Kinachowakimbiza wanaume mwanzoni mwa uhusiano-2

Katika makala yaliyopita nilieleza kuwa, mwanamume anapogundua mazingira aliyopo katika uhusiano hatayaweza, huanza kufungasha virago vyake kimya kimya.

Na akishafanya uamuzi wa kukukimbia basi utaona visingizo na sababu tele zisizo na mashiko zikimiminika. Sasa endelea
 

Wanaume wanapogundua kutawaliwa

Kwa kawaida wanaume wanafuata mapokeo ya asili kwamba, wao ni viongozi na watawala wa familia.

Hutaka kuliona hili hata kabla hamjaingia kwenye ndoa. Kwa bahati mbaya wako wanawake kwa sababu za kiasili au malezi na makuzi wamekuwa ni wenye kutaka kupewa nafasi.

Hutaka kuamrisha, kuongoza au kufanya uamuzi kwa wengine na wasio rahisi kuongozwa. Wanawake wa jinsi hii ni rahisi sana kukimbiwa na kila mwanamume anayetaka kuwanao kwenye uhusiano, au hata kama wameishia kuoana basi hukutana na mashindano au misuguano mikali kwa sababu mwanamume huona ni bora ndoa ife kuliko kuipoteza nafasi yake ya uongozi au ukuu wa familia, hususan katika nguvu ya kufanya uamuzi.

Katika kujitutumua huku mwanamume anaweza kuonyesha tabia zenye kumuumiza mwanamke, kama vile hasira za mara kwa mara, fujo, matusi na visasi.
 

Utegemezi mkubwa wa wazazi au ndugu zako

Ndoa imetengenezwa katika hali ya kwamba wanandoa wote wanatakiwa kuwaacha wazazi au ndugu zao na kushikamana na wenza wao katika mambo yote, ikiwamo uamuzi wao. Wanaume wengi huwa makini sana, tena kimya kimya kuangalia jinsi wapenzi wao wa kike wanavyohusiana na wazazi wao na ndugu zao wengine.

Iwapo watagundua umemezwa, umekamatwa na kushikwa jumla na ndugu zako na huwezi kufanya uamuzi bila wao kuuridhia, hata yale yanayomhusu mume wako basi wao huhamaki na kuwa na hofu kubwa, huku mioyo yao ikiona kama wao ndio wameolewa badala ya kuoa. Hisia hizi ni mbaya sana kwa mwanamume, hivyo kuweza kujihami kwa kurusha mishale ya maneno na kuamsha misuguano mingine, sawa sawa na ile niliyoisema kwenye sababu ya nne. Kushirikiana na ndugu zetu sio kitu kibaya ili mradi nafasi ya mume ibaki pale pale na kuheshimiwa hata kama mchango wake kiuchumi hauonekani kuwa na mashiko.

Kwa upande mwingine katika hili, inaweza kumuwia ngumu kuolewa binti anayetegemewa kwa asilimia 100 na ndugu au wazazi wake, kwa maana kila kijana anayejileta kwake hata kama binti ni mzuri, bado kijana anaona mzigo mkubwa mbeleni na kuamua kumkwepa au kumkimbia.
 

Matatizo fulani kwenye tendo la ndoa

Ni ukweli usiopingika kwamba wanaume wameumbwa kupenda na kutamani kufanya tendo la ndoa mara kwa mara, wao ni rahisi sana kukimbizwa katika uhusiano na mwanamke pale wanapogundua au kukutana na ugumu wowote kwenye suala zima la ufanyaji wa tendo la ndoa, ingawa ni mara chache sana wanaweza kuwa wazi wakwambie nini kinacho wasumbua au wasichokipenda, labda muwe na kiwango cha juu sana cha mawasiliano.

Baadhi ya vitu vinavyoweza kuleta ugumu au changamoto kwenye tendo la ndoa na kumfanya mwanamume akimbie ni kama vile, umbo kubwa au uzito wa mpenzi wake wa kike, harufu mbaya ya sehemu za siri au maeneo mengine ya mwili kama vile chini ya matiti, mdomoni au puani, changamoto nyingine ni kama vile ukavu uliopitiliza, au uchafu mwingine wa mwili usiovumilika.

Akigundua una mtoto, kutoa mimba

Wanaume wengi huwa na kiu ya kuja kuanza familia zao wao wenyewe na sio kukuta mtoto wa mwingine.

Ni rahisi sana mwanamke akamkuta mtoto wa mumewe na akaendelea kuishi naye kuliko mwanamume kumkuta mtoto wa mke wake na kuishi naye bila matatizo.
Hii ndio maana kinadada wengi wakisha pata ujauzito kabla ya kuolewa wanahisi au wanakumbana na changamoto kubwa sana katika kuchumbiwa na wanaume wengine kwa sababu tu mtoto anakuwa kikwazo.

Vilevile mwanamume anapogundua kama mpenzi wake amewahi kutoa mimba huwa anakuwa na hofu ya kuendelea na uhusiano, maana anakuwa kwenye njiapanda ya uhakika wa kupata mtoto au la.