Katambi alia na mpango wa urithishwaji ujuzi

Muktasari:

  • Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Vijana na Ajira), Patrobas Katambi amewataka wageni walioajiriwa kwenye miradi mbalimbali kutekeleza mpango wa urithishaji ujuzi kwa wafanyakazi wazawa kama inavyoelekezwa kwenye sheria ya kuratibu ajira kwa wageni.

Dodoma.  Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Vijana na Ajira), Patrobas Katambi amewataka wageni walioajiriwa kwenye miradi mbalimbali kutekeleza mpango wa urithishaji ujuzi kwa wafanyakazi wazawa kama inavyoelekezwa kwenye sheria ya kuratibu ajira kwa wageni.

Katambi ameyasema hayo alipotembelea mgodi wa Barrick uliopo Nyamongo mkoani Mara ikiwa ni sehemu ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa sheria za kazi kwenye maeneo mbalimbali ya kazi mkoani humo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na kitengo cha mawasiliano cha wizara hiyo, Katambi ameeleza kuwa Serikali kupitia ofisi ya waziri mkuu, kazi, vijana, ajira na wenye ulemavu imeendelea kusimamia utekelezaji wa sheria za kazi kwenye maeneo mbalimbali ya kazi.

 “Hivi sasa vibali vya kazi kwa raia wageni vimekuwa vikitolewa hususan kwa wenye ujuzi ambao ni adhimu, na wageni hao wanatakiwa kuhakikisha wanatekeleza mpango wa kurithisha ujuzi kwa wazawa ili waweze kutekeleza majukumu yao baada ya wageni hao kumaliza muda wao wa kazi hapa nchini,” amesema.

Katambi amesema kuna  wimbi kubwa la maombi ya wafanyakazi wa kigeni kwenye maeneo mbalimbali wakitaka kuleta raia wa kigeni ambao kazi zao zinaweza kufanywa na wazawa.

“Yapo baadhi ya makampuni yamekuwa na tibia ya kutokurithisha ujuzi kwa wafanyakazi wazawa ili kukwamisha wazawa wasiweze kuendelea kufanya kazi zinazofanywa  na wageni hao lengo ikiwa kampuni hizo ziendelee kutegemea sana wageni kutoka nje ya nchi,” amesema.

Meneja mkuu wa mgodi huo wa Barrick,  Luiz Correia amesema wamejipanga kuwawezesha Watanzania kwa kuwapatia mafunzo kwenye programu mbalimbali za mafunzo na wapo tayari kushirikiana na Serikali kutatua changamoto ya ukosefu wa ujuzi ambao ni adhimu nchini.