Kinachojiri mahakamani kesi ya kina Mbowe

Muktasari:

Kesi hiyo ya uhujumu uchumi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe na wenzake watatu wanaotuhumiwa kwa makosa ya ugaidi inaendelea muda huu ambapo shihidi wa sita upande wa mashtaka anatoa ushahidi

Kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe na wenzake watatu wanaotuhumiwa kwa makosa ya ugaidi inaendelea kuunguruma katika Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi leo Alhamisi Novemba 4, 2021.

Mahakama hiyo inapokea ushahidi wa upande wa mashtaka kutoka kwa shahidi wa sita.

Hapa ni sehemu ya kinachoendelea ndani ya mahakama hiyo baada ya Jaji kuingia:


Jaji Joachim Tiganga ameingia mahakamani na kesi inaanza kuitwa.

Washtakiwa wanapanda kizimbani na waendesha mashtaka wanajitambulisha wakiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Robert Kidando

Mawakili wa Utetezi wakiongozwa na Wakili Peter Kibatala wanajitambulisha

Wakili wa Serikali Kidando: Mheshimiwa Jaji shauri linakuja kusikilizwa na leo tuna shahidi mmoja na tuko tayati kuendelea

Shahidi amefuatwa

Sasa shahidi anaingia mahakamani na anapanda kizimbani

Jaji anamhoji shahidi utambulisho

Shahidi wa Sita: Naitwa SSP Sebastian Madembo (46), Mhehe, Ofisa wa Polisi, Mkristo.

Sasa shahidi anaapa kiapo cha kusema ukweli

Shahidi ataongozwa na Wakili w Serikali Mwandamizi Pius Hilla.

Shahidi: Naitwa SSP Sebastian Madembo. Naishi eneo la Iyumbu Dodoma, tangu Agosti 2020

Awali nilikuwa naishi Uwanja wa Ndege Ukonga Dar es Salaam nikiwa makao makuu Polisi.

Niliajiriwa tarehe 2, 10, 1999

Katika Jeshi la Polisi niko Kamisheni ya Upelelezi Makos ya Jiani, kitengo cha udhibiti na usajili silaha za kiraia. Kinahuska na masuala ya utoaji leseni, vibali vya usafirisjaji silaha na risasi na vya upitisjaji silaha na risasi kwenda nchi jirani, vibaki vya uuzaji silaha.

Pia tunashirikiana na nchi mbalimbali udhibiti uzagaaji wa silaha nyepesi, kikanda na Kimataifa.

Usajili silaha za kiraia ni silaha zilizoruhusiwa kwa Sheri ya Silaha kama vile pistol, riffles, shotgun, gobole na silaha yoyote ambayo Bodi ya Ushauri na Udhibiti wa Silaha itapendekeza iingizwe silaha za kiraia

Udhibiti uzagaazi silaha ni zaidi ya hizi tunazozisajili, unahusisha za kivita.

Silaha ndogo hutumiwa na mtu mmoja, Silaha nyepesi inahitaji watu wawilI kuiendesha ili ilete matokeo.

Wadhifa wangu ni mrajisi wa leseni za bunduki (CO Armed Registrar)

Majukumu yangu ni kuhakikisha napokea maombi ya umiliki silaha yaliyopitishwa na Kamati za Ulinzi na Usalama kuanzia ngazi ya mtaa anakoishi mwombaji, kata, wilaya na mkoa.

Pili, kuyakagua maombi hayo, ili kuona kama yana vigezo kisheria, kuona ya kwamba yatakuwa yamepitishwa katika kamati nilizozitaja na yanayaokidhi vigezo huendele kuyashughulikia na yasiyo na vigezo hurudishwa yalikotoka yarekwbishwe

Utoaji vibali vya uingizaji silaha nchini, usafirishaji silaha nje, vibali vya upitishaji silaha kwa nchi zisizo na bandari

Vibali vya biashara ya silaha na risasi, utunzaji wa silaha, kibali cha kufanyia matengenezo silaha za kiraia zikiwa na matatizo. Kuto leseni kwa waliokidhi vigezo vya kumiliki silaha.

Pia kutunza kumbukumbu za silaha na wamiliki waliosajiliwa

Mwisho ni kupokea maombi ya kiuchunguzi pale silaha inapookotwa ili kuona kama imesajiliwa au la.

Maombi mengine ya uchunguzi wa silaha ni silaha yoyote ambayo tayaari zinaweza kuhitajika kwa upelelezi, hivyo ni kitengo kinachosaidia uchunguzi masuala ya silaha.

