Kikwete: Jibuni maswali kwa ufasaha

Rais mstaafu wa Tanzania, Jakaya Kikwete

Muktasari:

  • Rais mstaafu wa Tanzania (2005-2015), Jakaya  Kikwete ni miongoni mwa wananchi ambao tayari amehesabiwa katika Sensa ya Watu na Makazi iliyoanza saa 6:01 usiku wa leo Jumanne, Agosti 23, 2022 huku akiwahimiza wananchi kutoa taarifa sahihi.

Dar es Salaam. Wananchi wametakiwa kuhakikisha wanajibu kwa ufasaha maswali wanayoulizwa na makarani wa sensa ili Serikali iwezekupanga mipango yake kutokana na mahitaji ya wananchi pamoja na kufahamu maendeleo yaliyofikiwa na Watanzania kwa sasa.

Wito huo umetolewa na Rais mstaafu wa Tanzania, Jakaya Kikwete baada ya kuhesabiwa katika makazi yake eneo la Kawe jijini Dar es Salaam, leo Jumanne, Agosti 23, 2022.

Kupitia matangazo ya moja kwa moja yanayorushwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), ameonekana Kikwete akiwa na mkewe mama Salma wakitoa tarifa kwa karani wa sensa aliyefika katika makazi yao.

Kikwete ametolea mfano sensa ya mwaka 2012 wakati yeye akiwa mkuu wa nchi, kulikuwa na maswali yaliyolenga kufahamu idadi ya nyumba za nyasi na bati zilizokuwepo kipindi hicho.

“Ni swali ambalo unaweza kushangaa kwa nini linaulizwa lakini linatumika kupima maendeleo tuliofikiwa,” amesema.

Hivyo, ametoa rai kwa wananchi kujitokeza kwa wingi na kutoa ushirikiano kwa makarani wa sensa kwani ni muhimu kwa maendeleo ya nchi kwa ujumla.

“Shabaha ya sensa ni kujua idadi ya watu ili Serikali iweze kupanga mipango yake kulingana na mahitaji ya makundi mbalimbali yaliyopo katika jamii,” amesema.

Kabla ya Kikwete mapema leo Jumanne, Rais Samia Suluhu na Makamu wake, Dk Philip Mpango walihesabiwa kila mmoja akiwa katika kaya yake.

Sensa ilioanza kufanyika leo inakuwa ni ya sita kufanyika tangu muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964 na inatarajiwa kufanyika kwa siku saba.