Kauli ya Kimei bungeni yawasha moto jimboni

Wednesday December 01 2021
kaulikimeipic

Raymond Mushi (katikati), aliyejitambulisha kuwa ni mwenyekiti wa wazee wa kabila la wachaga Tanzania, akitoa tamko la wazee hao kulaani kauli aliyodai imetolewa bungeni na Mbunge wa Vunjo, Charles Kimei hivi karibuni kwamba wachaga ni watu wanaopenda magendo. Na Mpigapicha Wetu

By Florah Temba

Moshi. Kauli ya Mbunge wa Vunjo, Dk Charles Kimei kuwa Wachaga wanapenda biashara ya magendo inakiibua kikundi cha wazee jimboni humo na kutoa tamko kali dhidi yake.

Katika tamko hilo, wazee hao wa Kichaga wamelaani kauli hiyo na kwamba wanachukulia kauli hiyo kama matusi kwao na kumtaka Dk Kimei ajitokeza hadharani na kufuta kauli hiyo katika kumbukumbu rasmi za Bunge.

Mbali hilo, wazee hao wameitaka CCM itafakari juu ya kauli hiyo na kumchukulia hatua za kinidhamu mbunge huyo wakidai kuruhusu kauli hizo ni kutawafanya watilie shaka umakini katika kuwapata viongozi.

Hata hivyo, Dk Kimei alipotafutwa alipatikana kwa njia ya Whatsapp hakutaka kuzungumzia suala hilo.

“Una matatizo wewe na mimi?” alihoji Dk Kimei. Alipoelezwa umuhimu wa yeye kueleza upande wake alijibu kwa kifupi, “achana nao” na aliposisitiziwa akasejibu “achana nami”.

Advertisement

Kauli iliyoleta mtafaruku

Kauli iliyoleta mtafaruku Dk Kimei aliitoa bungeni wiki mbili zilizopita wakati akiuliza swali la nyongeza katika Wizara ya Mambo ya Ndani.

“Jimbo la Vunjo mheshimiwa spika ni jimbo lililo mpakani na majimbo yaliyo mpakani yanakuwa na changamoto tofauti kidogo. Kwa mfano magendo unajua Wachaga wanavyopenda magendo,” alisema Dk Kimei alipokuwa akiuliza swali.

“...la pili kule Vunjo unywaji wa gongo, ulaji mirungi, bangi na dawa za kulevya umekithiri kwa sababu watu wengi hawana ajira...nataka tuombe wizara iweze kutueleza inachukua mikakati gani,” alisema.

Wazee wamshukia

Kutokana na maelezo hayo katika swali, kundi la wazee wa Kichaga limeibuka likieleza kusikitishwa na kushtushwa na kauli hiyo na kumtaka mbunge huyo kujitokeza hadharani kuifuta na kuomba radhi.

Mbali na kauli ya “wachaga kupenda magendo”, wazee hao pia walilaani kauli ya mbunge huyo kuwa vunjo unywaji wa gongo, ulaji wa mirungi na matumizi ya dawa za kulevya vimekithiri.

Akizungumza mjini Moshi, mmoja wa wazee hao, Raymond Mushi ambaye alijitambulisha kama mwenyekiti wa wazee wa kabila la Wachaga, alisema kauli hiyo imewatafakarisha na kuwafanya wajiulize maswali mengi.

“Kauli hizi zimetupa mashaka dhidi ya umakini wake na kujiuliza yeye si sehemu ya Wachaga? Angewezaje kututhibitishia kuwa Wachaga tunapenda magendo?” alihoji Mushi aliyeambatana na wazee wengine wanne, wakisema wanawakilisha Wachaga.

“Magendo ni kinyume cha sheria za nchi anaweza kuthibitisha kauli hizo mbele ya vyombo vya dola na sheria?” Sisi kama wazee, kauli hizi zilitushtua sana lakini tulijipa muda tukiamini kwamba angetoa kauli za kutengua kauli hizo”

“Kwa mantiki hiyo kwa niaba ya wazee wote uchagani na jamii ya Wachaga wote, tunalaani vikali kauli hizo na kwamba sisi kama wahusika wa kabila alilolitaja, tunachukulia kauli hizi ni matusi dhidi yetu na kashfa kwetu,” alisisitiza.

Kuhusu unywaji wa gongo, matumizi ya mirungi na dawa za kulevya alisema hiyo si sifa ya jimbo hilo.

CCM Kilimanjaro nao watia neno

Hata hivyo, Katibu wa CCM mkoa Kilimanjaro, Jonathan Mabhiya alipoulizwa, alisema CCM inaheshimu utawala wa sheria ambao umeweka mihimili mitatu ya dola.

“Mimi kama katibu naona sitakuwa nimemtendea haki Dk Kimei kumjadili kutokana na kauli alizozizungumza kwenye moja ya mihimili ya dola.

Advertisement