Kitendawili kuwahamisha walioathiriwa na mafuriko Rufiji

Muktasari:

  • Tanesco yasema pamoja na madhara yanayojitokeza, mafuriko yangekuwa makubwa kama maji yasingedhibitiwa.

Rufiji. Zikiwa zimebaki siku tatu kabla ya shule kufunguliwa Jumatatu Aprili 8, 2024, baadhi ya wananchi wilayani Rufiji wanaendelea kuhamishia mizigo na samani shuleni kujihami na mafuriko.

Wananchi hao wameathiriwa na mafuriko yaliyofunika makazi na mashamba yao baada ya maji ya Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP) kufunguliwa.



"Tunaambiwa tuondoke, lakini hatujui twende wapi," amesema Yusuf Mbawala, ambaye ni mwalimu wa Shule ya Msingi Mohoro.

Amesema, "sisi walimu tumepanga nyumba huko mitaani, nyumba ndio zimezama, twende wapi? Mimi nimehamia hapa ofisini."

Bahati Msura amesema alihamia Kijiji cha Mohoro mwaka 2023 akitoa Mkoa wa Mara, kwa ajili ya kazi za kilimo, lakini ameambulia uharibifu.

"Nilipokuja huku nilipata shamba nimelima, mazao ya kwanza yalizama na sasa ya pili yamezama na nyumba imezama," amesema.



Ameeleza, "kabla maji hayajaanza kujaa tukaambiwa tuhame, sasa mimi na watoto wawili, sina ndugu, nitahamia wapi? Kweli maji yakaja, najua kweli shule zinafunguliwa, lakini mwanangu yuko darasa la nne na mwingine la kwanza, nikaona tuje hapahapa shule."

Awali, akizungumza na wananchi hao, Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Edward Gowele, amesema Serikali inatafuta majengo ya umma ya kuwahamishia watu hao wapatao 67.

"Tunajua shule zinafunguliwa, viongozi watafute maeneo mengine ya kuwahifadhi watu hawa. Tunashukuru kwa kuwapokea ndugu hawa, ikishindikana tutaangalia majengo ya Serikali ili kuwahifadhi. Tumewapokea hapa vizuri lakini tutawatafutia maeneo mengine, kwa sababu shule hazisubiri," amesema.

Amesema ili kuepusha maafa kwa wanafunzi, wanaangalia uwezekano wa chakula kwa wanafunzi.

"Tutaangalia kuwasaidia watoto ili wasivuke mara kwa mara kwenye maji.

“Na tunajua kuwa magonjwa yanaweza kutokea kwa sababu maji yanakuja na uchafu," amesema.

Mtendaji wa Kata ya Mohoro, Hilda Kiboja amesema kuna maeneo wanayoandaa kwa ajili ya kuwahifadhi waathiriwa ambayo ni pamoja na maghala na nyumba za ibada.

Kuhusu chakula, amesema asilimia 80 ya wakazi wa kata hiyo, hawana chakula.

"Kwa sasa tuna mpango wa chakula kwa watoto, ili wasiwe na mizinguko ya kwenda na kurudi kutafuta chakula. Hii ya watoto kuvuka maji na kurudi ni changamoto, tunataka tupate eneo moja wapate chakula,” amesema.

"Kwa sasa hatujapokea hicho chakula, lakini halmashauri ina mpango wa kuleta," amesema.


Tathmini ya mafuriko

Gowele amesema wanaendelea na tathmini ya madhara yaliyosababishwa na mafuriko hayo.

Akizungumza na wananchi katika Kijiji cha Mohoro, alipokagua maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko hayo, Gowele amewaomba wananchi wahame makazi yaliyo bondeni.

"Tunapata taarifa za maafa kila siku kutoka kwa viongozi wetu. Hameni kwa wakati, hata hivyo wananchi wa Mohoro mmetufurahisha,” amesema na kuongeza:

"Hatuwezi kuwafukuza bali tutawashauri, na muwapokee walioathiriwa, hata kama si ndugu zenu. Hameni kwa utaratibu. Huu ni wakati wa kushikamana."

Amesema kabla maji hayajaanza kujaa, walitoa tahadhari na baadhi ya wananchi waliondoka kwenye maeneo hatarishi.

"Kila wakitupa taarifa na sisi tunawaambia, tunawashukuru walioitikia. Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa bwawa hilo, vinginevyo hali ingekuwa mbaya," amesema.

Kuhusu tathmini ya maafa, amesema kati ya kata 13 za wilaya hiyo, 12 zimeathiriwa.

Amesema mpaka sasa wameshakamilisha tathmini katika kata sita na bado wanaendelea.

