Kiongozi wa mila acharuka jina la Kimasai kutumika vibaya

Mwenyekiti wa taasisi ya FTL Maasai Tanzania, Joseph Laizer akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa kikao kilichofanyika Orkolili Wilayani Siha Mkoani Kilimanjaro. Picha na Fina Lyimo.
Muktasari:
- Migogoro mingi inayotokea nchini siku hizi inachangiwa na baadhi ya makundi ya watu wanaotumia vibaya jina la jamii hiyo kwa kufanya mambo yaliyo kinyume na mila, desturi na maadili.
Siha. Viongozi wa Kimila wa Jamii ya wafugaji wa Kimasai kupitia taasisi yao ya Umoja wa Viongozi wa Jamii hiyo nchini, FTL-Maasai wamemwomba Rais Samia Suluhu Hassan kuingilia kati baadhi ya makundi ya watu wanaotumia jamii ya Wamasai kwa maslahi yao binafsi ambayo yanachochea chuki, mifarakano na migogoro isiyokuwa ya lazima katika maeneo mbalimbali nchini.
Akizungumza leo Jumatatu Septemba 11, 2023 katika eneo maalumu la kufanyia mila zao za Kimasai lililopo katika Kata ya Orkolili wilayani Siha mkoani Kilimanjaro juzi, Mwenyekiti wa Taasisi ya Foundation for Traditional Leaders for Maasai nchini (FTL-Maasai Tanzania), Joseph Laizer amesema kuwa jamii ya Wamasai kutoka maeneo mbalimbamli nchini wamekutana katika eneo hilo maalumu la mila ili kujadili pamoja na mambo mengine masuala ya kulinda maadili ya kimila ya jamii hiyo.
Laizer amesema kuwa, migogoro mingi inayotokea nchini siku hizi inachangiwa na baadhi ya makundi ya watu wanaotumia vibaya jina la jamii hiyo kwa kufanya mambo yaliyo kinyume na mila, desturi na maadili ya jamii hiyo kwa maslahi yao binafsi na kusababisha chuki, mafarakano na migogoro isiyokuwa ya lazima.
“Leo tumekutana hapa wake kwa waume, wazee na vijana kukumbushana mila na desturi zetu nzuri zenye lengo la kusimamia maadili hasa kwa vijana wetu kwa maslahi makubwa ya taifa kwani tumegundua kuwa kuna watu ambao hawatoki jamii ya wafugaji ya Maasai ambao wamekuwa wakipotosha umma kwa kutumia jina la Maasai kwa maslahi yao binafsi, sisi viongozi wa mila wa jamii ya Wamasai tunakemea tabia hiyo kwani inaleta chuki, mifarakano na migogoro isiyo ya lazima kama inayotokea kule Ngorongoro,” amesema Laizer.
Mwenyekiti huyo amesema, mila na desturi zao zimeingiliwa na baadhi ya makundi wasiyoitakia mema nchi yetu na kusababisha migogoro isiyokuwa ya lazima na kumwomba Rais Samia Suluhu Hassan kuingilia kati jambo hilo ili kuendelea kudumisha upendo na amani nchini.
“Kuna baadhi ya ndugu zetu wanavaa mavazi yanayofanana na mavazi yetu ya asili ya kimila tunayovaa na kufanya mambo ambayo ni kinyume kabisa na maadili yetu sisi wamasai, hivi juzi pia kuna kikundi cha watu walifanya Kongamano Arusha na kutangaza kuwa ni la jamii yetu ya Maasai kwa maslahi yao binafsi, sisi viongozi wa jamii Kimasai kupitia taasisi yetu ya FTL-Maasai Tanzania hatulitambui hilo kongamano,” amesema.
Laizer amesema kuwa, wanatamani kukutana ana kwa ana na Rais Samia ili wazungumze naye masuala mbalimbali yenye lengo la kudumisha amani na upendo nchini na wanatarajia kuandaa Kongamano maalumu la kuhamasisha kuzingatia maadili ili kuondokana na migogoro isiyokuwa ya lazima.
Mmoja ya ajumbe kutoka Baraza la Wazee wa Mila wa Kimasai (Legwanani) kutoka wilayani Monduli mkoani Arusha Anna Mollel amesema kuwa wamefika eneo hilo maalumu la kufanyia mila za Kimasai kujadili mambo mbalimbali ya kudumisha mila na desturi za jamii hiyo pamoja na masuala ya kuporomoka kwa maadili nchini.
“Pia leo tumejadili Kongamano ambalo limefanyika Arusha hivi karibuni ni batili maana halikupitia kwenye vikao halali vya Baraza la Ma-Legwanani, pia taasisi ya Viongozi wa jamii yetu, kwani hata mambo mengi yaliyofanyika pale hayakuzingatia maadili yetu,” amesema Mollel.
Aliendelea kufafanua kuwa, jamii ya kimasai inao viongozi wake hivyo siyo vizuri vikundi vya watu kufanya mambo yaliyo kinyume na maadili ya Kimasai kwa kutumia jina la Wamasai ni kosa kubwa.