Mchakato wa vibali vya umiliki silaha ni kununua silaha toka duka lililopewa kibali cha biashara ya silaha na risasi, au kununua silaha kutoka kwa mmiliki aliyekuwa anaimiliki kihalali kwa kuandikiana mkataba wa kisheria

Kama silaha ni ya mirathi kikao cha ndugu kitakaa chini ya mwenyekiti na watakubaliana kwamba nani airithi silaha hiyo na wakimteua mrithi kwa makubaliano anaweza kuomba kuimiliki mwenyewe au kuiuza lakini atahakiikisha mteja anayemuuzia anamkabidhi nyaraka zote za mirathi na ule mkataba walioandikishiana kisheria.

Pia mwombaji anaweza kununua silaha nje ya nchi kwa kuomba kibali cha kuingiza silaha nchini, kisha clearing agent ataipeleka kwenye ghala kuilhifadhi wakati mwombaji akiendele na taratibu za umiliki.

Katika vyanzo hivyo vyote silaha inatakiwa kuwa imehifadhiwa ghalani na mnunuzi atapewa tu nyaraka zimsaidie katika maombi hayo

Kuna fomu za maombi ya kumiliki silaha ambazo mwombaji hupaswa kuzijaza na kuambatanisha nyaraka zote zinazoonyesha chanzo cha silaha hiyo pamoja na nyaraka zinamwelezea mwenyewe kazi anazozifanya na nyaraka zinazomthibitishia ulazima kumiliki silaha au matishio.

Maombi huambatanishwa na muhtasari kiIa ngazi ya Mtaa, kata, Wilaya na mkoa. Pia hati ya tabia njema inayotolewa na Polisi Kitengo cha uchunguzi wa Kisayansi.

Wakili Kibatala anamtambulisha wakili Mtobesya kisha anaomba Wakili Mtobesya atoe hoja ya kisheria kwa ushahidi uliotolewa

Jaji anarekodi kisha Wakili Mtobesya anasimama na anaeleza kuwa maelezo ya shahidi hayako kwenye mwenendo wa maelezo ya mashahidi yaliyotolewa Mahakama ya Kisutu na kwamba ni kinyume cha sheria na hivyo ushahidi wa shahidi huyo utakuwa haujaingia vizuri kwenye mwenendo na anaomba mahakama itoe mwongozo

Kwa kuwa upande wa mashtaka kama wakitaka kumtumia katika mazingira hayo walipaswa wawasilishe maombi rasmi lakini hawajafanya hivyo.

Pia tutaomba maelekezo kuhusu ushahidi wake ambao umeshaingia iwapo upande wa mashtaka waliwasilisha maombi hayo na Mahakama ikaridhia.

 Anahoji iwapo itakuwa ni sahihi kuwasilisha maombi hayo kwa kuwa tayari shahidi ameshaanza kutoa ushahidi kabla ya maombi kuwasilisha kwa mujibu wa Sheria.

Jaji anarekodi hoja za wakili Myobesya

Wakili Kidando anajibu hoja

Mheshimiwa Jaji pingamizi hilo halina mashiko yoyote kisheria.

Kwanza limeletwa katikati ya ushahidi ni kinyume cha utaratibu kabisa. Kama wangekuwa na hoja hiyo walitakiwa kuitoa mapema. Pengine ni matokeo ya kutokufuatilia mwenendo kwa umakini.

Hoja yetu ya pili, Mheshimiwa Jaji ni kwamba shahidi huyu aliorozeshwa tangu kipindi cha committal proceeding katika rekodi za Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ukurasa 32 na jina lake ni namba 23.

Substance ya ushahidi huo ilisomwa katika mwenendo wa shauri hilo katika mwenendo wa Agosti 23, 2020.

Lakini pia katiba ile orodha ya vielelezo nyaraka anayokuja kuizungumIa imeorodheshwa namba 18 na imesainiwa naye shahidi, Sebastian Madembwe SSP.

Kwa hiyo katika haki yoyote ile hatukutakiwa kuleta maombi chini ya kifungu cha 289 CPA ili shahidi huyu aweze kutoa ushahidi wake

Pia Kanuni 8(2) ya Mahakama hii za mwaka 2016 takwa hilo la kisheria lilitekelezwa

Kwa jina linaloonekana kwenye committal proceeding hakuna kitu kipya ambacho wakili amekionyesha na hivyo hakuna haja ya kuhoji uhalali wa usahidi wake maana yuko hapa kihalali na tunaomba pingamizi litupiliwe mbali na shahidi wetu aweze kuendelea.

Mtobesya: Wenzangu naona wameni attack personal kuwa sikuwepo tangu mwanzo. Tunachofanya ni kusaidia mahakama.

