Kasi ya matatizo ya ukuaji wa neva, usonji kwa watoto yashtua
Muktasari:
- Wataalamu wataja sababu, wakisisitiza umuhimu wa kumlinda mama mjamzito dhidi ya msongo mkubwa wa mawazo, kazi nzito na mazingira yasiyo salama, wakieleza kuwa hali hizo zinaweza kuathiri ukuaji wa ubongo wa mtoto akiwa tumboni.
Dar es Salaam. Kwa muda mrefu, Joyce Fred aliamini mwanawe wa miaka minne alikuwa na tabia ya ukaidi na uzembe wa kawaida wa kitoto.
Mtoto huyo alikuwa akijikojolea hata akiwa macho, wakati mwingine mbele ya watu, hali iliyomfanya mama huyo kuingiwa na aibu na kuchoshwa na lawama kutoka kwa ndugu na majirani.
“Nilikuwa namkemea sana. Niliamini anafanya makusudi. Nilijiuliza kwa nini mtoto mkubwa kiasi kile anajikojolea ovyo,” anasimulia Janeth, mkazi wa jijini Arusha, kwa sauti ya huzuni.
Lakini changamoto hazikuishia hapo. Anasema mwanawe akiwa shuleni huonekana kuwa mtulivu kupita kiasi, akishindwa kushiriki michezo na watoto wengine na wakati mwingine hukaa peke yake kana kwamba hafahamu kinachoendelea darasani.
“Walimu walikuwa wananiambia mtoto ni mzito kuelewa, hasikii maelekezo vizuri na hapendi kuchanganyika na wenzake. Nilikuwa naumia sana,” anasema.
Katika familia nyingine jijini Dar es Salaam, Rehema Mushi naye alipitia mkanganyiko kama huo baada ya mwanawe kufikisha miaka miwili bila kuzungumza.
Mtoto huyo hakupenda kushikwa na watu wengine, alikuwa na hasira kali mara kwa mara na alionyesha tabia za kujitenga.
“Watu walikuwa wanasema labda nimerogwa au nimemlea vibaya mtoto. Nilipata msongo mkubwa sana,” anasema Rehema.
Kwa upande wake, Asha Omary anasema changamoto kubwa kwa mwanawe ilikuwa kukataliwa na shule nyingi kutokana na kutotulia darasani na kushindwa kushirikiana na watoto wengine.
“Shule nyingi hazikutaka kumpokea. Nilikuwa naelezwa mtoto wangu ana usumbufu,” anasema.
Tatizo kubwa kiafya
Wazazi hao hawakujua kuwa watoto wao walikuwa wakionesha dalili za tatizo kubwa la kiafya lijulikanalo kama usonji na pia ukuaji wa neva yanayotajwa kushika kasi hivi sasa nchini.
Kwa mujibu wa Profesa Karim Manji, licha ya kwamba hakuna sababu moja inayosababisha usonji, tatizo hilo hutokana na mkusanyiko wa sababu mbalimbali zinazoweza kuathiri ukuaji wa ubongo wa mtoto.
“Vinasaba vina nafasi, lakini mazingira nayo yana mchango mkubwa,” anasema.
Anataja mazingira yanayoweza kuongeza hatari kuwa ni matumizi makubwa ya skrini kwa watoto wadogo, kemikali hatarishi pamoja na msongo mkubwa wa mawazo kwa mama wakati wa ujauzito.
Aidha, anasisitiza umuhimu wa mjamzito kupata lishe bora, utulivu wa akili na mazingira salama, ili kupunguza hatari ya matatizo ya ukuaji wa neva kwa mtoto.
“Kinamama wengi wanafanya kazi ngumu, hawapati muda wa kupumzika. Kwa upande wa neva, mama anatakiwa kupata chakula bora. Mjamzito anastahili kupata huduma bora kabisa kadiri ya uwezo wetu,” anasema na kuongeza:
“Mama akiwa kwenye msongo mkubwa wa mawazo au mazingira yasiyo salama, ukuaji wa ubongo wa mtoto unaweza kuathirika.”
