Michepuko inavyovuruga mipango ya familia

Jana jioni nimepata bahati kupata chai na injinia. Nisingependa kutaja jina lake kwa minajili ya kutunza faragha yake, lakini ni mtu mwenye mafanikio makubwa katika maisha yake na biashara. Tunapata kikombe cha chai baada ya kufanya kazi pamoja mjini Dodoma.

Najua mafanikio yana siri nyingi na wakati mwingine watu huogopa kumwaga mchele hadharani. Hali ni tofauti kidogo kwa injinia. Ninapomchokoza anisimulie safari yake ya mafanikio uso wake unakunjuka.

Haraka haraka anazima simu zake mbili na kuziweka mezani. Tangu tuanze mazungumzo amekuwa akipokea simu za dharura na kutoa maelekezo ya hapa na pale. Naona hapa anaamua kunipa uzingativu wake wote. Ninamkazia macho yangu kumsubiri aseme.

Injinia anaanza kwa kunieleza makosa kadhaa aliyowahi kuyafanya katika safari yake ya biashara. “Ningekuwa kijana kama wewe ningeanza kujenga uhusiano mzuri na benki mapema. Huwezi kufanikiwa kwa fedha zako mwenyewe.”
Hoja ya namna bora ya kukopa na kufanyia kazi mkopo wa benki inachukua muda mrefu lakini hatimaye tunahamia kwenye hoja ya pili.

Dakika 30 zimepita na hakuna simu imeingilia mazungumzo yetu. Simu zimezimwa kabisa. Ishara ya umakini katika mazungumzo yetu. Injinia anakaa vizuri kwenye kiti chake, anasita kidogo, anauzungusha mkono wake wa kulia kifuani kisha analipua bomu,

“Christian ninachokwambia utakishangaa lakini nivumilie. Nimefanya utafiti usio rasmi muda mrefu na nimethibitisha,” ananipa uhakika wa kile anachokisema. Ninamwitikia. “Unajua kuna upuuzi mwingi sana wanaume tunaambukizana vijiweni na tunaangamiza maisha yetu bila kujua. Wengi wetu tunakuja kugundua kwa kuchelewa sana.” Ninashtuka kidogo.

“Mfano tunadanganyana sana ili mambo yaende lazima umtenge mke kwenye mipango yako. Tunaaminishana mke sio wa kuambiwa mambo ya maana. Tunawaona wake zetu kama akina Delila wanaoweza kutuuza kwa maadui kwa bei ya punguzo.

“Sasa nikwambie usifanye makosa kwenye kuoa. Kukurupuka kuingia kwenye ndoa ndio sababu hasa ya huu upuuzi tunaoambiana vijiweni. Huwezi kuwa mtu asiye sahihi na unataka upate mtu sahihi. Mafanikio yanaanza kuonekana mapema unapochagua mwanamke wa kuoa.”

Injinia anapiga msumari wa moto. Kabla sijaonana na injinia nilitoka kunyoa. Ninasikia kuwashwa kipara. Ninajikuna kidogo. Injinia anachukulia kama ishara ya dawa kuniingia. Sasa anatumia mikono kueleza. “Usioe mwanamke kwa sababu za kijinga jinga. Mwanamume mwenye akili ya mafanikio huwa haoi kizembe zembe. Tulia unapotafuta mke wa kuoa. Hao jamaa wanaosema mwanamke sio mtu wa kumwamini ni watu waliokurupuka kuoa.

“Ukishakurupuka kuoa, lazima utalazimika kuishi kama digidigi. Huna uhakika na mambo yako. Utawachukulia wanawake kama maadui wa siri ambazo hata wewe mwenyewe unaziogopa. Najua unaweza kunishangaa lakini nikwambie Christian, huwezi kufanikiwa ukimuweka mkeo mbali na wewe. Nilichojifunza katika miaka michache ya kupambana na maisha, Christian, mafanikio ya mwanamume hubebwa na mke wake.” Injinia ni kama alihisi ninahitaji mifano halisi. “Mimi mke wangu anajua biashara zangu zote. Mke wangu anajua akiba zangu zina nini. Nikisafiri vitabu vya cheque (hawala ya fedha) anabaki navyo. Simfichi chochote.

“Mipango yangu yote anaijua. Ninamshirikisha kila ninachofanya. Ninafahamu ukweli ambao sio wanaume wengi huwa wanaufikiria vizuri. Siku nikiondoka hapa duniani, mke wangu ndiye atabaki na wanangu. Hakuna mjomba, wala baba mdogo, wala shangazi atakuja kuniokolea watoto wangu. Mke wangu ndiye anayejua uchungu wa mwana na namna tulivyotafuta maisha. Nitakuwa mjinga nikificha mambo yangu ya maana kwake wakati nalala naye usiku.” Hapo tayari ilikuwa ni saa tatu za usiku. Hata sikutamani aondoke.

Injinia anaomba kutoka akateme mate kidogo. Namruhusu. Ninatafakari mambo aliyokwisha kuniambia mpaka sasa. Usimfiche jambo mkeo. Mke ndiye atabaki na wanao siku wewe haupo. Maneno mazito ambayo ukiyasema kwa wanaume wengi unaonekana hujitambui. Ishini na wake zenu kwa akili. “Hii ina maana gani?” Ninatafuta uzani wa kuyatathmini maneno ya Injinia. Dakika zipatazo tano huyo injinia akarudi. Darasa linaendelea.

“Wanaume wengi hawafanikiwi kwa sababu wanaelekeza nguvu na muda mwingi kufanya vitu visivyochangia mafanikio yao. Tusiende mbali. Nguvu za wanaume wengi zinaishia kwenye uzinzi. Uzinzi ni gharama. Uzinzi ni umaskini.” Ninacheka kwa aibu. Injinia anacheka kwa kejeli na kupigilia msumari, “wewe muda wote unawaza wanawake wa kuhonga mipango ya maana unapanga saa ngapi?”

“Unajua hii michepuko inayosumbua wanaume wengi ukiangalia vizuri ni biashara ya utafutaji tu na ombaomba wanaotumia wanaume wajinga kuendesha maisha yao. Mwanamume ukikosa akili utajikuta unatumia fedha nyingi kumtunza mwanamke asiye na akili kama wewe. Hana akili kwa sababu anafanya kitu ambacho yeye mwenyewe asingependa kufanyiwa.”

Hoja nzito hii. Namwona injinia anagida kinywaji chake kidogo na kunitazama kwa kujiiba kidogo kama mtu anayepima namna ninavyopokea busara zake. Ninatingisha kichwa kuashiria kukubaliana naye. Ninagida na mimi.