Katambi: Vijana piganeni vita ya uchumi siyo majungu

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Patrobas Katambi

Muktasari:

  • Vijana nchini wametakiwa kutumia muda wao kwa ajili ya kuzalisha badala kuweka akili zao kwenye majungu na uchonganishi.


Dodoma. Vijana nchini wametakiwa kutumia muda wao kwa ajili ya kuzalisha badala ya kuweka akili zao kwenye majungu na uchonganishi.

Wito huo umetolewa leo Jumamosi Juni 4, 2022 na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Patrobas Katambi alipozungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma.

Katambi amesema kuna vijana bila kujali kama muda unawapita wao wanatumia muda huo kuzungumzia mafanikio na changamoto za wengine badala ya kutumia muda huo kuzalisha kwa faida ya nchi yao.

Amewahimiza vijana kufanya kazi zaidi na kuwa na uthubutu kwa wanachokiamini bila kusubiri mjomba ambaye hawamjui lini atakuja kuwasaidia.

Katambi ambaye ni Mbunge huyo wa Shinyanga Mjini amesema huu ni wakati kwa vijana kuishi kwa kutegemea Mungu zaidi ambaye atawaongoza kwenye mapito magumu na mepesi hata waweze kuyafikia malengo.

"Kama mtu anajituma kwenye kazi ataonekana, hakuna kubebwa wala mwenzake na huyo, mfano mimi sijawahi kuwa na mtu wa kunibeba lakini uzalendo umeniweka hapa na ninawashukuru sana mamlaka zilizonipa nafasi hii.

"Vijana amueni kupigana na vita ya uchumi msipigane na vita ya unafiki bali vita yenu mwachieni Mungu atawapigania na kuwapa ushindi mapema iwezekanavyo, lakini fanyeni mambo yenu chini ya Katiba na miongozo inavyotaka," amesema.

Amezungumzia suala la uzalendo kwamba linapaswa kubebwa na kila mmoja ili aisemee nchi yake kuliko kuchafuana kwenye mitandao na vyombo vya habari.

Kuhusu mikopo kwa vijana amesema wamesharekebisha mambo mengi ikiwemo idadi ya wakopaji kutoka kikundi cha angalau watu 10, sasa watano wanaruhusiwa kukopa na mmoja mwenye ulemavu anaweza kukopa.

Kingine amesema sera ya vijana inaendelea kuifanyia kazi ili kusudi ikawe msaada na mkombozi kwa vijana wengi katika kuwaondolea malalamiko.