Profesa Manji, ambaye ni daktari bingwa wa magonjwa ya watoto na maendeleo ya ukuaji wa ubongo kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas), anasema wakati dunia ikiendelea kushuhudia ongezeko la watoto wenye matatizo ya usonji, hali hiyo pia imeanza kuonekana nchini.
Imeelezwa matatizo ya ukuaji wa neva kwa watoto yapo katika makundi matano makuu, huku usonji ukiwa miongoni mwa changamoto zinazoongezeka kimyakimya.
Makundi hayo ni usonji, mbetuko wa tabia, tatizo la ‘Rett’ la ukuaji wa neva, matatizo ya muunganiko wa ubongo pamoja na matatizo ya ukuaji wa neva yasiyoainishwa moja kwa moja au yasiyo na sifa maalumu za kuingizwa katika kundi fulani.
Anasema makadirio yanaonyesha kuwa mtoto mmoja kati ya watoto 150 hadi 180 walio chini ya miaka mitano nchini anaweza kuwa na dalili za usonji.
“Kama tuna watoto milioni 20 nchini walio na umri wa chini ya miaka mitano, maana yake tuna zaidi ya watoto 140,000 wenye changamoto za usonji na idadi nyingine kubwa ya wenye matatizo ya ukuaji wa neva,” anasema Profesa Manji.
Anasema licha ya kutokuwepo kwa mfumo rasmi wa kitaifa wa kufuatilia watoto wenye usonji, idadi hiyo inaonyesha ukubwa wa tatizo linaloikabili jamii na mfumo wa afya nchini.
Usonji ni nini?
Kwa mujibu wa Profesa Manji, usonji ni tatizo la ukuaji wa ubongo na mfumo wa neva ambalo huanza mapema kabisa katika maisha ya mtoto, mara nyingi kabla hajafikisha miaka miwili.
Anasema watoto wenye usonji huwa na changamoto katika mawasiliano, uhusiano wa kijamii na tabia zinazojirudia.
“Mtoto anaweza kuchelewa kuzungumza, kushindwa kutazama watu usoni, kutopenda kucheza na watoto wengine au kuwa na tabia za kufanya jambo moja mara kwa mara,” anasema.
Anasema baadhi ya watoto huonekana wenye hasira kali, wengine hupendelea kukaa peke yao muda mwingi huku wengine wakionesha uwezo mkubwa wa kukariri vitu au kufanya hesabu kwa haraka.
“Unaweza ukamwona mtoto haongei vizuri lakini ana uwezo mkubwa sana wa akili,” amesema.
Anatoa mfano wa mtoto aliyewahi kumuona hospitalini ambaye alikuwa na uwezo wa kuchora picha kwa usahihi mkubwa baada ya kuiona mara moja tu.
Anasema watoto wengi wenye changamoto hizo huchelewa kugundulika kwa sababu jamii bado haina uelewa wa kutosha.
“Wazazi wengi huamini mtoto ni mkaidi, mbumbumbu, mwenye maajabu au ana laana. Wengine huchelewa kutafuta msaada wa kitabibu,” anasema.
Dalili za awali
Profesa Manji anasema mtoto anapofikisha mwaka mmoja anatakiwa kuanza kuonyesha ishara za mawasiliano kama kupunga mkono, kuonyesha kitu kwa kidole au kuitikia anapoitwa.
Akikosa hatua hizo, mzazi anatakiwa kuwahi kutafuta ushauri wa kitaalamu.
“Utambuzi wa mapema ni muhimu sana. Kadri mtoto anavyopata msaada mapema, ndivyo uwezekano wa maendeleo mazuri unavyoongezeka,” anasema.
Anatahadharisha wazazi kutochanganya usonji na matatizo mengine ya neva kama mtindio wa ubongo au uchelewaji wa kawaida wa ukuaji.
