Kilombero, Ulanga kupata umeme wa uhakika

Meneja wa Mradi na usimamizi kutoka Wakala wa Nishati Vijijini(REA) Mhandisi Romanus Lwena akionyesha waandishi wa habari baadhi ya vifaa vilivyokamilika na kufungwa tayari katika kituo Cha kupokea, kupoza na kusambaza umeme Ifakara wilayani Kilombero. Picha na Lilian Lucas,
Muktasari:
- Kukamilika kwa ujenzi wa kituo cha kupokea, kupoza na kusambaza umeme cha Ifakara (Ifakara Substation), sasa kunazifanya wilaya za Kilombero na Ulanga mkoani Morogoro, kupata umeme wa uhakika na hivyo kuondokana na changamoto ya kukatika mara kwa kwa mara kwa nishati hiyo.
Morogoro. Wakala wa Nishati Vijijini (Rea), umekamilisha mradi wa ujenzi wa kituo cha kupokea, kupoza na kusambaza umeme cha Ifakara (Ifakara Substation), huku ukiwahakikishia wakazi wa wilaya za Kilombero na Ulanga, kuondokana na tatizo sugu la kukatika kwa umeme.
Meneja wa mradi na usimamizi kutoka Rea, Mhandisi Romanus Lwena, ameyasema hayo leo Agosti 31, 2023 mjini Ifakara, wilayani Kilombero, wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Amesema azma ya Serikali kupitia Rea katika kutekeleza mradi huo, ilitokana na changamoto ya umeme mdogo waliyokuwa wakiipata wananchi wa maeneo hayo, na kwamba ikawepo dhamira ya kutatua tatizo hilo ili shughuli za kijamii na kiuchumi ziweze kufanyika bila kuwepo kwa changamoto hiyo.
Awali wananchi hao walikuwa wakipata changamoto ya upatikanaji wa umeme mdogo na wenye kukatika mara kwa mara.
“Kwa sasa tumehitimisha zoezi la kuunga kituo hiki kwenye Gridi ya taifa...changamoto ya umeme mdogo imesababisha hali ya uwekezaji katika wilaya hizi kuwa chini,” amesema.
Aidha amesema kukamilika kwa mradi huo wenye uwezo wa MVA 20 wa msongo wa Kilovoti 220, kumetokana na mikakati mahsusi ya Serikali inayolenga kuhakikisha wananchi wote wanapata umeme wa uhakika hata wale waishio vijijini.
“Changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara sasa itaisha, wananchi sasa wataweza kufanya shughuli za ujasiliamali kwa ajili ya kukuza uchumi wao na kujiongezea kipato kwa mwananchi mmoja mmoja,” amesema.
Meneja mradi kutoka kampuni inayojenga kituo hicho, Faisal Hleei, amesema kwa sasa wapo katika hatua ya mwisho ya umaliziaji na wanaangalia na kukagua vifaa vyote kimoja hadi kingine wakiwa na wahandisi wa Tanesco na Rea.
“Tunaamini hadi sasa mambo yanakwenda vizuri na tunamalizia hatua za mwisho na tunatarajia kumaliza kazi ndogo ndogo na sasa wafanyakazi kwa kushirikiaña na Tanesco tunamalizia kazi zote muhimu," amesema.
Ujenzi wa kituo umegharimu Euro 8.75 milioni ambayo ni sawa na Sh22 bilioni zilizotolewa na Serikali kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya (EU).