Kaya 208 zaathiriwa na mafuriko Kyela, misaada yahitajika

Mbunge wa Kyela mkoani Mbeya, Ally Mlaghila akiangalia maji ya mafuriko katika vitongoji vilivyopo Kata ya Katumba Songwe wilayani humo.

Muktasari:

  •  Hali hiyo imesababisha wananchi kuishi kwa hofu huku ikielezwa kwamba mvua zilizonyesha Machi 31, 2024 hadi Aprili 3, 2024 zimesababisha ongezeko la maji Ziwa Nyasa, hivyo limesogea kwenye makazi ya watu. Pia, Mto Songwe umezidiwa maji na kusababisha kaya 208 kuzingirwa na maji.

Mbeya. Wananchi wa vitongoji vinavyozunguka kata ya Katumba Songwe wilaya ya Kyela mkoani hapa wameathiriwa na mafuriko kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.

Imeelezwa kuwa  mvua zilizonyesha Machi 31, 2024 hadi Aprili 3, 2024 zimesababisha ongezeko la maji Ziwa Nyasa, hivyo limesogea kwenye makazi ya watu. Pia, Mto Songwe umezidiwa maji na kusababisha kaya 208 kuzingirwa na maji.

Wakizungumza na Mwananchi leo Aprili 11, 2024, baadhi ya wananchi waliokumbwa na kadhia hiyo wamesema licha ya matukio hayo kujirudia kwenye maeneo yao, mafuriko ya Aprili 3, 2024  yalikuwa hatari na yalileta madhara.

Mkulima wa mpunga na mkazi wa kijiji cha Ndwanga, Ramadhani Mwakalebela amesema hali ni mbaya kwani makazi yake yamezingirwa na maji, amepoteza mifugo na chakula hususani mazao shambani ambayo yamesombwa na maji na kufukiwa na tope.

“Kwa kweli tumeingia kwenye umaskini mkubwa, nilikuwa na mashamba matatu, mpunga umesombwa, lingine umefunikwa na tope zito pia ng'ombe wangu aliyekuwa amezaa, kitoto kimesombwa na maji ya mafuriko,” amesema.

Amesema sababu za mafuriko kujirudia katika eneo hilo ni kingo za Mto Songwe kumeguka ikiwepo sehemu ya maji ya Ziwa Nyasa kuingia kwenye makazi ya wananchi mvua zinaponyesha.

Mwakalebela amesema anakumbuka tukio hilo la mafuriko limetokea usiku wa kuamkia Aprili 3, saa 9.45 alfajiri akiwa amelala. Alisikia mlio wa ng’ombe na kishindo cha sehemu ya nyumba yake iliyomegwa na maji yaliyokuwa yanapita kwa kasi.

“Baada ya kusikia kishindo nilitoka nje, nikagundua tayari mafuriko yameingia. Tulianza kuokoa baadhi ya mali na mifugo na kutupia juu ya paa lakini  vyakula vilikuwa  vimeshaharibika,” amesema.

Christopher Mwafongo amesema mafuriko hayo yamemsababishia umasikini kwani mazao yake kama mpunga, mihogo, migomba na kokoa ambayo aliyategemea kuendesha maisha yake, yamesombwa na maji.

Amesema kwa sasa hana sehemu ya kwenda, bado wanaishi kwenye nyumba zilizojaa maji na wanalazimika kuishi, hivyo hadi Serikali itakapotoa mwelekeo, baadhi yao wamehamia maeneo yenye mwinuko mwambao mwa Ziwa Nyasa.

Kauli ya Mbunge

Mbunge wa Kyela (CCM), Ally Mlaghila amefanya ziara katika kata hiyo na kubaini kaya 208 zimeharibiwa na mafuriko, huku baadhi ya wananchi wakihama makazi yao na kuweka kambi kwenye maeneo ya milima, mwambao mwa Ziwa Nyasa.

Miongoni wa vitongoji vilivyoathirika ni Ndwanga, Bugema na Ilopa vilivyopo kata ya Katumba Songwe.

“Nimefika kujionea hali halisi, sio nzuri kwani kuna kaya 136 kwenye kitongoji cha Bugema na kaya 70 kitongoji cha Ilopa wamekosa makazi baada ya nyumba zao kuzingirwa na maji, hivyo inahitajika nguvu ya ziada kutoka serikalini kwani mafuriko si tendo la kukusudiwa, ni bahati mbaya,” amesema.

Amesema kutokana na changamoto hiyo anaangalia namna ya kuwasaidia kwa kushirikiana na watendaji wa vijiji husika sambamba na kuwasiliana na Serikali, kitengo cha maafa kuona njia mbadala ya kuwasaidia.

“Maeneo hayo yako kwenye ukanda wa Ziwa Nyasa na jirani na Mto Songwe, hivyo mvua kubwa zikinyesha, yanazidiwa maji na kuzingira makazi ya watu, hali ambayo inahatarisha usalama wao,” amesema Mlaghila.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Katumba Songwe, Harod Mwakatundu amesema kufuatia mafuriko hayo, wananchi wamehama makazi yao na kwenda kujenga makambi ya muda mfupi pembezoni mwa Ziwa Nyasa.

“Mvua hii ilianza kunyesha Machi 29 hadi Aprili 3, adha hii imetokana na maji kujaa Ziwa Nyasa na Mto Songwe upande wa Kyela, hivyo tunahitaji misaada ya hali na mali kuwasaidia waathirika,” amesema.

Mtendaji wa kijiji hicho, Lusajo Mwakapiso amesema mbali na mafuriko kuathiri makazi ya watu pia mashamba ya mpunga yamefukiwa na maji.

“Kwa hali ilivyo kwenye mashamba ya mpunga ni mbaya sana, wakulima hawana matarajio ya kupata mavuno kwani maji ni mengi, yametuama na haijukani yatakauka lini,” amesema Mwakapiso.

Kwa upande wake, diwani kata ya Katumba Songwe, Fyuda Syanaloli Msusi amesema mafuriko hayo yameleta athari kubwa kwa wananchi, sambamba na kuharibu miundombinu ya barabara ambazo ni kiungo kwa shughuli za kiuchumi.