Kauli ya Serikali ulipaji fidia katika upanuzi wa barabara

Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya akizungumza wakati akijibu maswali kwenye kipindi cha maswali na majibu bungeni jijini Dodoma  leo Ijumaa Aprili 19, 2024.Picha na Merciful Munuo

Muktasari:

  •  Tanroads yafanya uchambuzi wa kina kuepuka mzigo mkubwa wa ulipaji fidia inapoongeza ukubwa wa barabara.

Dodoma. Serikali imesema tathmini iliyofanyika nchini inaonyesha gharama kubwa ya fidia ya mali zilizomo ndani ya eneo la hifadhi ya barabara lililoongezwa la mita 7.5 kila upande,  iko katika majiji na miji.

Hayo yamesemwa leo Ijumaa Aprili 19, 2024 na Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya alipokuwa akijibu swali la msingi la mbunge wa Kibaha Vijijini, Michael Mwakamo.

Mwakamo amehoji Serikali ina mpango gani wa kuepuka mzigo mkubwa wa ulipaji wa fidia wakati inapoongeza ukubwa wa barabara.

Akijibu swali hilo, Kasekenya amesema Serikali kupitia Sheria ya Barabara namba 13 ya mwaka 2007, iliongeza upana wa hifadhi ya barabara kutoka mita 45 hadi mita 60 kwa barabara kuu na za mikoa.

Amesema lengo ni kukidhi mahitaji ya uendeshaji wa miundombinu ya barabara kwa wakati huu na baadaye, ili uendane na ongezeko la watu na ukuaji wa shughuli za kiuchumi.

Kasekenya amesema ili kupunguza ulipaji wa fidia Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), imefanya tathmini ya awali ya gharama inayohitajika kwa ajili ya kulipa fidia kwa mali zilizomo ndani ya eneo la hifadhi ya barabara lililoongezwa la mita 7.5 kila upande.

Amesema  tathmini hiyo imeonyesha  gharama kubwa za fidia ziko katika majiji na miji.

Amesema kutokana na hali hiyo, Serikali inaangalia uwezekano wa kuchepusha barabara kwenye maeneo hayo.

Kasekenya amesema uchambuzi wa kina unafanyika ili kubaini ni barabara zipi zinahitaji upana wa eneo la hifadhi ya barabara wa mita 60 kwa kuzingatia mahitaji ya sasa na ya baadaye, yakiwamo ya kuzipanua kulingana na ongezeko la wingi wa magari. 

Amesema shughuli hiyo ikikamilika taarifa kamili itatolewa.