Prime
Kipindi cha kufunga mkanda kwa wakazi Kigamboni
Dar es Salaam. Ni kipindi cha wakazi wa Kigamboni jijini Dar es Salaam kufunga mkanda.
Kauli hiyo inaakisi uhalisia wa uvumilivu wa zaidi ya mwaka wanaopaswa kuwa nao watumiaji wa vivuko katika eneo la Kigamboni-Magogoni.
Wanachopaswa kuvumilia hasa ni huduma hafifu katika eneo hilo kwa kipindi cha karibu mwaka, zitakazosababishwa na uchache wa vivuko, baada ya vikubwa vilivyokuwepo kupelekwa kwenye matengenezo makubwa.
Matarajio ya hali ngumu ya huduma katika eneo hilo, yanatokana na vivuko vya MV Magogoni na MV Kigamboni kuwa nje ya huduma kutokana na matengenezo makubwa.
Juni 6, mwaka huu Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (Temesa), ulitangaza kusimamisha huduma za kivuko cha MV Kigamboni, kutokana na kwenda kufanyiwa matengenezo makubwa.
Kabla ya kivuko hicho, kivuko cha MV Magogoni nacho hakikuwa katika huduma tangu Februari mwaka 2023, kilipopelekwa Mombasa nchini Kenya, kwa ajili ya matengenezo makubwa.
Kipindi cha kufunga mkanda
Kutokana na matengenezo ya kivuko cha MV Kigamboni, wananchi wanaotumia huduma ya kivuko hicho, watalazimika kufunga mkanda kwa takribani mwaka.
Makadirio ya muda huo, yanatokana na kile kilichoelezwa na Meneja wa Vivuko Temesa Kanda ya Mashariki, Abdulrahman Ameir, kuwa bado zabuni haijatangazwa.
Kinachofanyika sasa, alieleza ni hatua za ununuzi zinazohusisha tathmini ya kujua kitu gani cha kubadilishwa na kitagharimu kiasi gani cha fedha kwenye kivuko hicho.
“Mchakato wa ununuzi utafanyika kwa wiki mbili na ukimalizika ndipo tutakapojua kitu gani kinahitajika na zabuni itatangazwa ili kumpata mzabuni atakayekuwa na uwezo wa kufanya matengenezo yatakayobainika,” ameeleza.
Baada ya mchakato wa ununuzi kwa mujibu wa Ameir, zabuni itatangazwa kimataifa ambayo kisheria itakuwa kwa siku zisizozidi 21 hadi atakapopatikana mkandarasi.
Meneja huyo amefafanua mchakato huo utafanikisha kupatikana mkandarasi na kuanzia hapo ndipo kazi ya matengenezo itakapoanza, ikihusisha kubadilisha injini zote nne, gia boksi, mifumo ya uendeshaji na mabati.
Kwa uzoefu wa Ameir, amesema kazi hiyo itachukua si chini ya miezi minane, kwa kuwa ndani yake kuna mchakato wa mkandarasi kuagiza injini, jambo ambalo aghalabu huchukua muda mrefu.
“Kwenye kuagiza injini huwa inachukua muda mrefu kwa sababu ni zote nne, kwa hiyo hapa mkandarasi kwa kawaida hutumia muda mrefu,” amesema.
Kutokana na maelezo ya meneja huyo, watumiaji wa kivuko hicho watalazimika kufunga mkanda muda wote huo wakisubiri kukamilika kwa ukarabati huo.
Subira kama hiyo, wanapaswa kuwa nayo kwa kivuko cha MV Magogoni ambacho Naibu Waziri wa Ujenzi, Geofrey Kasekenya, aliahidi kitakamilika Desemba mwaka huu.
Kivuko hicho kilichopaswa kukamilika Agosti mwaka jana, sababu za kuchelewa kwake ni kile kilichobainishwa katika uchunguzi uliofanywa na gazeti hili, kuwa Serikali ilichelewa kumlipa mkandarasi kwa ajili ya kukamilisha kazi.
Malipo ya awali yaani asilimia 10 ya Sh7.5 bilioni ambayo Serikali ilipaswa kumlipa mkandarasi African Marine and General Engineering Company Ltd Februari mwaka jana, ndiyo kwanza imeyafanya Februari mwaka huu.
Hata hivyo, Mwananchi linatambua kuwa hadi jana Serikali haikuwa imekamilisha malipo yaliyosalia kwa ajili ya matengenezo ya kivuko hicho, hivyo bado kunaibuka shaka kama kitarejea katika muda uliotajwa.
Mapito ya kufunga mkanda
Katika kipindi cha kufunga mkanda, watumiaji wa vivuko hivyo watatumia muda mrefu kupata huduma katika eneo la Kigamboni-Magogoni.
Vivuko vinavyoendelea kutoa huduma kwa sasa ni MV Kazi na Sea Tax mbili.