Gharama kubwa za huduma
Licha ya ongezeko la watoto wenye usonji, wataalamu wanasema huduma za uchunguzi na tiba bado ni chache nchini.
Asha Omary anasema familia yake imekuwa ikitumia fedha nyingi kwa ajili ya huduma za tiba ya mazungumzo, matamshi na ujuzi wa maisha.
“Huduma nyingi ni binafsi na gharama zake ni kubwa sana. Si kila mzazi anaweza kumudu,” anasema.
Kwa upande wake, Marko Mwakyusa wa Mbeya anasema changamoto kubwa ni unyanyapaa katika jamii.
“Watu wengine wanawaona watoto hawa kama wenye matatizo ya akili au wasiokuwa na malezi mazuri,” anasema.
Profesa Manji anakiri kuwa Tanzania bado ina upungufu mkubwa wa wataalamu wa kutathimini na kutoa huduma kwa watoto wenye usonji.
“Wataalamu ni wachache sana ukilinganisha na mahitaji yaliyopo,” anasema.
Anasema huduma nyingi pia hazipo kwenye vifurushi vya bima za afya, jambo linalowafanya wazazi wengi kushindwa kuzifikia.
Muhas yaanzisha mafunzo maalumu
Kutokana na ongezeko la changamoto hizo, Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas), kimeanza programu maalumu za kufundisha wataalamu, lengo likiwa kuongeza idadi ya wataalamu watakaosaidia watoto wenye changamoto za ukuaji wa neva.
Profesa Manji anasema kazi za kitafiti zilizofanywa na Muhas zimeonyesha kuwa watoto wanaopata malezi ya kuchangamshwa mapema, huwa na maendeleo mazuri zaidi katika kujifunza na kushirikiana kijamii.
“Mazoezi ya kuzungumza na mtoto, kucheza naye na kumchochea kutumia hisia zake tangu akiwa mchanga, yana mchango mkubwa katika ukuaji wa ubongo,” anasema.
Kwa mujibu wa tafiti hizo zilizofanyika Kigamboni na Temeke, watoto waliopata mazingira ya kuchangamshwa mapema, walionesha maendeleo mazuri zaidi katika kujifunza na kuwasiliana.
Serikali yachukua hatua
Kutokana na ongezeko la tatizo hilo, Serikali imeanza kutoa mafunzo kwa walimu 4,000 wa shule za msingi na sekondari ili kuwasaidia kutambua mapema dalili za usonji kwa watoto.
Mkurugenzi msaidizi wa magonjwa yasiyoambukiza na afya ya akili kutoka Wizara ya Afya, Dk Omary Ubuguyu, anasema mafunzo hayo ni sehemu ya mradi wa majaribio wa mwaka mmoja unaotekelezwa katika shule 100 za Dar es Salaam.
“Mafunzo haya yanawapa walimu maarifa ya kutambua dalili za usonji mapema ili watoto wapate msaada kwa wakati,” anasema.
Anasema walimu wana nafasi muhimu kwa sababu watoto hutumia muda mwingi zaidi shuleni kuliko hospitalini.
Mradi huo unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Afya, Wizara ya Elimu, Wizara ya Maendeleo ya Jamii pamoja na Taasisi ya Lukiza Autism Foundation.
Kwa upande wa walimu, Rehema Musa wa shule ya awali ya Kijitonyama anasema mafunzo hayo yamebadili namna wanavyowaangalia watoto wenye changamoto za kitabia.
“Tulikuwa tunadhani mtoto anayekaa kimya au asiyependa kucheza na wenzake ni mgumu kuelewa. Sasa tunajua inaweza kuwa dalili ya usonji,” anasema.
Wataalamu wanaamini kuwa pamoja na changamoto zilizopo, kuongeza uelewa wa jamii, huduma za uchunguzi wa mapema na elimu jumuishi kunaweza kuwasaidia watoto wengi wenye usonji kuishi maisha bora, kujifunza na kuonyesha vipaji vyao bila kunyanyapaliwa.