Kwenye committal proceedings hakuna substance ya ushahidi wake. Substance kuna vitu vitatu. Kwanza jina lake, hatukatai lipo lakini statement yake haipo kuwa anakuja kusema nini. Statement hiyo ni ya muhimu sana.

Wakili wa Serikali Hilla: Naona wakili anaanza kujielekeza kwenye maelezo yenyewe.

Wakati Mtobesya anaendelea simu ya msikilizaji inaita na kusimamisha mwenendo.

Jaji: Tukubaliane maana sisi ndio watumiaji wa hiki chumba kaama mtu simu yake ikiongea hivyo na kusimamisha mwenndo tumfanyeje?

Baadhi ya wasikilizaji: Atokeww nje.

Jaji atolewe halafu baaaye tumuingize tena?

Wasikilizaji: Asirudi

Jaji: Kwa hiyo tum-ban kabisa?

Wasikilizaji: Ndio

Jaji: Sawa sasa ikitokea mtu huyo tunamtoa nje na si kwa siku hiyo tu bali awe marked asirudi tena siku yoyote:

Wasikilizaji: Sawa.

Kesi inaendelea na baada ya msikilizaji huyo ambaye simu yake imeita kutolewa nje na maaskari Magereza.

Wakili Mtobesya anasisitiza hoja yake kuwa maelezo ya shahidi hayako katika kablasha la vielelezo na hivyo hayakusomwa. anaomba mahakama itoe mwongozo kuhusu hilo.

Jaji: Mmezisikia hoja wote si ndo? Naomba nipate muda na mimi wa kuzipitia na sheria zinazohusika ili niweze kutoa uamuzi. Naomba turudi hapa saa 5:15 kwa ajili ya uamuzi.

Kesi inaahirishwa kwa muda.

Baada ya kesi kuahirisha kwa muda sasa kesi ineendelea

Jaji anarejea kutoa uamuzi

Jaji Tiganga anaanza kusoma uamuzi wake kwa kurejea hoja za pingamizi la utetezi na majibu ya Serikali, kisha anafanya uchambuz iwake kabla kutoa uamuzi

Jaji: Pande zote mbili hukubaliana malengo ya sheria ni kuhakikisha ushahidi unafahamika kwa washtakiwa, kwa kusomwa Mahakamani na kwa nyaraka kuandakiaa na kukabidhiwa upande wa Utetezi.

Usomaji maelezo hufanywa na upande wa mashtaka na nyaraka huandaliwa na mahakama

Sheria inamruhusu Mtobesya kuleta pingamizi wakati wowote.

Na ushahidi unapokuwa haujasomwa mahakama ya chini hauwezi kutolewa isipokuwa kwa maombi ya upande wa mashtaka.

Mahakama inapaswa kurejea katika kumbukumbu ili kupata majibu. Mahakama imeona mwenendo wa Agosti 23, 2021 imebaini kuwa maelezo yanayoeleza kuwa maelezo hayo yamesomwa na yakaorodhesha majina ya mashadi 24 akiwemo shahidi huyu ambaye pia amesaini. Huo ndio msimamo wa kumbukumbu zilizoko Mahakamani na hiyo kumbe maelezo ya mashahidi wote yamesomwa.

Pia mahakama imeona kwenye kumbukumbu kuna nakala ya maelezo ya shahidi huyo kwa hiyo tuna ushahidi kuwa maelezo ya shahidi yamesomwa na hivyo pingamizi lililoletwa halina mashiko.

Hivyo mahakama inaelekeza shahidi huyu aendelee kutoa ushahidi

Pingamizi la utetezi limetupiliwa mbali na sasa shahidi anaendelea kuelezea taratibu za umiliki wa silaha.

Shahidi: Nyaraka nyingine zimazoambatanishwa kwenye maombi ni zile zinazomtambulisha kama vile kazi anayoifanya.

Maombi yakishawasilishwa kwangu nayakagua ili kujiridhisha kama yanakidhi vigezo vilivyowekwa kwa mukibu wa sheria. Kama hayajakidhi vigezo yanaweza kurudishwa kwenye mkoa husika kukamilisha vigezo vinanyokosekana.

Endapo itaonekana mwombaji hana sira za kisheria hata akirekebisha vigezo maombi hayo hubako makao makuu na mkoa husika hujulishwa.

