Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kina Sabaya waweka pingamizi

Muktasari:

Mawakili wa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya na wenzake watano wameweka pingamizi la awali katika kesi ya rufaa waliyofunguliwa na Serikali.

  

Arusha. Mawakili wa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya na wenzake watano wameweka pingamizi la awali katika kesi ya rufaa waliyofunguliwa na Serikali.

Leo Jumanne Desemba 13,2022 mawakili hao wamewasilisha hoja mbili za pingamizi hilo wakidai rufaa hiyo namba 155/2022  haiko sawa kisheria na kuomba itupiliwe mbali.

Wakili Mosses Mahuna ambaye anamwakilisha Sabaya amewasilisha hoja hizo kwa niaba ya mawakili Fauzia Mustafa na Fridoli Bwemelo.

Katika rufaa hiyo namba 155/2022 mbali na Sabaya wajibu rufaa wengine ni Enock Mnkeni, John Aweyo, Sylvester Nyegu, Jackson Macha na Nathan Msuya.

Mbali na Sabaya mjibu rufaa mwingine ambaye alikuwepo mahakamani hapo ni Nyegu ambaye anawakilishwa na wakili Sylvester Kahunduka.

Muomba  rufaa katika shauri hilo aliwakilishwa na jopo la mawakili wa Serikali watano ambao ni Patrick Mwita, Abdallah Chavula, Hebel Kihaka, Felix Kwetukia na Timotheo Mmari.

Leo Mahakama hiyo imeanza kusikiliza rufaa hiyo ambayo Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) anapinga hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, iliyowaachia huru Sabaya na wenzake waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 27/2021.

Wakili Mwita aliieleza mahakama jana Desemba 12, 2022 walipokea notisi ya pingamizi la awali toka kwa wakili Mahuna.

Katika hoja ya kwanza, wakili Mahuna amesema rufaa hiyo imewasilishwa nje ya muda ambapo inapingana na matakwa ya kisheria, kifungu cha 379(1) b cha Sheria ya Mwenendo wa makosa ya jinai ambacho kinataka rufaa ikatwe siku 45 tangu watu waachiwe au siku maamuzi/hukumu imetolewa.

Wakili Mahuna alidai kifungu hicho kinaeleza wakati wa kuandaa rufaa namna ya kuhesabu hizo siku 45 kutoka siku ya uamuzi, muda utakaotumika katika kupata nakala za mwenendo na hukumu inayokatiwa rufaa, muda huo utaondolewa katika siku hizo 45.

Alieleza kuwa hukumu ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha ilitolewa Juni 10, 2022 na rufaa iliyoletwa mahakamani hapo inaonekana ilipelekwa Oktoba 28,2022 baada ya miezi minne na kuwa rekodi walizonazo inaonyesha waomba rufaa walipata nakala ya hukumu na mwenendo wa kesi Septemba 14, 2022 ila rekodi za mahakama zinaonyesha walipewa Septemba 13,2022 na baada ya kupewa wamewasilisha Oktoba 28,2022 hivyo maombi ya  rufaa yamewasilishwa baada ya siku 58.

Hoja ya pili, wakili huyo alidai kuwa notisi ya rufaa inatofautiana na maombi ya rufaa yaliyowasilishwa mahakamani kwa sababu mjibu rufaa namba tatu hayupo kwenye maombi ya rufaa yaliyowasilishwa mahakamani Oktoba 28,2022.

Wakili Mahuna alidai kuwa notisi ya nia ya kukata rufaa DPP alieleza anategemea kukata rufaa dhidi ya watu saba akiwemo aliyekuwa mshitakiwa wa tatu Watson Mwahomange ila katika maombi ya rufaa hayupo hivyo kufanya idadi ya wajibu rufaa kuwa sita badala ya saba.

Akijibu hoja hizo Wakili Mwita aliiomba mahakama kutupilia mbali pingamizi hilo la awali na kuwa nyaraka hizo zilizopo mahakamani hapo zimekidhi matakwa ya kisheria.

Alidai kuwa pingamizi hilo linaegemea sehemu ndogo ambayo ni tafsiri ya kisheria kutoka kwa wajibu rufaa ambao wametafsiri kuwa muda wa rufaa unaanza kuhesabiwa mara baada ya hukumu inayokatiwa rufaa amekosea na badala yake  muda wa kukata rufaa unaanza kuhesabika baada ya kukabidhiwa nakala ya hukumu na mwenendo wa kesi.

Kuhusu hoja pili ya Mwahomange, wakili huyo alieleza kuwa notisi ya rufaa inaanzisha maombi ya rufaa yenyewe na huwezi kujua sababu za rufaa hadi apate mwenendo na hukumu na kuzipitia wakaona hawana haja ya kumuunganisha Mwahomange.

"Nyaraka zote zilizopo mbele ya mahakama zimefuata matakwa ya kisheria  na hatujui kutokuwepo kwa Watson kwenye rufaa hii kunaathiri vipi haki ya waliokatiwa rufaa,hakuna haki imekiukwa na hatuwezi kuchaguliwa watu wa kukatia rufaa,sisi ndiyo tunaamua nani tumkatie rufaa,"aliongeza

Naye wakili wa Serikali mwandamizi, Abdallah Chavula aliunga mkono hoja za wakili Mwita na kuiomba mahakama isitilie hoja hizo maanani na ione rufaa hiyo imekidhi vigezo vya kisheria.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili Jaji Maghimbi  ameahirisha rufaa hiyo hadi kesho Desemba 13, ambapo atatoa uamuzi mdogo juu ya pingamizi hilo.

Awali Juni 10,2022 Hakimu Patricia Kisinda aliwachia huru Sabaya na wenzake sita waliokuwa wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi na kudai ushaidi uliotolewa na Jamhuri ulighubikwa na utata,hivyo kushindwa kuthibitisha mashitaka yaliyokuwa yakiwakabili na kuwatia hatiani.