Kiini cha matatizo ‘Kwa Mkapa’

Dar es Salaam. Haikuwa siku nzuri kwa mashabiki wa mchezo wa soka nchini na hata nje ya nchi, walioshuhudia kwa mara nyingine, umeme ukikatika katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini hapa.

Hali hiyo ilitokea wakati wa pambano la Yanga dhidi ya Rivers United kutoka Nigeria likiendelea.

Mchezo huo wa Kombe la Shirikisho Afrika ulisimama kuanzia dakika ya 25 kipindi cha kwanza na kuwafanya wachezaji kurejea vyumbani, wakisubiri matengenezo yafanyike na baadaye kurejea na kuendelea na pambano lilioshia kwa sare ya bila kufungana.

Licha ya Yanga kufuzu hatua ya nusu faainali kwa kuwaengua Rivers kwa magoli 2-0 waliyoshinda nchini Nigeria, kilichojitokeza kimeibua maswali mengi kwa mamlaka za usimamizi wa uwanja huo.
 

Si tukio la kwanza

Kabla ya tukio la juzi, Machi 28 mwaka huu, timu ya Taifa ya Tanzania ikicheza na timu ya Taifa ya Uganda kwenye michuano ya kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon), mchezo ulilazimika kusimama baada ya umeme kukatika.

Aidha, tukio la kwanza la kukatika umeme uwanjani hapo, lilishuhudiwa mwaka 2011, wakati Yanga ikikabidhiwa kombe la Kagame baada ya kuinyuka Simba, sherehe ambazo ziliendelea kwa Yanga kukabidhiwa kombe kwa msaada wa taa ya gari la wagonjwa.

Kufuatia tukio la juzi, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezio, Balozi Pindi Chana aliagiza mechi zote zitakazochezwa kwenye uwanja huo, zichezwe jioni.

Pia Balozi Chana aliagiza kusimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi kwa watumishi saba akiwemo Kaimu Meneja wa uwanja huo, Said Mtumbuka. Wengine ni, aliyekuwa mhandisi wa Umeme, Manyori Kapesa na aliyekuwa Ofisa tawala wa uwanja huo, Tuswege Nikupala.

Pia wamo wafanyakazi wa uwanja huo, Gordon Mwangamilo, Gabriel Mwasele, Yanuaria Imboru na Dk Christina Luambano.
 

Kiini cha tatizo

Kama hivyo haitoshi, Waziri Chana alisema baada ya kutokea kwa kadhia ya kukatika kwa umeme baina ya Tanzania na Uganda, alimuelekeza Naibu Waziri, Hamis Mwijuma kukaa na wataalamu kuchunguza tatizo hilo na kupata suluhisho.

Uchunguzi huo ulibaini sababu ya kukatika kwa umeme, ni kutokana na mchanganyiko wa umeme wa jenereta na umeme wa gridi ya Taifa, hivyo wataalamu hao wakapendekeza taa hizo ziwashwe kwa umeme wa jenereta pekee.

Hata hivyo, aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira Tanzania (TFF), Angetile Osiah alisema kuwaondoa watendaji kuna sura tofauti, akisisitiza suala muhimu la kufanya maandalizi kabla ya mechi.

Alisema matukio hayo yana athari kubwa, kwani yanaweza kuwatoa wachezaji mchezoni na kusababisha matokeo mabaya.

"TFF inatakiwa kuwajibika kwenye hili kwani nao wanahusika kwenye maandalizi kwa ujumla, lazima maandalizi yafanyike mapema ili kujua wapi pana shida na nini kifanyike kwa haraka zaidi," alisema.

Tukio hilo limetokea ikiwa ni takribani wiki tatu zimepita tangu Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere, awasilishe ripoti yake ya uchunguzi kwa mwaka 2021/22 bungeni jijini Dodoma na kubainisha upungufu kwenye uwanja huo na ule wa Uhuru.

CAG Kichere alibaini miundombinu na vifaa kuwa duni, viti kuvunjika na kutokarabatiwa, hali inayoweza kuwakatisha tamaa mashabiki kuhudhuria mechi na hata kuathiri mapato.

“Matengenezo yasiyotosheleza, uangalizi duni wa uwanja kutokana na kutokuwepo kwa mpango wa matengenezo wa mali ambao umesababisha usalama kuwa mdogo kwa sababu viyoyozi havifanyi kazi vizuri. Usambazaji wa maji na mfumo wa usafi haukufanya kazi kwa njia inayoridhisha,” alisema

CAG alipendekeza menejimenti ya wizara husika kuweka mpango wa matengenezo na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa usalama ili kuboresha usalama wa viwanja, ili kuvifanya vidumu miaka mingi na kuokoa upotevu wa mapato.