"Si ninyi tu, nimechelewa hapa kwa sababu kata zote 12 zimeathiriwa na maji. Kuna timu ya tathmini inaendelea na sisi tunakuja kufuatilia. Tunamshukuru mbunge (Mohamed Mchengerwa) aliyekuja kutembelea, ametembelea maeneo ambayo hata sikuyafikiria, tumefanya mikutano minne," amesema.

Amewataka wazazi kuwalinda watoto wasizame kwenye maji na kujilinda magonjwa ya mlipuko.

Awali, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Rufiji, Rajab Mbonde ameitaka Serikali kuwafariji kwanza wananchi walioathiriwa kabla ya kuwataka kuhama.

"Mkuu wa wilaya tangu umehamia hapa hujawahi kututembelea, lakini wasaidizi wako wakija hapa, wanasema muhame, muhame, kwa nini wasituambie mwafaka wetu?” amehoji.

“Sisi tunataka mbegu za mazao. Wananchi wanataka maneno ya faraja. Hali hii tunaweza kusema tumeshaizoea, leo mtu ana shamba halafu unasema ahame?" amesema.

Diwani wa Kata ya Mohoro, Aboubakar Chobo ameomba kuharakishwa misaada kwa waathiriwa wa mafuriko.

"Kukitokea msaada wowote tuangalie watoto wetu, kuna shule zilizoathiriwa zikiwamo za Mohoro na Nyampaku. Tuangalie madarasa ya mitihani. Tusije kufanya vibaya,” amesema.

"Tathmini ifanyike vizuri, kama ni chakula kila mtu apate sawa. Kama ni kilo moja basi apate, si wengine wanapata wengine wanakosa," amesema.

Wakati huohuo, baadhi ya wananchi wameonekana wakiendelea kuhamisha vitu vyao kutoka kwenye maeneo yaliyoathiriwa.

"Maji yanazidi kuongezeka ndiyo maana unaona tunahamisha vitu hivi," amesema Mohamed Said.


Kauli ya Tanesco

Licha ya kuleta madhara kwa makazi ya watu na mazao ya kilimo, imeelezwa mafuriko ya mwaka huu hayajafikia ya mwaka 2020 kwa kuwa yamedhibitiwa.

Mhandisi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kutoka bwawa la JNHPP, Dismas Ngoto amesema hayo leo Aprili 5, 2024 alipozungumza katika ziara ya mkuu wa wilaya kukagua madhara ya mafuriko katika Kijiji cha Mohoro.

Amesema walianza kufungua maji hayo Machi 5, 2024 na wanatarajia kuyafunga Mei 25, 2024.

"Hivi sasa maji yanayokuja katika bwawa la Nyerere ni mita za ujazo 8,300 sawa na lita milioni 8.3 kwa sekunde. Kama tusingeyazuia moja kwa moja madhara yake yangekuwa makubwa mno,” amesema.

Amesema mafuriko yaliyotokea mwaka 2020 yalikuwa mita za ujazo 7,000 sawa na lita milioni 7 kwa sekunde, na yalikuwa yanashuka.

"Maji yale yalileta madhara makubwa japo watu walipona. Sasa kama haya yangeachiwa yashuke moja kwa moja, madhara yake yangekuwa makubwa mno," amesema.

Amesema kwa sasa wanayadhibiti maji hayo kwa kuyaachia mita za ujazo 3,000 hadi 6,000 kwa siku.

"Hii yote ni kutokana na mvua zilizotangazwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kwamba zitakuwa kubwa, na si hapa tu, madhara yako nchi nzima.

"Sisi Tanesco tunasema pole, pole, pole sana. Maji haya tunayofungulia ni kidogo mno ukilinganisha na yanayokuja katika bwawa la Nyerere," amesema.

Akizungumzia suluhisho la kudumu la mafuriko, Gowele amesema wameshatenga eneo la kuwapa wananchi ardhi.

"Mohoro tumeshatenga eneo ambalo ni salama zaidi na tumeshawapatia wananchi maeneo yale, baadhi ya ambao wako hapa tayari wana maeneo huko ni muda tu,” amesema.

"Tunaendelea kufanya utaratibu wa kuwahasisha wananchi ili wahamie huko waache kuhama-hama," amesema.

Kuhusu athari za kiafya, Gowele amesema wameunda kamati ya afya iliyo chini ya mganga mkuu wa wilaya inayoratibu.

"Tunayo timu ya mganga mkuu imeshaweka kambi hapa karibu na maeneo yote yaliyoathirika. Tuna vituo vya afya vya kutosha, tuna zahanati za kutosha tuna vifaa vya kutosha, tuna jengo la dharura pale Ikwiriri,” amesema.

Ameeleza, “yote haya yapo kwa ajili ya kuhudumia yanapotokea magonjwa ya mlipuko, kuna timu iko ‘mobile’ na nyingine imetulia."