamba wazawa wa mkoa huu walioko Kenya wanaitumia kutuma fedha kwa ndugu zao kwa ajili ya uwekezaji na kusaidia ndugu zao kwenye mambo mbalimbali, kama mitaji," alisema.

Pamoja na mambo mengine, anasema wenyeji wa mkoa huo ni wajasiriamali na wanaushirika wazuri.

"Wanasaidiana katika kupeana mitaji na wanaitumia katika kuanzisha biashara mbalimbali, ndiyo maana utakuta kuna Vyama vya Kuweka na Kukopa (Saccos) vingi, na vingine vinafanya kazi kibenki zaidi, vilevile mbali na hivyo kuna vikundi vidogo wanavyocheza michezo ya kupeana fedha (vibati), mambo haya pia yanasababisha mzunguko wa kifedha kuwa mzuri," alisema.

Mchumi Mwandamizi kutoka Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi, Dk Yusuph Kulindwa anasema zipo sababu ambazo zimekuwa zikitajwa kusababisha kuwepo kwa benki nyingi katika Mji wa Moshi, akisema kuwa watu wa mkoa huo wana asili ya biashara tangu zamani, uwepo wa biashara ya utalii, wasomi wengi na biashara nyingine kufanyikia nje ya Moshi.

“Hapa Moshi kuna benki nyingi sana ukilinganisha na miji mingine na inawezekana ndiyo manispaa pekee yenye benki nyingi kuliko nyingine zote hapa Tanzania, takwimu zinaonyesha kwa wingi wa benki, Moshi inashindana na majiji kama Dar es Salaam, Mwanza na Arusha.

“Hili ni jambo ambalo unaweza kuliona kama kizungumkuti, kwani idadi ya watu ni ndogo, lakini benki ni nyingi na zinafanya kazi vizuri na moja ya sababu inaweza kuwa kweli huu mji ni wa zamani ambao umeanza biashara miaka mingi na una mwingiliano mwingi wa watu kutoka nchi jirani kama Kenya.” alisema.

“Sababu ni biashara nyingi za kitalii hapa, lakini bado kuna changamoto, kwani huoni kwa macho shughuli kubwa za kibiashara zikiendelea, biashara ni kidogo lakini mzunguko mkubwa wa fedha kwenye taasisi za fedha au vituo vya kubadilisha fedha, watu wana pilika na benki zinafanya kazi vizuri, lakini biashara halisi huzioni”.

Mmoja wa wakazi wa mji wa Moshi, Josephine Dismas anasema sababu anayoiona ya mji wa Moshi kuwa na benki nyingi ni kwamba Wachaga wengi wanapenda sana sherehe na kwamba sherehe hizo zinaambatana na matumizi makubwa ya vyakula na vinywaji.

Pamoja na mambo mengine, anasema, "Mlima Kilimanjaro umekuwa ukiwavutia sana watalii, huu mlima unaleta watalii, watu mbalimbali, kwa hiyo suala la fedha ni lazima taasisi za fedha ziwekeze ili kuwepo na urahisi wa upatikanaji wa fedha."