SADC yamtaja Rais Samia kinara wa nishati safi

Muktasari:
- Hilo limejiri wakati viongozi mbalimbali na wataalamu kutoka nchi nane za (SADC) ambao walikutana jijini Harare nchini Zimbabwe katika mkutano unaolenga kuimarisha na kujadili masuala mbalimbali yatakayowezesha mtangamano wa kikanda katika sekta za nishati na maji.
Dar es Salaam. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametajwa na kupongezwa na mawaziri wanaoshughulikia masuala ya Nishati na Maji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuwa ndiye kinara wa uhamasishaji wa matumizi ya nishati safi ya kupikia Afrika.
Pongezi hizo zimetolewa leo Julai 3, 2025 na viongozi mbalimbali na wataalamu kutoka nchi nane za (SADC) ambao wamekutana jijini Harare nchini Zimbabwe katika Mkutano unaolenga kuimarisha na kujadili masuala mbalimbali yatakayowezesha mtangamano wa Kikanda katika sekta za nishati na maji.
Akizungumza katika mkutano huo, Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amesema kuwa Serikali imeendelea kuwezesha, kuhamasisha na kutoa elimu kuhusu umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kufikia malengo yaliyoainishwa kwenye mkakati wa kitaifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia (2024 - 2034).
Kuhusu utekelezaji wa nishati safi ya kupikia kwa jumuiya hiyo, Kapinga ameitaka SADC kuweka dhamira na mikakati ya utekelezaji wa ajenda ya nishati safi ya kupikia ili kuwafikia watu wengi zaidi SADC.
Amesisitiza SADC kuwa wabunifu katika matumizi ya nyenzo mbalimbali zitakazowezesha na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia huku akitolea mfano matumizi ya mkaa mbadala katika matumizi ya kupikia kama njia ya kuhamasisha matumizi ya nishati hiyo kwa wananchi.
Katika mkutano huo Kapinga ameitaka SADC kuweka nguvu zaidi katika uelimishaji na uhamasishaji wa matumizi ya nishati safi ya kupikia na kuwataka wanachama wa SADC kuweka mkakati utakaowezesha unarahisisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kuwa muhimu kwa uchumi endelevu katika maeneo yao.
Katika hatua nyingine, Kapinga amepokea pongezi zilizotolewa na wanachama wa SADC kwa Tanzania kwa kuandaa, kuwa mwenyeji na kufanikisha mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Nishati wa Afrika (Misheni 300 - M300) kwa ufanisi mkubwa uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Nishati wa Malawi, Ibrahim Matola amempongeza Rais Samia kwa uthubutu wake wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa Watanzania. Matola ameitaka SADC kuitumia Tanzania kama balozi wa matumizi ya nishati safi ya kupikia katika jumuiya hiyo.
Kwa upande wa Tanzania mkutano huo ulihudhuriwa na Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe, Suzan Kaganda, Wataalam mbalimbali kutoka Wizara ya Nishati akiwemo Kamishna Msaidizi wa Maendeleo ya Umeme, Styden Rwebangila na Mkurugenzi Mkuu wa REA, Hassan Saidy.
Wengine ni Mkurugenzi wa Mipango na Uwekezaji (TPDC), Derick Moshi, Mkurugenzi wa Mifumo ya Udhibiti Umeme (Tanesco) , Deogratius Mariwa, Mkurugenzi wa Udhibiti Uchumi (EWURA), Msafiri Mtepa na Wataalamu kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.