Kilo 453 za dawa za kulevya zateketezwa

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dk Yahya Nawanda (wakwanza kulia) akipokea Mwenge wa Uhuru kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Amos Makala ( kushoto) makabidhiano yalifanyika wilayani Busega mkoani Simiyu. Picha na Samirah Yusuph.

Muktasari:

Kati ya kilo hizo, 386.94 ni za mirungi na kilo 66.4 zilikuwa za bangi huku jumla ya watuhumiwa 58 wakikamatwa na 20 kati yao wametiwa hatiani.

Busega. Jeshi la Polisi Mkoa wa Simiyu katika kipindi cha Julai 2022 hadi Juni 2023 limekamata watuhumiwa 58 wa dawa za kulevya kati yao, 12 ni wa makosa ya mirungi na 48 ni makosa ya bangi.

Akitoa taarifa ya mkoa kwa kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2023 wilayani Busega, leo Julai 21,2023 Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Dk Yahya Nawanda amesema kilo za dawa za kulevya 453.34 zilikamatwa na kuteketezwa.

"Watuhumiwa 48 wa dawa za kulevya aina ya bangi na mirungi walifikishwa mahakamani kwa kukabiliwa na kesi za makosa hayo ambapo 20 wametiwa hatiani na 28 mashauri yao yanaendelea katika hatua mbalimbali," amesema Dk Nawanda

Amesema jitihada zinaendelea kuchuliwa ili kudhibiti dawa za kulevya ikiwa ni pamoja na kufanya doria na misako, kuweka vizuizi na kupekua magari hasa yatokayo nchi jirani na kutoa elimu kuhusu madhara ya kutumia dawa za hizo.

Katika Mkoa wa Simiyu Mwenge wa Uhuru utakimbizwa kilomita 769.1 katika Halmashauri sita, ukikagua, kuweka mawe ya msingi na kufungua miradi ya maendeleo yenye thamani ya Sh10.8 bilioni katika sekta ya afya, elimu, maji, kilimo, barabara na maendeleo ya jamii.

Kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa, Abdalla Kaim Shaibu amewataka viongozi kuwa watiifu kwa Mwenge wa Uhuru huku akiwataka kutimiza ipasavyo itifaki hiyo ya kitaifa.