Kesi ya Sabaya yakwama tena, augua moyo
Aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya baada ya kushuka kwenye gari la kubebea mahabusu.
Muktasari:
Kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya, leo imeahirishwa tena hadi Novemba 21, 2022 kutokana na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Salome Mshasha kuwa mafunzoni kwa wiki moja.
Moshi. Kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya imeendelea kupigwa kalenda huku Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi, ikielezwa mshtakiwa kwa sasa anasumbiwa na maradhi ya moyo.
Hayo yalijitokeza leo Jumatatu Novemba 7, 2022 wakati kesi hiyo ilipotajwa mbele ya Hakimu Mkazi, Erasto Philly baada ya kuelezwa Hakimu Mkazi Mfawidhi anayesikiliza kesi hiyo, Salome Mshasha yuko mafunzoni kwa wiki moja.
Kutokana na Hakimu Mshasha kuwa na udhuru, hakimu Philly alisema kesi hiyo inaahirishwa kwa siku 14 ili baada ya muda huo wa wiki moja, hakimu huyo atarejea na ataendelea na shauri hilo na Sabaya ataendelelea kuwa mahabusu.
Wakili Hellen Mahuna anayemtetea Sabaya, alisisitiza kesi hiyo kusikilizwa kwa wakati kwani mteja wao ni mgonjwa na anatatizo la moyo na kwamba shauri hilo limechukua muda mrefu. Hadi leo Sabaya amekaa mahabusu siku 160.
Hakimu Philly alisema kesi hiyo imedumu kwa muda mrefu na kuwataka upande wa Jamhuri kama vibali vya kusikilizwa kesi hiyo kutoka kwa mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) vipo tayari ni vyema vikawasilishwa mahakamani.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Novemba 21, 2022 kesi itakapotajwa tena.
Utaratibu wa kisheria ni kuwa, kama vibali vitawasishwa siku hiyo, upande wa mashitaka unaweza kumsomea mshitakiwa maelezo ya awali (PH) kama watakuwa tayari, au kuomba tarehe nyingine itakayotumika kumsomea PH.
Sabaya anakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi inayohusisha kuunda genge la uhalifu, kutumia vibaya madaraka yake na kujipatia Sh30 milioni huku akijua fedha hizo ni zao la uhalifu, kosa ambalo linahusisha utakatishaji wa fedha.
Kwa karibu miezi miwili mfululizo, Sabaya kupitia kwa mawakili wake, Mahuna na Emmanuel Anthony, amekuwa akilalamikia kucheleweshwa usikilizwaji wa kesi hiyo na kuna wakati alimuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuingia kati suala hilo.