Kilichojificha kuhusu aliyemuua Sheikh Karume

Dar es Salaam. Leo imetimia miaka 52 tangu alipouawa kwa kupigwa risasi Rais wa kwanza wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Sheikh Abeid Amani Karume, Ijumaa ya Aprili 7, 1972 katika mazingira na sababu za kutatanisha.

Vyombo mbalimbali vya habari Tanzania na duniani wakati huo vilimtaja Luteni Humud Muhammed Humud kuwa ndiye aliyetekeleza mauaji hayo akishirikiana na wengine ambao baadaye walipigwa risasi na vikosi vya usalama au kujiua.

Jarida ‘African Events’ la Agosti 1992 lilidai kuwa Humud alikufa papo hapo ‘…katika mazingira ambayo bado hayajaeleweka ...’ Serikali ilisisitiza kwamba mauaji hayo yalikuwa sehemu ya njama ya kuipindua.

Lakini Humud alikuwa na nia yake kibinafsi ... baba yake alikamatwa miezi michache baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya 1964 na Humud alipokuwa akifanya mazoezi baadaye katika Umoja wa Kisovieti aliambiwa kwamba baba yake alikuwa ameuawa ... Humud alikuwa ameapa kulipiza kisasi.”

Ingawa simulizi ziko nyingi, ni wachache waliobakia ambao wanaweza kueleza nini hasa kilitokea siku ile na namna kilivyotokea, hata kama hawataeleza sababu ya tukio hilo.

Machapisho mengi yamesimulia kilichotokea siku na saa ile, lakini katika maeneo fulani fulani kuna kupishana.

Hata hivyo, baadhi ya marejeo yanakubaliana katika maelezo yake kuhusu tukio hilo.

Miongoni mwa marejeo hayo ni kitabu 'The Afro-Shirazi Party Revolution 1964-1974' kilichoandikwa na Kamati Maalumu ya TPDF chini ya mwenyekiti wake, Kanali Seif Bakari Omar, ambacho pamoja na mambo mengine kimezungumzia kwa kina mauaji ya Karume. Kitabu hicho kinawataja wauaji kama ‘wasaliti’.

Saa 12:05 ya siku ile Sheikh Karume aliuawa kwa kumiminiwa risasi katika tukio la kusikitisha lilitokea katika Makao Makuu ya chama, Kisiwandui.

Wauaji walifika wakiwa ndani ya magari mawili, moja liliingia kupitia upande wa kusini, na lingine kaskazini.

Gari la mwanzo lililokuwa linamilikiwa na Serikali ya Mapinduzi (SMZ) lilikuwa na namba ya usajili 'SZ 490' na maandishi ya MBM katika kibati chake cha namba.

Lilikuwa likitumiwa na Khamis Abdallah Ameir, ambaye wakati huo, alikuwa Mjumbe wa Baraza la Mapinduzi. Baadaye alituhumiwa kwa mauaji ya Karume.

Gari hilo likiwa limebeba watu watatu pamoja dereva wake, lilijongea kidogo kidogo kuelekea Makao Makuu ya Chama likifuatiwa na gari lingine.

Liliingia ndani kutokea upande mwingine tofauti na kusimama karibu sana na lile gari la mwanzo mbele ya Makao Makuu ya chama.

Mara tu baada ya gari hilo kusimama, abiria waliokuwamo walishuka ghafla na kuanza kuwashambulia kwa risasi walinzi wa Sheikh Karume waliokuwa nje ya jengo. Mmoja wao alingia ndani ya jengo na kumkuta Sheikh Karume na viongozi wengine wa chama ukumbini wakiwa wamekaa kuizunguka meza ya viti sita.

Karume alikaa katikati ya viti vitatu vya mwanzo akiuelekea mlango wa kuingilia. Kiti cha karibu yake kilikuwa kimekaliwa na Mstahiki Meya ambaye kwa wakati huo alikuwa ameenda msalani akikiacha kiti chake wazi. Sheikh Muhiddin Ali Omar, kiongozi wa chama aliyefahamika vizuri, na mbunge, alikaa katika kiti cha tatu. Viti vingine vitatu vya upande mwingine vilikuwa vimekaliwa na Mheshimiwa Shah Kombo, Mweka Hazina wa chama na mbunge aliyekaa mkabala na Mzee Karume; Sheikh Thabit Kombo, Katibu Mkuu wa chama na Mwenyekiti (Waziri) wa Biashara na Viwanda; na Sheikh Ibrahim Saadalla, kiongozi mwingine wa chama na mbunge.

Wakati huo Sheikh Karume alikuwa akizungumza na wenzake wakati wakimsubiri Mzee Mtoro Rehani Kingo arudi ili waendelee kucheza draft na dhumna ndipo muuaji aliingia na kuanza kumimina risasi sehemu zote. Mlengwa mkuu alikuwa ni Hayati Karume ambaye alikuwa ameshambuliwa kwa risasi kutoka shingoni hadi kifuani na kuanguka.

