Serikali yatangaza mlipuko wa kipindupindu Ilala

Muktasari:

Wizara ya Afya imetangaza mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu katika halmashauri ya Ilala jijini Dar es Salaam huku watu 10 wakithibitika kuwa na ugonjwa huo.

Dar es Salaam. Wizara ya Afya imetangaza mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu katika halmashauri ya Ilala jijini Dar es Salaam huku watu 10 wakithibitika kuwa na ugonjwa huo.

Kwa kupitia taarifa iliyotolewa na wizara hiyo jana Jumatatu Aprili 24, 2023 imesema ugonjwa huo uliripotiwa kwa mara ya kwanza Aprili 20, 2023 eneo la Kivule jijini hapa ambapo watoto wawili kutoka familia moja, akiwemo mwanafunzi mmoja kutoka shule ya msingi Kivule walithibitika kuwa na dalili za ugonjwa huo.

Pia, watu wanne walithibitika kuwa na dalili za ugonjwa huo, ambapo kati yao wanaume wawili na wanawake wawili.

“Dalili za ugonjwa huo zilianza kuonekana kuanzia Aprili 19, 2023. Visa vyote vinne vya ugonjwa huo wa mlipuko vimetokea kwa wanafamilia wanaoishi kaya moja kata ya Kivule mtaa wa 10.

“Katika visa hivyo vyote vinne vimetoka kaya moja, kwa sasa wagonjwa hao wamelazwa katika hospitali ya wilaya ya Kivule,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa visa vitatu vipya viliripotiwa katika maeneo ya Tabata, Ilala na Buguruni.

“Hadi kufikia jana jumla ya kesi 10 ziliripotiwa lakini hakuna vifo vilivyorekodiwa tangu kutokea kwa ugonjwa huo” imeeleza taarifa hiyo.

Kuhusu kukabiliana na ugonjwa huo, Wizara ya Afya imesema wanaendelea kufanya utafiti ili kutambua visa vingine na kukusanya sampuli mbalimbali.

“Tunaendelea kufanya utafiti ili kutambua visa vingine, tunakusanya sampuli za maji kwenye visima na maji ya bomba, pamoja na vyanzo vingine vya maji kwa ajili ya majaribio,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Tayari wizara imeanzisha kituo cha matibabu ya Kipindupindu katika hospitali ya wilaya ya Kivule.