Kero ya maji inapogeuka tishio la afya

Recho Shaabani akichota maji katika kisima cha kienyeji kilichopo eneo la Mbezi Makabe jijini Dar es Salaam. Picha na Said Khamis

Muktasari:

  • Siku moja baada ya wakazi wa Mbezi Makabe wilayani Ubungo kueleza namna wanavyotumia saruji na majivu kusafisha maji, wataalamu wameeleza kwa undani.


Dar es Salaam. Siku moja baada ya wakazi wa Mbezi Makabe wilayani Ubungo kueleza namna wanavyotumia saruji na majivu kusafisha maji, wataalamu wameeleza kwa undani.

Suala hilo liliibuka juzi katika hafla ya utilianaji saini utekelezaji wa mradi wa maji wa Mshikamano uliofanyika kituo cha Mbezi Makabe jijini Dar es Salaam.

Mradi huo wenye thamani ya Sh5.4 bilioni unatekelezwa na kusimamiwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa).

Wakati hali ikiwa hivyo baadhi ya wataalamu wa maji akiwemo Mhandisi Herbert Kashilila wa Shirika la Shahidi wa Maji alisema matumizi ya saruji na majivu hayana shida kwa kuwa hayo ndio yanatumiwa kusafisha maji kwenye mito kwenda kwenye matumizi ya binadamu.

“Tofauti ninayoiona hapa ni wananchi kutokuwa na vipimo maalumu kama wanavyofanya wataalamu hivyo kuweza kuwaletea shida wanapokunywa ikiwamo kuumwa matumbo au kuharisha,” alisema mtaalamu huyo.

Theresia John (kulia) mkazi wa Mbezi Makabe akigombea kuchota maji kisimani na Mariam Hamidu baada ya wawili hao kufika kwa pamoja na kila mmoja kudai ni zamu yake. Picha na Said Khamis

Katika ushauri wake, alisema kuna haja ya taasisi za maji au wataalamu wao kutoa elimu ya mara kwa mara kwa wananchi kuhusu njia bora wanazopaswa kuzitumia kusafisha maji wakisubiri utekelezaji wa miradi ya Serikali.

Kashilila alizitaja njia za asili ambazo mtu anaweza kuzitumia kusafisha maji kuwa ni kutumia shabu au mlonge unaoyafanya maji kuwa meupe lakini ili yawe salama inabidi kuyatibu kwa dawa maalumu zilizothibitishwa. Kuna mtungi maalumu wa udongo pia ambao hutumika kusafisha maji.

Mtaalamu mwingine, Dk Edwinus Lyaya wa Heritage Drinking Water inayouza maji ya kunywakwa njia ya mashine kama ATM alisema maji yanaweza kusafishwa kwa mchanga, mionzi ya jua au umeme.

Kwa mchanga alisema unaweza kuweka maji yako kwenye chombo ambacho tayari kina mchanga ambapo baadaye yatajichuja na kubaki masafi juu.

Hata hivyo njia hii alisema ni nzuri zaidi kwa maji yanayotiririka na kufafanua kuwa yakipita kwenye mchanga hubaki meupe.

Kwa mionzi, alisema ndio njia wanayoitumia katika mashine zao za kuuza maji kituo cha mabasi Simu 2000 na Tegeta.

“Maji haya, tofauti na yaliyochujwa kwa mchanga...ni safi na salama kwa kunywa,” alisema.


Adha kwa wananchi

Wakazi wa Mbezi Makabe wanategemea maji wanayochota kwenye mashimo ambayo mengi yamekauka ambako Ally Omary (23) alikutwa kwenye moja kati ya mengi yaliyopo akisubiri maji yapande juu ili aweze kuyachota.

Alisema huwa wanaamka saa kumi alfajiri kuwahi maji kwani ikifika saa nne yanakuwa yameisha.

“Mimi nilileta ndoo usiku nikaziacha kwenye foleni lakini kurudi ndio hivyo nimekuta maji yameisha, inabidi nisubiri yapande. Haya ndio maisha yetu,” alisema.

Julieth Joel alisema licha ya kuyatibu maji hayo kwa saruji wanayoinunua kwa kati ya Sh500 na Sh600 kwa kilo, bado wanatumia sabuni nyingi kwani hayakati povu.

“Nimeishi hapa kwa miaka 23 sasa, hali ni hii. Naiomba Serikali ituondolee adha hii,” alisema Julieth.

Naye Zainabu Rashid alisema nafuu kwao hupatikana kipindi cha masika wanapokinga maji ya mvua kutoka kwenye paa la nyumba au kwenye mitaro na mifereji inayotiririka.

“Maji ya mvua nayo sio salama lakini kwetu yana afadhali kwani kuona maji meupe kwetu ni ndoto,” alisema Zainabu.

Rachel Shabani naye alisema harakati za kutafuta maji husababisha ugomvi ndani ya ndoa. “Imefika mahali wanaume wetu hawatuamini, ukiaga wanakuambia unaenda kudanga na ukirudi nyumbani kumekucha unaambulia kipigo kama unavyoliona kovu hili hapa jichoni limesbabishwa na hizi tabu za maji,” alisema.

Festo Christopher, mwenyeji wa Arusha alikuja Dar es Salaam kumuuguza mwanaye alisema “sikuwahi kudhani Mkoa wa Dar es Salaam unaweza kuwa na tatizo kubwa la maji kiasi hiki.”


Daktari atahadharisha

Daktari bingwa wa magonjwa ya mfumo wa chakula na ini wa Hospitali ya Aga Khan, Masolwa Ng’wanasai alisema saruji na majivu hutumika kusafisha maji, hata hivyo, alionya kuwa saruji inatakiwa kutumika ikiwa imeganda na si vinginevyo.

“Saruji ambayo inatakasa maji ni ile ambayo tayari imeshatengeneza zege ikaganda, inawekwa juu ya maji na kutumika kama chujio la kusafisha maji. Ile ambayo haijaganda ina madhara kwani inaweza kuziba utumbo na kuleta madhara katika mfumo wa chakula,” alisema Dk Ng’wanasayi.

Juzi, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa), Cyprian Luhemeja alikiri uhaba wa maji katika eneo hilo na kueleza kuwa mradi wa Sh5.4 bilioni unaojengwa utaondoa kero hiyo pindi utakapokamilika kwani lita 23,300 zitakazozalishwa kwa siku zitakidhi mahitaji ya wananchi 179,476 waliopo kwa miaka 20 ijayo.

Katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, wananchi walilalamika kwamba wanatumia maji machafu kwa muda mrefu huku wakilazimika kuyasafisha kwa saruji au majivu.

Kuthibitisha uchafu wa maji wanayotumia, Beatrice John alionyesha nepi ya mwanaye iliyofubaa na kidumu cha lita tano kilichokuwa na maji yenye tope.