Kilio kwa wanafunzi waliofutiwa mitihani

Kilio kwa wanafunzi waliofutiwa mitihani

Muktasari:

Siku moja baada ya Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) kutangaza kufuta matokeo ya wanafunzi 1,059 waliofanya mtihani wa darasa la saba Oktoba mwaka huu kwa kufanya udanganyifu, wazazi na wadau wameiangukia Serikali kwa kuiomba kutoa nafasi nyingine kwa watoto hao waliokumbwa na mkasa huo.

Dar/mikoani. Siku moja baada ya Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) kutangaza kufuta matokeo ya wanafunzi 1,059 waliofanya mtihani wa darasa la saba Oktoba mwaka huu kwa kufanya udanganyifu, wazazi na wadau wameiangukia Serikali kwa kuiomba kutoa nafasi nyingine kwa watoto hao waliokumbwa na mkasa huo.

Juzi wakati akitangaza matokeo ya darasa la saba Katibu Mtendaji Necta, Dk Charles Msonde alieleza kuwa watahiniwa walioadhibiwa sawa na asilimia 0.1 ya watahiniwa wote, hawatapata nafasi nyingine ya kurudia mtihani huo.

Wazazi na wadau jana waliiambia Mwananchi kuwa kimsingi kuwa wanafunzi hao wameathirika wakati hawahusiki.

Sambamba na kufutiwa matokeo kwa watahiniwa hao pia baraza limezifungia shule 38 zilizofanya makosa mbalimbali ikiwamo kuiba mitihani, kugawa majibu kwa wanafunzi na kubadilisha watahiniwa kwa kuwaweka wasio halisi ili kuwafanyia mitihani wanafunzi watoro.


Wazazi wanasemaje?

Wazazi wa wanafunzi wa waliohitimu darasa la saba katika shule za Ng’arita na Nyawa Wilaya ya Bariadi wamesema uamuzi wa kufuta matokeo ya mitihani ya wanafunzi wa shule hizo umewakatisha tamaa na kuwatia hofu ya watoto wao wa kike kuolewa badala ya kuendelea na masomo.

Akizungumza na Mwananchi jana, kuhusu uamuzi wa kufuta matokeo ya mitihani katika shule hizo, Masalu Machibya ambaye mtoto wake wa kike ni kati ya waliofutiwa matokeo katika Shule ya Msingi Ng’arita alisema uamuzi huo huenda ukarejesha nyuma juhudi za elimu kwa watoto wa kike katika jamii za wafugaji.

“Nilijiandaa kumpeleka mtoto wangu shule ya sekondari kutokana na juhudi zake darasani, ndoto hiyo imekufa baada ya matokeo yake kufutwa. Akikaa nyumbani nahofia atarubuniwa na kutoroshwa na wanaume. Nimechanganyikiwa,” alisema Masalu.

Agnes Paschal ambaye mtoto wake ni kati wahitimu wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Nyawa, alisema hatua hiyo imeathiri hadi wanafunzi wenye bidii ya masomo.

“Sio wazazi, walimu wala wanafunzi wote wanaoshiriki vitendo vya udanganyifu; wapo wasiohusika. Uwepo mfumo mzuri wa kuwatambua na kuwaadhibu waliohusika pekee,” alisema Agnes.

Kauli hiyo iliungwa mkono na mzazi mwingine, Hamis Rajab, ambaye mtoto wake amefutiwa matokeo kwenye shule ya Chabutwa mkoani Tabora, aliyetupa lawama kwa walimu na wazazi wachache wanaoshiriki njama za kufanya udanganyifu katika mitihani.

“Mpwa wangu ni mmoja kati ya wanafunzi waliothirika na uamuzi huo wa kufuta matokeo,” alisema Rajab


Kauli ya wadau

Akizungumza na Mwananchi jana, mwalimu Ezekiah Oluoch alieleza pamoja na uamuzi huo kuchukuliwa kama onyo, alishauri ni vyema Serikali ikaangalia mustakabali wa maisha ya watoto hao.

“Katika hali ya kawaida baraza limetekeleza sheria lakini adhabu waliyopewa watoto hawa ni kubwa. Ingewezekana wangezuiwa kufanya mtihani kwa muda wa mwaka mmoja au miwili lakini sio kuwafungia maisha,” aliongeza.

Kwa upande wake, mchambuzi wa masuala ya elimu, Faraja Kristomus alisema vitendo hivi vinatokea kwa sababu elimu sasa imekuwa na ushindani, mfano kwenye shule binafsi udanganyifu unafanyika kwa lengo la kuzitangaza shule zionekane zimefaulisha,” alisema Kristomus.

Upande wa shule za Serikali, Kristomus alieleza huenda msukumo ukawa wa maofisa wa elimu wa kata na halmashauri ili shule za maeneo yao zing’are.

Naye Rais wa Chama cha Walimu Tanzani (CWT), Leah Ulaya alisema Serikali iangalie namna ya kuwatafutia utaratibu wa kufanya tena mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi ili safari yao ya elimu isiishie hapo.

“Kama uongozi wa chama cha walimu na wazazi tumesikitishwa na hili lililotokea na tunalaani walimu waliohusika na udanganyifu,” alisema Leah.

Wakati wadau wakitoa maombi hayo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Tekinolojia, Dk Leonard Akwilapo alisema walichofanya Necta ni kutekeleza sheria kwa lengo la kukomesha vitendo vya udanganyifu.

“Hiyo ni sheria na Necta wametekeleza sheria inavyoelekeza, sasa kama inaonekana haiko sawa kwa sababu wale ni watoto, hayo yatakuwa maamuzi ya wadau. Ina maana darasa la saba hawajui udanganyifu?” alihoji Dk Akwilapo.

Imeandikwa na Elizabeth Edward, Samira Yussuf na Robert Kakwesi.