Kijana amuua mama wa kambo akidai amemroga

Kijana amuua mama wa kambo akidai amemroga

Muktasari:

  • Grace Chacha (67), mkazi wa kijiji cha Guta Wilaya ya Bunda mkoani Mara amefariki dunia baada ya kukatwa mapanga na mwanaye wa kambo, Matiku Chacha akidaiwa ni mchawi.

Bunda. Grace Chacha (67), mkazi wa kijiji cha Guta Wilaya ya Bunda mkoani Mara amefariki dunia baada ya kukatwa mapanga na mwanaye wa kambo, Matiku Chacha akidaiwa ni mchawi.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Mara,  Daniel Shillah amethibitisha kutokea kwa tukio hilo huku akiahidi kutoa taarifa baada ya kupata maelezo ya kina.

Akizungumzia tukio hilo mtoto wa marehemu, Joseph Chacha amesema tukio hilo lilitokea Aprili 22, 2021 saa 4 asubuhi katika kijiji cha Guta.

Amebainisha kuwa mama huyo anadaiwa kuuawa na kijana huyo aliyekuwa akiishi jirani na Grace, na kwamba kabla ya tukio hilo mtuhumiwa huyo anadaiwa kutamka  maneno ya vitisho kwa marehemu akimtuhumu kuwa chanzo cha yeye kuwa na maisha magumu.

Chacha amesema kuwa siku ya tukio mama yake akiwa anatoka shambani alikutana na Matiku aliyeanza kumshambulia kwa mapanga sehemu mbalimbali.

"Alimkata na panga kwenye mkono wake wa kulia kisha begani baadaye akamkata maeneo mbalimbali mwilini..., alimkata puani na kutenganisha sehemu ya chini ya macho na pua kisha kuendelea kumkata kichwani  hadi akapoteza fahamu,” amesema.

Chacha amesema mama yake hakupata msaada wa haraka kwa kuwa kitendo hicho kilitokea asubuhi na watu wengi walikuwa shambani akidai wivu ndio chanzo cha kijana huyo kufanya tukio hilo.

" Alikuwa anasema mama yetu ana maisha mazuri kwa sababu watoto wake wote wana kazi nzuri na wanamjali na kudai kuwa yeye ana maisha magumu kwa sababu mama yetu amemloga wakati sio kweli,” amesema.

Mwenyekiti wa mtaa wa Ihale, Marwa Mataga amesema, “sijawahi kushuhudia tukio la kikatili kama lile, yaani mama huyu aliuwawa kikatili sana alikatwakatwa kama mnyama nilipofika pale alikuwa bado anapumua lakini hakuwa na uwezo wa kuongea kutokana na hali aliyokuwa nayo.”

“Nitoe wito kwa vijana kuachana na hizi imani potofu na wafanye kazi kwa bidii ili waondokane na umasikini kuliko kukaa bila kujishughulisha  na kuanza kulaumu watu kwa uzembe wao wenyewe," amesema Mataga