Kibano cha Waziri Aweso kwa mkandarasi

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akiwa na baadhi ya wakazi wa Mtama. Picha na Bahati Mwatesa
Muktasari:
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amemwagiza mkandarasi anayejenga mradi wa Navanga Kordo, kuhakikisha mradi huo unakamilika ifikapo Februari 26 mwaka huu.
Mtama .Waziri wa Maji Jumaa Aweso ametoa siku 30 kwa mkandarasi anayejenga mradi wa Navanga Kordo uliopo Mtama mkoani Lindi, kuhakikisha unakamilika kwa wakati ili wananchi wapate maji.
Akizungumza jana Ijumaa Januari 26, 2024 Waziri Aweso amesema kuwa hadi ifikapo Februari 26, mradi huo uwe umeshakamilika ili wananchi wapate maji.
Waziri Aweso ameendelea kufafanua kuwa, mradi huo wa Navanga Kordo utakapokamilika utagharimu kiasi cha Sh4 bilioni na utahudumia vijiji vinane katika Halmashauri ya Mtama.
"Nimetoa siku 30, kuanzia leo (jana) kwa mkandarasi anayejenga mradi huo wa Navanga Kordo kuhakikisha unamalizika ili wananchi wapate maji kwani hadi sasa mradi huo umefikia asilimia 90, ni sehemu chache iliyobaki," amesema Waziri Aweso.
Mbali na hayo, Waziri Aweso amewataka wananchi wa Navanga kutunza miundombinu ya maji sambamba na jumuiya ya watumia maji kuhakikisha wanasimamia vizuri miradi ya maji ili kutimiza malengo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kumtua mama ndoo kichwani.
"Nimeona baadhi ya maeneo unakuta kunajengwa miradi mikubwa ya maji, baada ya muda mabomba yanavunjwa. Niwaombe wananchi kutunza miundombinu ya maji, kwani Rais Samia anatoa pesa nyingi kwa ajili ya wananchi wake wapate maji," amesema.
Awali akitoa taarifa kwa Waziri, Meneja wa Mamlaka ya maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa) Wilaya ya Lindi, Mhandisi Idd Pazi amesema kuwa, changamoto waliyonayo ni kukosekana kwa pampu, kwani ya awali iliungua.
Mhandisi Pazi amefafanua kuwa, ifikapo Februari maji yataanza kutoka na wananchi hao watakuwa wameondokana na adha ya kutumia maji ambayo si salama.
"Vijiji vinane vitanufaika na mradi huo ambapo kijiji kimoja kipo katika Wilaya ya Lindi na vijiji saba vipo katika Halmashauri ya Mtama.
“Hadi sasa tumeshajenga vituo 30 vya maji na pia tumeshalaza mabomba kutoka kwenye chanzo cha maji hadi kwenye tangi la maji, changamoto ya pampu tutaikamilisha na wananchi watapata maji ya uhakika," amesema Mhandisi Pazi.
Akizungumzia kero wanayopitia, mmoja wa wananchi wa Mtama, Asha Muanya amesema wanauziwa ndoo moja ya maji kwa Sh500 hadi 700 na wanatembea umbali wa hadi kilometa tano kufuata maji ya chumvi visimani.
"Tunamshukuru Rais Samia kwa kutuletea fedha kwa ajili kijiji chetu cha Navanga, mradi ukikamilika adha ya maji itakwisha," amesema Asha.