Kipindupindu chaibuka Kondoa

Dodoma. Ugonjwa wa kipindupindu umezuka katika Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma na hadi jana watu watano waliripotiwa kuugua ugonjwa huo na kulazwa hospitalini.

Jana, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Best Magoma alisema wagonjwa hao hali zao zinaendelea vizuri, huku akitaka tahadhari ichukuliwe, ili kuzuia ugonjwa kusambaa zaidi kwa maeneo mengine ndani na nje ya mkoa.

Mara ya mwisho ugonjwa huo kuripotiwa mkoani hapa ilikuwa Februari 2018, ambapo wilaya za Chamwino, Mpwapwa, Bahi na Kongwa zilikuwa na wagonjwa 471, lakini Kondoa haikuwa na wagonjwa kwa wakati huo.

“Ni kweli tuna ugonjwa huo, huwezi kusema kuwa walitoka wapi wagonjwa ila wananchi wanafahamu kuwa ndani ya mkoa na wilaya yetu ya Kondoa tuna wagonjwa wa kipindipindu, hilo pekee ndilo la muhimu wala si kingine kwa sasa,” alisema Dk Magoma.

Alisema hadi jana wagonjwa watatu walikuwa wakiendea na matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Kondoa na wataalamu walikuwa wakiendelea na juhudi za kuhakikisha hakuna maambukizi mengine mapya na elimu inatolewa kwa wananchi ili kuchukua tahadhari.

Mkuu wa wilaya hiyo, Dk Khamis Mkanachi alisema mpaka jana kulikuwa na wagonjwa watano ambao walifika katika Hospitali ya Mji Kondoa kwa ajili ya matibabu na kati ya hao, wawili walisharuhusiwa.

Alisema kati ya wagonjwa hao, watatu ni ndugu wa familia moja ambao walikwenda Arusha kwenye msiba na waliporudi walianza kuumwa na kuonyesha dalili za kipindupindu, ikiwemo kuharisha na kutapika na walipokwenda hospitali ilithibitika ni ugonjwa huo.

Kwa mujibu wa Dk Mkanachi, sampuli zao zilipochukuliwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali, mmojawapo alikutwa na ugonjwa huo na wawili walionyesha dalili za kipindupindu. Kwa mujibu wa mkuu huyo wa wilaya, tayari wametenga wodi maalumu kwenye Hospitali ya Halmashauri ya Mji Kondoa kwa ajili ya wagonjwa hao na kama idadi hiyo itaongezeka wataweka kambi kwenye uwanja wa Sabasaba.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji Kondoa, Dk Emiliana Donald alisema hawezi kuzungumza jambo hilo hadi atakapopata kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kondoa ambaye hata hivyo simu yake haikupatikana hewani.

Hata hivyo, Ofisa Habari wa Halmashauri ya Mji Kondoa, Sekela Mwasubila aliyataja maeneo yaliyoathirika na ugonjwa huo ni mitaa ya Bicha na Maji ya Shamba ambapo ndiko walikotoka wagonjwa hao.