KCMC kupokea wagonjwa 900 wa saratani kwa mwaka

Muktasari:
Wagonjwa wa saratani wametajwa kuendelea kuongezeka ambapo Hospitali ya Rufaa ya KCMC huwaona wagonjwa wapya wa saratani 900 hadi 1,000 kwa mwaka.
Moshi. Wagonjwa wa saratani wametajwa kuendelea kuongezeka ambapo Hospitali ya Rufaa ya KCMC huwaona wagonjwa wapya wa saratani 900 hadi 1,000 kwa mwaka.
Hayo yamebainishwa na mtaalamu wa saratani katika Hospitali ya KCMC, Dk Furaha Serventi wakati wa kupokea msaada wa vitu mbalimbali kutoka Benki ya CRDB waliofika kuona wagonjwa wa saratani.
Benki ya CRDB imeadhimisha wiki ya huduma kwa kutembelea wagonjwa wa saratani katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC, ambapo walipeleka misaada ya vitu mbalimbali, zawadi kwa wagonjwa na wafanyakazi kujengewa uelewa juu ya ugonjwa huo.
Dk Furaha ambaye ni mtaalamu wa saratani ya watu wazima amesema saratani inayosumbua zaidi wanaume ni tenzi dume huku kwa wanawake ikiwa ni saratani ya shingo ya kizazi ikifuatiwa na saratani ya matiti.
"Magonjwa ya saratani yanaendelea kuongezeka, na kuongezeka huko kumeonekana kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo uwezo wa kuweza kugundua hizo saratani, kuwepo kwa wataalamu wa ziada wa kugundua hizo saratani lakini pia kuwepo kwa miundombinu ya kugundua hizo saratani" amsemema Dk Furaha
"KCMC tunaona wagonjwa wa aina zote za Saratani za watoto hata wakubwa, na kwa mwaka tunawaona wagonjwa wapya wa saratani 900 kwenda 1,000"
Akizungumza mkurugenzi wa ukaguzi wa ndani CRDB Godfrey Sigalla, amesema kwa mwaka huu katika kuadhimisha wiki ya huduma wameamua kufika KCMC, kuona wagonjwa na kuwapa zawadi, ikiwa ni kuunga mkono jititihada zinazofanywa na hospitali hiyo katika kuwahudumia wagonjwa wa saratani.
"Tumeona tuje KCMC kuona wagonjwa, tumeleta runinga kwa ajili ya wagonjwa, vifaa vya usafi kwa wagonjwa, vifaa vya watoto vya kuchezea pamoja na kutoa zawadi kwa wagonjwa, na kilichotusukuma tuje hapa ni kwa sababu wanatoa huduma nzuri kwa watoto na hata watu wazima hasa kitengo cha saratani"
"Pamoja na kutoa zawadi na vifaa mbalimbali, pia tumekaa nao kujua vitu gani wanatarajia kufanya huko mbele ili pia benki iweze kuona ni jinsi gani inaweza kuwa sehemu ya kufanikisha hilo"amesema.
Wakizungumza baadhi ya wazazi wenye watoto wenye saratani, waliolazwa katika hospitali ya KCMC waliishukuru Benki ya CRDB kwa kuwatembelea na kuwapa zawadi, ambapo walitoa wito kwa wadau wengine kuiga mfano huo kwa kuwa ni sehemu ya sadaka.