Kipindupindu chabisha hodi Geita, watoto wawili wapoteza maisha

Baadhi ya wakazi wa Mtaa wa Uwanja kata ya Nyankumbu Mjini Geita wakipatiwa dawa za kutibu maji kufuatia vifo vya watoto wawili vilivyotokea kwenye eneo hilo, baada ya kuugua ugonjwa wa kuhara na kutapika na muda mfupi baadaye kupoteza maisha.

Muktasari:

  • Aprili 21,2024 katika Mtaa wa Uwanja Kata ya Nyankumbu Mjini Geita watoto wawili wa familia moja walipoteza maisha muda mfupi baada ya kuhara na kutapika huku mama yao na mdogo wao wakipelekwa kupata matibabu kutokana na tatizo hilo.

Geita. Uongozi wa  Mkoa wa Geita umewataka wananchi wa mkoa huo hususan mjini Geita kuchukua tahadhari na kuzingatia usafi kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa utoaji chanjo ya saratani ya mlango wa Kizazi iliyofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Mwatulole, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita,  Omar Sukari  amesema kuna wagonjwa wamebainika kuugua kipindupindu mjini Geita, hivyo wananchi wanatakiwa kuchukua tahadhari ili usienee.

“Nichukue nafasi hii kusema Geita tuna kipindupindu. Kuna familia imetibiwa, wapo waliolazwa wanaendelea na matibabu na wengine tumewaruhusu leo, niwaombe mchukue tahadhari zote za kukabaliana na magonjwa ya mlipuko hasa katika kipindi hiki,” amesema Dk Sukari.

"Wananchi chemsheni maji ya kunywa na ya kunawa, tumieni vyoo bora, tumieni maji tiririka na sabuni. Niwasihi walimu, simamieni shule kuhakikisha watoto wanapata maji lakini mnapoona dalili za kuharisha wapelekeni wapate matibabu mapema.”

Aprili 21, 2024 katika Kata ya Nyankumbu Mjini Geita, watoto wawili wa familia moja walipoteza maisha muda mfupi baada ya kuhara na kutapika huku mama yao na mdogo wao wakiwahishwa hospitali kupata matibabu.

Taarifa zilizopatikana zimesema watoto hao walizikwa na wataalamu kutoka idara ya afya.

“Hata maji tuliyokuwa tunatumia msibani yalitibiwa na dawa na majirani tulipatiwa  dawa za kutibu maji na tukatakiwa kuchukua tahadhari za kujikinga na magonjwa ya mlipuko,” amesema mmoja wa majirani na familio hiyo ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe.

Taarifa zisizo rasmi zinaeleza kuwa mpaka watu 11 akiwemo mama wa watoto hao, wameugua ugonjwa huo na kulazwa na watano kati yao, wameruhusiwa leo Aprili 23 kutoka hospitali huku wengine wakiendelea na matibabu.

Ester Charles, mmoja wa wanafamilia ambayo imekubwa na ugonjwa wa kuhara na kutapika, amesema mmoja wa watoto waliopoteza maisha alitoka shule na kula wali maharage kisha kwenda kucheza, lakini saa moja jioni alijisikia vibaya na kwenda kulala.

“Ilipofika saa 10 usiku alianza kutapika, nikatoa ‘flagyl’ na panado nikampa akaendelea kutapika, akaniambia mama nataka kujisaidia, akaanza kuharisha muda mfupi na mdogo wake naye akaanza kutapika na kuharisha, wakalegea. Saa 12 asubuhi mdogo wao mwingine naye akaanza kuharisha, tukawabeba na mama yao tukawapeleka hospitali binafsi wakaongezewa maji na vipimo wakasema ni homa ya matumbo na malaria, wakatupa dawa lakini walizidi kuharisha, tukarudi nyumbani.

“Tuliporudi hali ikazidi kuwa mbaya tukashauriana tuwapeleke hospitali kubwa, tukawaweka kwenye bajaji, tulipofika hospitali wakawafikisha chumba cha dharura, baada ya muda mfupi wakatwambia watoto wamepoteza maisha. Ndio tukarudi tukamkuta mama na huyo mdogo hali zao ni mbaya, tukawapeleka hosptali wakalazwa na wanaendelea na matibabu,” amesema Charles.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela amesema siku mbili zilizopita tatizo la ugonjwa wa kuhara na kutapika lilikumba familia moja mjini Geita na akawataka wananchi kuchukua tahadhari kwa kuwa ni ugonjwa hatari unaoweza kusababisha madhara.

“Ni ugonjwa unaosababisha vifo kwa haraka kwa kuwa unapoteza maji mengi, asilimia 70 ya mwili wa mwanandamu imebebwa na maji, unapotapika na kuhara uwezo wa kuhimili ni mdogo. Ugonjwa upo, unaweza kuwa kipindupindu au ugonjwa mwingine. Mnapokuwa na watu wana tatizo hilo lazima tuchukua tahadhari,” amesema Shigela

“Niwaombe tuchukue tahadhari hii itasaidia tusitumie gharama kubwa za matibabu, zingatieni maelekezo yanayotolewa na wataalamu ili tatizo lisisambae. Serikali inachukua kila hatua kudhibiti tatizo lisiendelee kuenea na kusababisha madhara zaidi,” amesema.