Baada ya kubaini kuwa maombi yamekidhi vigezo ni kumjulisha mwombaji kwamba amekubaliwa kwa barua na huambatanishwa hivyo anatakiwa kwenda kwa mkuu wa Polis Wilaya kulipia malipo ya leseni kisha arudi ofisi ya mrajisi akiwa na barua ya kumjulisha kukubaliwa kumiliki silaha ikiambatanishwa na risti za malipo ya leseni, malipo ambayo hufanyika kwa OCD

Baada ya kuwasilisha nyaraka kuthibitisha amekamilisha malipo kinachofuata ni kukamilisha usajili kwanza kwa kuipa silaha husika namba ya usajili (Central Arms Registry Numbe - CAR) ambayo inakuwa juu ya kutabu cha kumiliki silaha.

 Kitabu hicho kitaandikwa maelezo ya silaha husika, yanayotokana na nyaraka mwombaji alizopewa ambayo inakuwa na maelezo yote ya silaha na anuani ya mwombaji.

Kisha picha hubandikwa kwenye kitabu hicho, kisha nitafungua file juu nitaandika ile registration number yaani CAR numbe kwa ajili ya kumbukumbu.

Nikimaliza kumsajili mfumo wa makaratasi namuingiza kwenye mfumo wa kielektroniki.

Kwenye mfumo utanitaka nianze kuingiza CAR number.  Baadaya haoo utanitaka niingize aina ya silaha, mtengenezaji yaani kampuni iliyoitengeneza na serial number, namba ya silaha ambayo mtengenezaji ameigonga kwenye silaha husika.

Taarifa za nyongeza ni nchi ilikotengenezwa silaha hiyo model number na caliber size. Hizi si za muhimu sana ila ni za nyongeza katika kutusaidia utambuzi

Pia tunaingiza idadi ya risasi ambazo mmiliki anatruhusiwa kuzimiliki kwa wakati mmoja, idadi ya risasi zinazoruhusiwa na mmiliki katika kipindi cha uhai wa leseni.

Baada ya particulars za silaha sasa tunajaza particular za mmiliki, majina yake matatu kama fomu alivyoijaza na kama yanavyoonekana kwenye kitambulisho cha Taifa kama anacho au kingine chochote.

 Kisha tunaingiza uraia jinsia kazi yake namba ya kitambulisho cha uraia au mpiga kura, makazi yake kuanzia mtaa, kata, tarafa, wilaya na mkoa.

Taarifa nyingine tunazoingiza kwenye mfumo ni mawasiliano yake, namba za simu, baruapepe, chanzo cha silaha kwamba alinunua dukani, ali-import au imehamishwa tu umiliki.

Baada ya hapo kinachofuata ni ku-save na hakutakuwa na ruhusa ya kuwa amended mpaka kwa ruhusa ya administrator wa mfumo.

Tuna-save ili kuweza kurejea taarifa zake zinapohitajika mfano kunapotokea uhakifu kama ni miongoni mwa silaha zilizosajiliwa.

Kwa Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Silaha na Risasi na Kanuni zake anachopewa mmiliki ni kile kitabu cha umiliki.

Kunapokuwa na maombi ya uchunguzi sisi hupokea maombi kutoa ofisi inayohusika na upepelezi na kutoka taasisi ambazo husimamia utekelezaji wa sheria kama Takukuru na Taasisi ya Kuzuia Madawa ya Kulevya

Maombi uchunguzi silaha lazima yawe na taarifa tatu za lazima.

Kwanza ni aina ya silaha kama pisto, Riffle nk., jina la mtengenezaji na namba za silaha (serial number ya silaha)

Hizo ndizo zitatuwezesha kujua imesajiliwa au haijasajiliwa hata kama taarifa hizo nyingine hazipo

Tunapopokea maombi tunagonga mhuri na tunaanza kuifanyia kazi kwa kuingiza hizo taarifa kwenye mfumo maana hizo number ni unique. Watengenezaji huwa wanawasiliana kuhakikisha serial number haziingiliani.

Tukishaingiza hizo taatifa kwenye mfumo nabonye alama Ok kama hiyo silaha imesajiliwa inaleta matokeo chanya. Nakwenda kujiridhisha kwenye jalada, kisha nina-printi

Matokeo yakiwa hasi maana yake baada ya kuingiza particulars za silaha mfumo unatafuta na kubaini hakuna kumbukumbu yoyote ya silaha.

Kama matokeo ni chanya nafanya mambo mawili. Kwanza naandika barua kwa aliyeomba uchunguzi kumjulisha matokeo na nitatoa printout na kuambatanisha na barua

Matokeo yakiwa hasi nitaandika barua tu kuwajulisha

Novemba 25, 2020 nikiwa ofisini kwangu Makao Makuu Dodoma niliipokea barua ya maombi ya uchunguzi wa silaha bastola toka Ofisi ya makao makuu ndogo idara ya upelelezi Dar.

