Asilimia 78.5 ya vijiji nchini vyapata maji

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso.
Muktasari:
- Waziri wa Maji Jumaa Aweso ameagiza Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa), kushirikiana na maofisa maendeleo ya jamii ili kutunza na kusimamia miradi ya maji kwenye maeneo yao.
Dodoma. Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema kutokana na jitihada zinazofanywa na Serikali katika kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama nchini jumla ya vijiji 9,675 vimepata maji, ambapo ni sawa na asilimia 78.5 ya vijiji vilivyopo nchini.
Aidha amesema vijiji vingine zaidi ya 2,400 vipo kwenye mpango wa kufikiwa huku miradi ya maji 1,500 ikiendelea kutekeleza kwenye maeneo mbalimbali nchini.
Aweso ametoa taarifa hiyo Leo Jumatano, Novemba 8, 2023 wakati akifungua kikao kazi kati ya Ruwasa na maofisa maendeleo ya jamii nchini kilichokuwa na lengo la kulinda na kusimamia miradi ya maendeleo kwenye maeneo yao.
Amesema sekta ya maji ni sekta nyeti ambayo imejaa lawama kwani hata kama watu wakipata maji kila siku hawaongei lakini yakikosekana siku moja wanaanza kulalamika na kuonekana hakuna juhudi zozote zinazofanyika.
"Zamani hali ilikuwa ni mbaya hapakuwa na kiongozi yeyote wa ngazi za juu aliyekuwa anasema mazuri kuhusu Wizara ya maji lakini sasa hivi hali imekuwa ni nzuri kidogo," amesema Aweso.
Amewataka Mameneja wa Ruwasa wa Mikoa kujua miradi yote inayotekelezwa kwenye maeneo yao ili kuondoa sintofahamu inayojitokeza pindi yanapokuja malalamiko ya wananchi kukosa maji.
Amesema kuna baadhi ya maeneo wananchi wanalalamikia huduma ya maji lakini kuna mradi mkubwa wa mabilioni ya fedha unatekelezwa kwenye eneo hilo lakini wananchi hawana taarifa.
"Washirikisheni wananchi kwenye miradi ya maji maana inawahusu siyo wanasubiri Waziri aende akazindue mradi ndipo waanze kutoa kero zao, hakikisheni wananchi wanajua miradi ya maji inayotekelezwa kwenye maeneo yao ili kuondoa malalamiko na maandamano ya kudai maji," amesema Aweso
Aidha amewataka Mameneja hao kuhakikisha kuwa miradi inayotekelezwa inaendana na thamani ya pesa na siyo fedha zinakuwa nyingi kuliko uhalisia wa mradi
Amewataka Maofisa maendeleo ya jamii kutumia ujuzi walionao katika kulinda na kutunza miradi ya maji kwani wao ndiyo msingi wa maendeleo ya wananchi katika maeneo yao.
Amewataka kuwasilisha changamoto zozote wanazokutana nazo katika kuwapatia wananchi huduma ya maji ili zitatuliwe kwa haraka badala ya kusubiri hadi hali kuwa mbaya.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Ruwasa Clement Kivegalo amesema lengo la kikao hicho ni kuona mapungufu ya huduma za maji kwa wananchi kupitia maofisa maendeleo ya jamii ambao wana mchango mkubwa kwenye utekelezaji wa miradi.
Amesema maofisa hao wakikaa vizuri huduma ya maji kwa wananchi itakuwa endelevu kwani kama kuna changamoto yoyote itatatuliwa kwa wakati na kumaliza malalamiko ya wananchi.
Mmoja wa Maofisa Ustawi wa Jamii, Clara Wisiko amesema kikao hicho ni cha kwanza kati yao na Ruwasa hivyo wamejipanga kupokea maagizo ya kwenda kuyatekeleza kwa wananchi ili waondokane na uhaba wa maji.