Hatimaye madaktari walieleza kwamba kuna uwezekano mkubwa kuwa kifo kilimkuta pale pale.

Wakati huo huo muuaji alimuelekezea bunduki Sheikh Thabit Kombo aliyejinusuru kwa kujificha chini ya meza. Risasi iliyompata Ibrahim Saadalla kwenye kidevu chake ilitokea upande wa pili.

Risasi iliyokusudiwa kulenga kichwa cha Sheikh Kombo, kwa bahati nzuri, ilipeperusha kofia yake bila kumwathiri. Viongozi wote hawa walianguka chini ya meza.

Wakati yote haya yakitokea ndani ya jengo, mashambulizi makali yaliendelea nje ya jengo.

Walinzi waliojeruhiwa hawakuruhusu wauaji wengine kuingia ndani ya jengo, na walijibizana nao risasi kwa risasi.

Hata hivyo, wauaji hawakuwa na huruma, na mpango wao wa kikatili waliutekeleza kwa ufanisi mkubwa kwa kuwafyatulia risasi viongozi hao.

Hata hivyo, walinzi wa Rais Karume walifaulu kuwazuia wauaji kuendelea na majaribio mengine ya mauaji na hatimaye kuwafanya wakurupuke na kukimbia kwa kutumia magari yao na kumwacha mmoja wao peke yake akifyatua risasi ovyo ndani ya jengo la ASP.

Muuaji aliyesalia peke yake ndani ya jengo la ASP, akiwaona watu wote wamelala sakafuni, kwa kudhani kuwa wameshakufa, alirudi kinyumenyume hadi katika mlango wa kuingilia

Kutokana na mambo yalivyokuwa wakati huo, mmoja wa walinzi wa Rais alijitokeza ghafla kutoka alipokuwapo na kufanikiwa kuingia ndani ya jengo la ASP.

Baada ya kumwona muuaji akirudi kinyumenyume kuelekea mlango wa kuingilia, mlinzi huyo alimpiga risasi.

Muuaji alianguka kwenye kizingiti cha mlango na kufa papo hapo; walinzi watatu nje ya jengo walijeruhiwa; wengine walinusurika. Sheikh Karume na wengine waliojeruhiwa waliondolewa na kupelekwa hospitali ambako madaktari walifanya kila walichoweza kwa muda wa dakika 45 wakijaribu kunusuru maisha yake bila mafanikio.

Hata hivyo, madaktari walifanikiwa kuokoa maisha ya majeruhi wengine.

Waliotajwa kuhusika na mauaji hayo ni Luteni wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Humud Mohamed Humud ambaye moja ya risasi kutoka kwenye bunduki yake ndiyo iliyohitimisha uhai wa Mzee Karume.

Wengine walikuwa ni askari mwingine wa JWTZ, Kapteni Ahmada Mohamed; koplo wa jeshi ambaye jina lake halikutajwa na raia mmoja aliyejulikana kwa jina la Ali Khatibu Chwaya, ambao kwa mujibu wa taarifa za kiulinzi na usalama waliuawa na walinzi wa Rais katika eneo la tukio wakijaribu kutoroka mara baada ya mauaji.

Mwaka 2001 Profesa Haroub Othman aliandika insha yenye kurasa 148 inayoitwa 'Babu: I Saw the Future and it Works', katika ukurasa wa 49 wa insha hiyo ameandika, "Karume aliuawa na Humud ambaye baba yake aliuawa na utawala wa Karume."

Kitabu 'Maisha Yangu' cha Khamis Abdulla Ameir kilichotajwa hapo juu, kuhusu mauaji ya Karume, katika ukurasa wa 184 kinasema: "Inasemekana kuwa Humud alifanya hivyo ili kulipiza kisasi kuuliwa kwa baba yake."

Jarida 'Tanzanian Affairs' la mwaka 1995 linasema Mohammed Humud, ambaye ni baba yake Humud Mohammed Humud, alikuwa amehukumiwa kifungo cha maisha gerezani lakini akaachiwa mara baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12, 1964. "Lakini baadaye mwaka huo alitiwa kizuizini bila kushtakiwa na akauawa baadaye."

Kitabu 'Mwalimu Julius Kambarage Nyerere' cha mwaka 1977 kilichoandikwa na William Edgett Smith, katika ukurasa wa 156 kinaandika hivi: "...Luteni kijana ambaye jina lake lilikuwa Humud Mohammed Humud, alikuwa na kisasi kingine cha binafsi. Wakati Karume alipowafungulia wafungwa, Humud aligundua kwamba baba yake ambaye naye alikuwa ameshtakiwa alikuwa ameuawa."

Vyovyote vile, kinachojulikana kwa hakika hadi sasa ni kwamba Rais wa kwanza wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Sheikh Karume, aliuawa kwa kupigwa risasi Ijumaa ya Aprili 7, 1972.