Ilinitaka nifanye uchunguzi wa silaha aina ya bastola, mtengenezaji Luger Serial number A5340

Niliyafanyia kazi kwanza kwa kujiridhisha kama maelezo ya silaha yanajitosheleza mimi kufanya uchunguzi? Nikiona jina la silaha, mtengenezaji na serial number nikaingiza kwenye mfumo. Mfumo ulinipa matokeo hasi kwamba silaha hiyo haijawahi kusajiliwa.

Niliandika barua ya taarifa ya uchunguzi kwenda kwa mwombaji wa uchunguzi

Nilieleza kwamba kufuatia uchunguzi uliofanyika matokeo ni kwamba silaha hiyo haijawahi kusajiliwa.

Shahidi anapewa nakala ya nyaraka aiangalie kama anaweza kuitambua kuwa ni ile aliyoiandika yeye.

Baada ya kuiangalia anasema ni barua inayoonesha taarifa ya umiliki wa silaha.

Hii nyaraka nina uhusiano nayo kwanza nimeisaini mwenyewe, ina majina yangu na wadhifa nilionao.

Ninaiomba mahakama barua hii inayoonesha taarifa za uchunguzi, ipokewe kama ushahidi

Mawakili wa utetezi baada ya kuikagua mmoja baada ya mwingine wanasema kuwa hawana pingamizi barua hiyo kupokelewa

Jaji Tiganga: Tunaipokea barua hii ambayo inaelekezwa kwa ACP H. Msangi, makao makuu ndogo Polisi Dar es Salaam kuhusu uchunguzi wa silaha kuwa kielelezo namba 10 cha upande wa mashtaka.

Baada ya mahakama kuipokea Jaji anamtaka shahidi aisome kwa sauti na shahidi anaisoma sasa

Katika maelezo ya barua hiyo anaeleza kuwa uchunguzi wa Silaha hiyo bastola aina ya Luger umebaini kuwa haijasajiliwa na ofisi hiyo.

Akiongozwa na Wakili Hilla shahidi anafafanua kuwa uchunguzi ulitaka kubaini kana silaha hiyo inamilikiwa na nani.

Kumbukumbu za Bastola aina ya Luger namba A5340 haijawahi kusajiliwa.

Shahidi anadai kuna makosa ya kiuandishi kuhusu mwaka kati ya jalada la uchunguzi linaonyesha kwaka 2021 lakini barua ya maombi ya uchunguzi ni ya mwaka 2020. Shahidi anaomba msamaha kwa Jaji kwa makosa hayo na kwamba mwaka kwenye jalada nao usomeke 2020 badala ya 2021

Wakili Myobesya anasimama na kupinga kuwa anachokifanya shahidi si sahihi kufanya marekebisho ya nyaraka kizimbani na kwamba nyaraka inapaswa ijieleze yenyewe

Wakiii Myobesya anaungwa mkono na wakili Kibatala

Wakili wa Serikali Kidando anajibu kuwa hakuna mahali ambapo sheria inamzuia shahidi aliyeko kizimbani kutoa maelezo ya ushahidi.

Mtobesya anasisitiza kuwa hiyo ni Kanuni ya siku nyingi na hakuna haja ya kuwa wanasimama kila mara na kuichosha mahakama kwa mambo ambayo yako wazi.

Jaji: Sheria kama ilivyo inataka nyaraka ijieleze yenyewe. Hapo shahidi hafanyi marekebisho bali anatoa ufafanuzi kuwa Kuna makosa na kwamba kuna ilipaswa isomeke hivi.

Jaji: Kwa hiyo mahakama ita- consider wakati inatolea maamuzi kuona kana kilichofanywa kinaathiri vifungu vya sheria husika au la.

Kibatala anaeleza kuwa upande wa utetezi wote hawana maelezo ya shahidi huyo hivyo anaomba kwa kuzingatia uamuzi wa mahakama katika pingamizi hilo ielekeze wapewe maelezo hayo ili yaweze kuwasadia kumhoji shahidi.

Ombi linakubaliwa na Jaji Tiganga anatoa maelekezo kwa msaidizi wake ili  mawakili wa utetezi wapewe maelezo hayo baada ya upande wa mashtaka kueleza kuwa hauna,

Ombi linakubaliwa na Jaji Tiganga anatoa maelekezo kwa Msaidizi wake ili  mawakili wa utetezi wapewe maelezo hayo baada ya upande wa mashtaka kueleza kuwa hauna pingamizi dhidi ya maombi  hayo ya Kibatala.

Kesi inaahirishwa hadi saa 8:15 itakapoendelea tena ambapo mawakili wa utetezi wataanza kumhoji shahidi kuhusiana na ushahidi wake huo.