Aidha, matukio hayo mawili ya hivi karibuni yameibua gumzo kwa wachambuzi wa masuala ya michezo, wataalamu wa umeme, uchumi wakisema yaliyotokea yameitia Tanzania aibu na dosari kiuchumi.

Mtaalamu wa umeme kutoka Dar es Salaam Raymond Haule alisema kumeliletea taifa aibu, kwani kilichotokea kimeonyesha uongozi wa uwanja huo namna usivyokuwa na umakini.

“Kama umeme ulikuwepo kama Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) lilivyoeleza kwamba ulikuwepo, jenereta tu ndio limeshindwa kufanya kazi... wakati jenereta lingetumia dakika moja umeme kurudi, kwanini umeme ukae dakika 20 hadi 30 haujarudi,” alisema
Sasa ukisema umeme umefeli unatumia dakika zote hizo kutatua tatizo ina maana hakukuwa na njia nyingine, jenereta lipo, umeme upo kama moja imesumbua kwanini usiweke upande wa pili kwa haraka..? alihoji.

Haule alisema kwasasa duniani mifumo ya umeme ipo nyingi za kisasa ambazo watu wanaweza kutumia kupitia umeme wa jua (sola) akishauri ni vyema uwanja wa Mkapa uwanze kutumia miundombinu hiyo.

Kwa upande wake, Greyson Mgonja ambaye ni mchambuzi masuala ya siasa na maendeleo alisema, tukio la kukatika kwa umeme uwanjani si tu kumeliletea aibu taifa, bali kulitia dosari kiuchumi.

“Tanzania imeomba kuanda mashindano ya Afcon sasa yaliyotokea yanatia hofu kama kweli tuna miundombinu ya kutosha,uwanja wa Mkapa ndio kiwanja kikubwa cha kisasa tuliyonayo sasa linapotokea mambo haya kidiplomasia tumepata dosari kwasasa mpira ni biashara,” alisema.

Mgonja alisema ili kuwavutia wawekezaji nchini jambo la kwanza mwekezaji analoliangalia ni uwepo wa umeme wa uhakika na utawala bora.

Alisema kilichotokea uwanja wa Mkapa ni matunda ya kutokuwepo kwa umakini katika utendaji akisisitiza kukatika umeme uwanjani kwa nyakati mbili tofauti, hatua za kusitisha vibarua vya wasimamizi wa uwanja ulipaswa kuanza mara moja tukio la kwanza lilipotokea.

Naye mtaalamu wa masoko ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini alisema, tukio lile kibiashara lina athari kwa wenyeji wa mchezo kwani muda ungefika kisheria ushindi ungekuwa wa Rivers.

Alisema kuwa bado kazi ni kubwa kuhakikisha vifa bora na vinapatikana ili kufanya uwanja uwe kwenye hadhi nzuri na kuwavutia wateja ambao ni mashabiki kufika kwani wanapata wanachotaka.

"Afcon inaweza kufanyika 2027 kama marekebisho yatafanyika kwa wakati unaopasawa na maandalizi mazuri kila mechi."Alisema Ofisa Masoko.
 

Usuli

Kabla ya kutokea kwa matukio hayo mawili ya kukatika umeme uwanjani hapo, mwishoni mwa Februari mwaka huu, Shirikisho la Soka Afrika (CAF), lilishauri uwanja huo kutotumika kwenye mechi zao kutokana na kuharibika eneo la kuchezea agizo ambalo ilifutiwa na tangazo la uongozi wa uwanja kuufunga kupisha marekebisho.

Machi mosi, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alifanya ziara uwanjani hapo na kuiagiza Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kuanza haraka ukarabati uwanja huo ili ukidhi mahitaji ya CAF baada ya kuufanyia ukaguzi.

“Ili mradi CAF wametupa onyo, ni onyo ambalo wametupa na muda wa kufanya marekebisho na muda huo waliotupa ni lazima tuanze jambo ndipo waridhie mambo mengine yaendelee, nimekuja kuwaambia msiruhusu uwanja huu umefungwa na CAF na kuzipeleka timu zetu zikacheze ugenini,”alisema Majaliwa.