Kanisa, Mzee Ismail wanavyogombea ardhi miaka 30

Muktasari:

  • Ni takriban miaka 30 tangu Kanisa la Anglikana na Bakari Ismaili (75), waingie katika mgogoro wa ardhi, ambao hadi sasa hakuna aliyekubali kushindwa.

Dar es Salaam. Imepita miongo mitatu bila mafanikio ya kumalizika kwa mgogoro wa ardhi kati ya Bakari Ismaili (75) dhidi ya Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Babati, Mkoa wa Manyara.

Mzizi wa mgogoro huo ni madai ya Ismaili kwamba alinyang’anywa eneo hilo la ekari tatu analodai lilikuwa la kwake mwaka 1994 na likakabidhiwa kwa kanisa.

Hata hivyo, kanisa hilo limeyakana madai hayo, likisema Ismaili alishashitaki zaidi ya mara tatu mahakamani, lakini zote alishindwa.

Akisimulia madai ya kunyang’anywa eneo hilo, Ismaili amesema mchakato ulianza kwa kuandikiwa barua kuhusu kuchukuliwa kwa eneo hilo na Ofisa Maendeleo wa Ardhi Halmashauri ya Wilaya ya Babati wa wakati huo.

Barua hiyo, amesema aliandikiwa Mei 27, 1994 na ndani yake ilieleza eneo hilo linakabidhiwa kanisa ili kujengwa kituo cha maendeleo ya vijana.

Kwa mujibu wa Ismaili, alilipata eneo hilo mwaka 1974 wakati wa oparesheni ya vijiji na kuliendeleza kwa kupanda mazao ya kudumu ikiwamo miti na migomba.

"Nilinyang'anywa kienyeji mwaka 1994, Mei 26, 1994 niliandika barua ya malalamiko kwa mkurugenzi mtendaji wilaya ambaye alinijibu kupitia afisa maendeleo wa ardhi.

"Barua ile yenye kumbukumbu namba GEN/BBT/VOL.IV/84 ya Mei 27, 1994 ilidai kutambua eneo hilo lenye mashina 50 ya migomba na miti 100, ikisema ni eneo la kanisa.

Ameongeza: "Juni 6, 1994 nilipokea barua ya uthamini wa mimea yangu ambayo barua ile ilidai mimea yangu ipo kwenye eneo la kanisa.

Amesema barua ilimjulisha mthamini wa Serikali atafika Juni 8, 1994 ili kuthaminisha mimea yake ya kudumu hivyo awepo kwenye eneo hilo saa 5:00 siku inayofuata.

"Nilikwenda kama nilivyoelekezwa lakini mthamini hakutokea na hakuna kilichoendelea tena, baadaye nilipeleka malalamiko yangu kwa mkuu wa wilaya ya Babati na mkuu wa mkoa wa Arusha kabla hujagawanywa (sasa ni Manyara) huko nako sikupata ushirikiano,” amesema

Amesema aliendelea kuhangaika kutafuta haki yake hadi Aprili, 23, 2021 alipomuandikia barua ya malalamiko Kamishna wa ardhi wa mkoa.

"Nilijibiwa kwamba Kamishna wa ardhi msaidizi  amemwandikia mchungaji kiongozi wa kanisa yenye kumb namba LD/MNR/01/VOL.3/49 ya Julai 22, 2021, lakini hadi sasa sijapata msaada.

"Nilipeleka malalamiko yangu kwa waziri wa Ardhi (Jery Silaa), Agosti 10, 2022 katika kufuatilia ilipofika Februari 12, 2023 hoja yangu ilipewa usajili namba ST-006-007-05722, baada ya hapo hakuna kilichoendelea, zaidi niliishia kuwekwa lock up (mahabusu) ili nisiendelee kutafuta haki yangu," amesema.

Mchungaji wa Dayosisi hiyo, Frank Chikoti amesema aliukuta mgogoro huo mwaka 2012 alipofika eneo hilo kwa ajili ya kazi ya uchungaji na wameshashitakiwa katika baraza la ardhi mara mbili na zote Ismaili alishindwa.

"Tumewahi kusuluhishwa na wakuu wa wilaya watatu wa hapa Babati kwa nyakati tofauti akiwamo huyu wa sasa. Kimsingi, huyo mtu ametushtaki sio mara moja na kashindwa zote.

“Kuna wakati alivamia kwenye eneo hilo wakamfunga miezi sita, alipotoka akafungua kesi akashindwa, akafungua tena akashindwa kanisa lina vielelezo vya umiliki," amesema.

Mchungaji huyo amesema umiliki wa eneo hilo waliupata mwaka 1994 walipokabidhiwa na mtu aliyemtaja kwa jina la Samson Agunda.

"Sehemu chache ya eneo iliyokuwa imesalia halmashauri ilisema tuwafidie wenye maeneo yao, tukafanya hivyo wakaondoka, japo wakati huo sikuwa mchungaji hapo, lakini vielelezo vya nyaraka hizo zipo na mmoja wa waliofidiwa alikuwa ni jirani wa huyo mzee Bakari.

"Huyo mzee alitia saini kwa mwenzake akipokea malipo, leo hii anakuja kudai kiwanja ni chake, hayo ndiyo yameleta utata ingawa kiwanja ni mali halali ya kanisa na lina hati miliki,” amesema.