Kesi ya Seth, Rugemalira wimbo ni ule ule

Muktasari:

  • Upande wa utetezi katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Habinder Seth na James Rugemalira umeutaka upande wa mashtaka kuharakisha upelelezi ili washtakiwa wajue hatima yao

Dar es Salaam. Upande wa utetezi katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Habinder Seth na James Rugemalira umeutaka upande wa mashtaka kuharakisha upelelezi ili washtakiwa wajue hatima yao.

Washtakiwa hao wanasota rumande kuanzia Juni 19, 2017 tangu walipofikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza na mara zote wanapofikishwa mahakamani, inaelezwa kuwa upelelezi bado haujakamilika.

Seth na Rugemalira wanakabiliwa na mashtaka 12 ya uhujumu uchumi kwa kula njama, kujihusisha na mtandao wa uhalifu, kughushi na kutoa nyaraka za kughushi.

Pia, wanadaiwa kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, kutakatisha fedha na kusababisha hasara ya Dola za Marekani 22,198,544.60 na Sh309,461,300,158.27.

Wakili wa utetezi, Dorah Malaba ameeleza hayo leo Alhamisi Julai 4, 2019 katika mahakama ya hakimu mkazi Kisutu mbele ya hakimu mkazi mkuu,  Huruma Shaidi baada ya  wakili wa Serikali, Wankyo Saimon kudai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

"Tunaomba upande wa mashtaka wajitahidi kuharakisha upelelezi  ili wateja wetu wajue kama  wana makosa au la,” amedai wakili Malaba.

Baada ya maelezo hayo Hakimu Shaidi ameahirisha kesi hiyo hadi Julai 18, 2019 na kuutaka upande wa mashtaka kuharakisha upelelezi.

Washitakiwa hao wapo rumande kutokana na mashtaka yanayowakabili kutokuwa na dhamana.