Kilio cha wabunge kuhusu Tanapa chasikika sasa kukusanya, kutumia fedha zake

Muktasari:
- Hatimaye Serikali imekubali maombi ya wabunge na wadau wa sekta ya utalii kwa ahadi ya kufanya mabadiliko katika Sheria ya Fedha, ili kuruhusu mashirika mawili kukusanya na kutumia fedha zake.
Dodoma. Bunge limepitisha bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka 2025/26 huku Serikali ikisema katika Sheria ya Fedha ya mwaka 2025 kutakuwa na mabadiliko yatakayowezesha mashirika mawili kukukusanya na kutumia fedha (rentetion).
Mashirika hayo ni Shirika la Hifadhi la Taifa (Tanapa) na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), makusanyo yao yalianza kwenda katika Mfuko Mkuu wa Serikali kwa Sheria ya Fedha ya Mwaka 2020.
Hayo yamesemwa leo Mei 19,2025 na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Pindi Chana wakati akihitimisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka 2025/26.
Bunge limeiidhinisha Wizara ya Maliasili na Utalii Sh359.98 bilioni katika mwaka 2025/2026 kwa ajili ya utekelezaji wa vipaumbele 10 huku Sh105.74 bilioni zikiwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Akihitimisha bajeti hiyo, Dk Pindi amesema lazima kuwa na retention
kwa kuwa katika maeneo ya utalii yanahitaji marekebisho mbalimbali ikiwemo madaraja.
“Sasa kama hamna retention, tutasubiri OC (matumizi ya kawaida) na tunashukuru kwa political will (utashi wa kisiasa) na maelekezo sasa Tanapa na NCAA kutakuwa na retention ,”amesema.
Amesema wameshajadili jambo hilo kwa kina na sasa watatoa mapendekezo hayo katika Sheria ya Fedha ya mwaka 2025.
“Kutakuwa retention kwa mashirika yetu haya ya Tanapa na NCCA na baadaye tunavyoendelea tutaangalia jinsi tunavyoweza kuwa na retention kwa mashirika mengine,”amesema.
Mwenyekiti wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Timotheo Mnzava wakati akiwasilisha maoni ya kamati yake kuhusu makadirio hayo alielezea changamoto hiyo ya mashirika hayo kutobakia na makusanyo yake kama ilivyokuwa awali.
Amesema kutokana na hilo, Tanapa na NCAA yamepata changamoto ya kujiendesha katika maeneo ya kutolea huduma kwa watalii na kushindwa kufanya shughuli za uhifadhi kwa ufanisi.
“Hali hii inachangia watalii wengi nchini kushindwa kufika katika vivutio vingi kwa wakati. Kamati inaitaka Serikali kurejesha utaratibu wa Tanapa na NCAA kukusanya na kutumia ili kuwezesha taasisi hizi kujiendesha kwa ufanisi,”amesema.
Suala hilo pia lilizungumziwa na Mbunge wa Moshi Mjini (CCM), Priscus Tarimo ambaye amesema ripoti ya Mthibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) ya mwaka 2023/24 inaonyesha kuwa fedha za miradi ya maendeleo zilitakiwa kwenda Sh28 bilioni katika Mamlaka ya Ngorongoro, lakini kwa mwaka huo iliambulia sifuri
“Kwa Tanapa kwa ujumla wake ilitakiwa iende Sh23 bilioni lakini Sh1 bilioni tu, mheshimiwa spika wanasema kuwa ng’ombe anayekamuliwa hachinjwi, ng’ombe anayekamuliwa analishwa vizuri,”amesema.
Tarimo amesema fedha hizo haziendi kama inavyotakiwa na hivyo kuua mashirika hayo na kuwa uwepo wa barabara mbovu si kwamba unamtesa mtalii bali hata magari ya wafanyabiashara yanaharibika.
Amesema licha ya miradi ya maendeleo kusimama lakini kuna suala la ulinzi, hivyo kutaka Serikali kuchukua hatua ya kuhakikisha fedha zinakwenda kama zilivyopitishwa na Bunge.