Katibu mkuu EAC, Balozi Kazungu wajadiliana kuimarisha ushirikiano

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ,Dk Peter Mathuki (kushoto) na Balozi wa Kenya nchini ,Dan Kazungu walipokutana makao makuu ya EAC jijini Arusha leo.

Muktasari:

  • Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC),Dk Peter Mathuki amefanya mazungumzo na Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Dan Kazungu kuhusu mambo muhimu yanayohusu mtangamano ya jumuiya hiyo.

Arusha. Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC),Dk Peter Mathuki amefanya mazungumzo na Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Dan Kazungu kuhusu mambo muhimu yanayohusu mtangamano ya jumuiya hiyo.

Mazungumzo hayo yamefanyika makao makuu ya EAC jijini Arusha leo Jumatano Juni 2, 2021 ambapo Dk Mathuki alitumia fursa hiyo kueleza wajibu wa balozi anayetoka katika nchi mwanachama wa EAC kuhakikisha anawezesha utekelezaji wa ajenda za mtangamano.

“Ninatarajia kufanya kazi kwa karibu na mabalozi wote wanaowakilisha nchi zao wanaotoka nchi wanachama za EAC kuhakikisha tunafanikisha mambo yote yanayohitaji tuyafanyie kazi kwa pamoja,” amesema Dk Mathuki.

Kwa upande wake Balozi Kazungu amesema nchi za Kenya na Tanzania zimeamsha upya ari ya mipango ya mtangamano na wametatua changamoto mbalimbali za kibiashara zilizokuwepo awali.

“Tunaweza kuzungumza kwa ujasiri kuwa changamoto za kibiashara zilizokuwepo kati ya Tanzania na Kenya zimetatuliwa na tumefungua ukurasa mpya,”amesema Kazungu

Amebainisha kuwa nchi hizo zinakusudia kuoanisha sera zinazolenga kuwezesha mtangamano wa EAC kwenda kasi ambazo ni elimu, sayansi na teknolojia, mambo ya nje, afya, usimamizi kwenye mipaka, sekta binafsi, sanaa, utamaduni, sekta ya wanyamapori na utalii.

“Ninayo furaha kuwa maandalizi ya mkutano wa tume ya pamoja kwa ajili ya ushirikiano unatarajiwa kufanyika Julai ambao utajadili kwa kina kuhusu biashara na uwekezaji  baina ya hizi nchi mbili,” amesema Kazungu.