Uwezo wa MV Kazi ni kupakia jumla ya abiria 800 na magari madogo 11 kwa wakati mmoja, huku kila Sea Tax moja ikiwa na uwezo wa kupakia abiria 250 kwa safari moja.
Kwa maneno mengine safari moja ya vivuko vyote vinavyoendelea na huduma sasa, vitabeba jumla ya abiria 1,300.
Hata hivyo, MV Kazi inafanya kazi kwa saa 24, huku Sea Tax zikifanya kazi kwa saa nane pekee, kwa mujibu wa mkataba wake wa ukodishaji kati ya Temesa na Kampuni ya Azam Marine Ltd.
Hii inamaanisha, kama kitaanza kasi saa 12 asubuhi, kitafanya kazi hadi saa 7 mchana kisha hadi siku inayofuata tena. Nyakati za jioni zenye uhitaji wa watu bila shaka kutakuwa na masaibu kwa watumiaji.
Kikianza zaidi ya saa tatu asubuhi, ina maana jioni kitakuwapo huku watumiaji wa chini ya saa tatu asubuhi wakipata shuruba.
ili kukidhi haja ya abiria wote 60,000 wanaokadiriwa kuvuka kwa siku, vivuko hivyo vinapaswa kufanya safari 46 kwa siku.
Kupungua kwa vivuko hivyo kutawagharimu baadhi ya wananchi ambao awali walitumia kuvuka kutoka Kigamboni hadi Magogoni kwa Sh200, lakini sasa baadhi watapaswa kuzunguka kwa daladala kwa gharama ya Sh700.
Kwa upande wa wenye magari wanaotokea Kigamboni, ili kuwahi katikati ya jiji, watapaswa kuzunguka kwa njia ya Daraja la Nyerere ambayo kimsingi ni ndefu na inagharimu mafuta.
Hata hivyo, kipindi hicho cha changamoto ya usafiri wa vivuko ni fursa ya kuongezeka kwa mapato ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).
Ongezeko la mapato hayo, litatokana na kuongezeka kwa magari yatakayopita katika daraja la Nyerere ambao hulipia Sh3,000 kwa gari ndogo na Sh200 kwa pikipiki.
Shaka kwenye bajeti
Ingawa wakazi hao wanakadiriwa kufunga mkanda kwa takriban mwaka hadi vitakaporejea MV Magogoni na Kigamboni, lakini yapo mambo yanayoibua shaka ya kukamilika kwa kazi hizo haraka.
Ukiachana na michakato iliyoelezwa na Ameir kuhusu matengenezo, masuala ya kibajeti huenda yakasababisha MV Kigamboni nayo kukwama kama ilivyotokea kwa MV Magogoni.
Hilo linatokana na uhalisia kwamba, Ameir alisema bajeti ya matengenezo ya MV Kigamboni, itatokana na fedha iliyotengwa kwa ajili ya matengenezo ya vivuko katika bajeti ya mwaka wa fedha 2024/25.
Katika bajeti hiyo, Wizara ya Ujenzi imetenga Sh11.535 bilioni kwa ajili ya matengenezo ya vivuko mbalimbali, kikiwemo Kigamboni na Magogoni.
Katika fedha hiyo, MV Magogoni inapaswa kulipiwa Sh6.7 bilioni kama gharama za kukamilisha matengenezo, huku MV Kigamboni ikikadiriwa kuhitaji takriban Sh6 bilioni kwa ajili ya matengenezo.
Kwa maneno mengine, inahitajika Sh12 bilioni kukamilisha malipo ya MV Magogoni na kufanikisha matengenezo makubwa ya MV Kigamboni, fedha ambayo ni zaidi ya ile iliyotengwa katika bajeti.
Mbali na hilo, kwenye Sh11.535 bilioni iliyotengwa ndani ya bajeti hiyo ya Wizara ya Ujenzi kwa ajili ya matengenezo ya vivuko hivyo, hiyo hiyo inapaswa kugharimia matengenezo ya vivuko katika maeneo mbalimbali ya nchi kama vile MV Mara, MV Ujenzi, MV Kome II, MV Misungwi, MV Nyerere na MV Kyanyabasa.
Vingine ni MV Kitunda, MV Lindi, MV Kazi, MV Mwanza, MV Ukara I, MV Ukara II, MV Sabasaba, MV Pangani II pamoja na ukarabati wa MV Kilombero II kabla ya kukihamishia eneo la Mlimba – Malinyi.
Vilevile, kuna ukarabati wa boti ya uokozi ya MV SAR III, ukarabati wa kivuko MV Malagarasi na MV Mafanikio. Lakini kama haitoshi bajeti hiyohiyo inatakiwa kutumika kwenye ufuatiliaji na tathmini ya miradi hiyo.