Kesi ya Malkia wa meno ya tembo kusikilizwa mfululizo

Muktasari:

Watuhumiwa watatu wanadaiwa kupanga na kutekeleza biashara hiyo


Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imepanga Februari 14  na 15, mwaka huu kuendelea na ushahidi wa upande wa mashtaka katika kesi ya uhujumu uchumi na kujihusisha na biashara ya meno ya tembo inayomkabili Salvius Matembo na wenzake wawili.

Mbali na Matembo, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Philemon Manase na raia wa China anayedaiwa kuwa Malkia wa Pembe za Ndovu, Yang Feng Glan (66) ambao kwa pamoja wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi kwa kujihusisha na biashara ya Meno ya Tembo yenye thamani ya Sh13 bilioni.

Wakili wa Serikali Elizabeth Mkunde alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, leo Februari 12, 2018, Huruma Shahidi kuwa shauri hilo lilikuja kwa ajili ya kuendelea na ushahidi lakini mawakili wanaoliendesha wapo Mahakama ya Rufaa wakiendelea na kesi nyingine.

"Washtakiwa wote wapo mbele ya mahakama yako, ila mawakili wanaoendesha shauri hili wapo Mahakama ya Rufaa wakiendelea na kesi nyingine, hivyo tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kuendelea na ushahidi," alidai Wakili Elizabeth.

Washtakiwa wote wanatetewa na mawakili wanne ambao ni  Nehemiah Nkoko, Hassan Kihangio, Alex Mgongolwa na Jamuhuri Johnson.

Awali, wakili wa utetezi Nehemiah Nkoko alidai kuwa upande wa mashtaka walipaswa kutoa taarifa mahakamani hapo kama hawatakuwepo mahakamani hapo jana.

"Mheshimiwa hakimu, kesi hii ni ya muda mrefu tangu mwaka 2014, tunaamini ofisi ya DPP ina mawakili wengi ambao leo wangeendelea kusikiliza shauri hili, kuliko kuendelea kupoteza muda kwa kuahirisha kesi hii, " alidai Nkoko.

Naye mshtakiwa  wa tatu katika kesi hiyo, Yang Feng Glan alinyoosha mkono na kumuomba Hakimu Shahidi kuwataka upande wa mashtaka kuleta mashahidi hata watatu ili kesi hiyo iweze kwisha haraka.

"Mheshimiwa hakimu naomba uzungumze na upande wa mashtaka ili waje na mashahidi wengi na kesi hii iweze kwisha haraka," alidai mshtakiwa Feng.

Baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote Hakimu Shahidi aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 14 na 15, mwaka huu kesi hiyo itakaposikilizwa mfululizo.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa kwa  pamoja wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi kwa kujihusisha na meno ya tembo yenye thamani ya Sh13 bilioni.

Washtakiwa hao wanadaiwa kuwa kati ya Januari Mosi, 2000 na Mei 22, 2014  walijihusisha na biashara  ya nyara za Serikali.

Katika kipindi hicho washtakiwa hao wanadaiwa kufanya biashara ya vipande 706 vya meno ya tembo vyenye uzito wa kilo 1,889 zenye thamani ya Sh5.4 bilioni bila ya kuwa na leseni iliyotolewa na mkurugenzi wa wanyamapori.

Wanadaiwa kuwa kati ya Januari Mosi, 2000 na Mei 22, 2014  kwa makusudi raia wa China, Yang Feng Glan  aliongoza na kufadhili vitendo vya kijinai kwa kukusanya na kusafirisha vipande 706 vya meno ya tembo bila ya kuwa na kibali chochote kile kutoka kwa mkurugenzi wa wanyamapori.

Kwa upande wa washtakiwa Salvius na Manase wanadaiwa kuongoza makosa ya uhujumu uchumi kwa kusaidia biashara ya nyara za Serikali kwa kukusanya, kusafirisha na kuuza meno ya tembo kwa nia ya kujipatia faida.

Ilidaiwa kuwa Mei 21, 2014 katika eneo la Sinza Palestina wilayani Kinondoni mshtakiwa Manase alitoroka chini ya ulinzi halali wa askari wa Jeshi la Polisi D 7847 Koplo Beatus ambaye alikuwa akimshikilia kwa makosa ya kujihusisha na biashara za nyara za Serikali.