Kilimanajro kutoa chanjo ya polio kwa watoto 474,000
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu akizungumza wakati wa uzinduzi wa chanjo ya polio awamu ya tatu. Picha na Janeth Joseph
Muktasari:
Kwa mujibu wa shirika la afya duniani (WHO), ugonjwa wa polio uliripotiwa kulipuka upya nchini Malawi Februari mwaka huu, hii ni baada ya WHO kutangaza Agosti 2020 kwamba bara la Afrika halikuwa tena na ugonjwa huo.
Moshi. Mkoa wa Kilimanjaro unatarajia kutoa chanjo ya polio kwa watoto 474,000 huku wazazi na walezi wakitakiwa kutoa ushirikiano kwa maofisa afya watakaopita majumbani kuwachanja watoto wao.
Hayo yamebainishwa leo Septemba 3, 2022 wakati wa uzinduzi wa chanjo ya polio mkoani humo ambapo wataalamu wa afya watapita nyumba kwa nyumba kuchanja watoto wenye umri kuanzia 0 hadi miaka mitano.
Akizungumza kwenye uzinduzi huo, mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amewaomba viongozi wa dini kuisemea vizuri chanjo hiyo kutokana na baadhi ya wananchi kuwa wapotoshaji wa chanjo zinazotolewa hapa nchini.
“Niwaombe viongozi wa dini kuhakikisha mnalisema vizuri jambo hili,kwasababu kuna baadhi ya watanzania wenye tabia ya kupotosha mambo, mlisemee vizuri jambo hili,hakuna serikali yoyote duniani ambayo inataka kumpa mwananchi wake sumu,hicho kitu hakipo.
“Hivyo niwaombe viongozi wa dini mkatusaidie sana kuhakikisha mnalisemea vizuri jambo hili,tunahitaji jamii ishiriki kikamilifu katika zoezi hili la utoaji wa chanjo na kutoa ushirikiano kwa wachanjaji watakaopita katika mitaa na nyumba zao kwa lengo la kuhakikisha watoto wote wanapatiwa chanjo,” alisema Babu.
Babu amesema asitokee mtu wakuzuia watoto wasipate chanjo hiyo huku akisisitiza watoto ndiyo taifa la kesho na kwamba ni muhimu wakapata chanjo ili kuepuka madhara makubwa yanayoweza kuwapata.
“Kamwe asiwepo mtu wakazuia mtoto yeyote asipate chanjo, watoto hawa wakipata chanjo wakikuwa vizuri ndio taifa la kesho, ni muhimu wakapata chanjo ili kuepuka madhara makubwa yanayoweza kumpata mtoto, niwahakikishie wananchi chanjo zote zinazotolewa ni salama,” alisema.
Naye mganga kuu wa mkoa huo, Jairy Khanga amesema kwenye mzunguko wa awamu ya pili mkoa huo uliweza kuchanja watoto 338,000 sawa na asilimia 113 ya lengo na kwamba mzunguko huu wa tatu ambao umeanza Septemba Mosi wanatarajia kuchanja watoto 474,000 sawa na asilimia 140 ya lengo la kitaifa.
“Safari hii ya awamu ya tatu, serikali iliona kuna baadhi ya watoto hawakupata chanjo wakaona tufanye kampeni nyingine ya mzunguko wa tatu ambayo imeanza Septemba Mosi hadi Septemba 4 mwaka huu na mkoa huu lengo lake ni kuchanja watoto 478,000 kwa kutambua kuna mwingiliano mkubwa wa wananchi na watoto,” amesema Dk Khanga.
Kwa upande wake, ofisa mradi mpango wa Taifa wa chanjo, Dk Mwendwa Mwenesi amesema ugonjwa huo unapotokea huathiri nguvu kazi ya taifa kwani unapompata mtoto unapelekea ulemavu na hata kifo.