Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kivumbi uchaguzi chaibua wadau

Dar/mikoani. Wakati Rais Samia Suluhu Hassan akisema mwakani kutakuwa na kivumbi cha uchaguzi wa viongozi wa Serikali za Mitaa, wanasiasa na wananchi wa kada mbalimbali wamesema ili kiwe kivumbi cha kweli ni muhimu sintofahamu zilizojitokeza mwaka 2019 zikaepukwa.

Mambo ambayo wameshauri yafanyike ili kuepuka sintofahamu hizo, ni pamoja na wasimamizi kutowaengua wagombea bila sababu za msingi na kuacha ushindani utamalaki pamoja na kuuondoa uchaguzi huo Tamisemi, badala yake usimamiwe na Tume huru ya uchaguzi.

Wadau hao wanautaja uchaguzi wa mwaka 2019 kuwa ulikuwa wa aina yake, ambapo wengi waliogombea kupitia vyama vya upinzani, wakiwemo wasomi na watumishi wa umma wastaafu, walienguliwa kwa kigezo cha kukosea kujaza fomu.

Hali hiyo, wamesema inawakatisha tamaa wananchi na iwapo dosari hizo zitajirudia, hawatapoteza muda kugombea au kupiga kura.

Pamoja na maoni hayo, wameeleza haja ya kuwepo chombo huru cha kuusimamia uchaguzi huo badala ya Tamisemi, wakisisitiza kwamba huo utakakuwa mwarobaini wa dosari nyingi.

Mtazamo huo ni sawa na ule uliotolewa na wadau wa demokrasia mbele ya Kikosi Kazi cha kuratibu maoni ya wananchi kuhusu demokrasia ya vyama vingi ambacho ripoti yake ilikabidhiwa kwa Rais Samia, Oktoba mwaka jana.

Wadau hao wakiwemo viongozi wastaafu serikalini, taasisi, asasi za kirai walipendekeza uchaguzi wa Serikali za mitaa usimamiwe na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ili kuongeza ufanisi na kuondoa mkanganyiko uliopo.

Hata hivyo, Tamisemi yenyewe ilipofika mbele ya kikosi kazi ilipendekeza iendelee kuusimamia uchaguzi huo.

Uchaguzi wa viongozi wa vitongoji, vijiji na mitaa 2019 ndiyo unaodaiwa kuacha makovu ya kisiasa na kijamii kutokana na wagombea wengi wa upinzani kuenguliwa.

Katika uchaguzi huo, CCM, ilitangazwa kushinda kwa asilimia 99 ikijizolea mitaa 4,207 kwa wagombea wake kupita bila kupingwa, vijiji 12,028 na vitongoji 62,927, huku maelfu ya waliogombea kupitia vyama vya upinzani wakienguliwa kwa sababu mbalimbali.

Licha ya CCM kunyakua ushindi huo, wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema chama hicho tawala kilikosa uhalali wa kisiasa katika maeneo mengi, jambo linalosababisha baadhi ya wananchi kuacha kuhudhuria mikutano.

Kumbukumbu za kilichotokea mwaka 2019, wanasema huenda ndiyo sababu Rais Samia aliufananisha uchaguzi wa Serikali za mitaa 2024 na kivumbi na hata kumpeleka Mohamed Mchengerwa kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii kuwa Waziri wa Tamisemi.

“Sasa nimempeleka Tamisemi. mwakani kuna kivumbi na mimi nakujua. Najua unaweza. Kivumbi kile kinafanana na kifua chako. Najua unaweza. Kwa hiyo nimekupeleka Tamisemi ni kazi kazi ili mwakani tu sail (tupite) vizuri,” alisema baada ya kuwaapisha viongozi mbalimbali aliowateua.

Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango alienda mbali akifafanua zaidi kuwa Rais Samia ameona apange safu ambayo inaweza kufunga magoli kuanzia uchaguzi serikali za mitaa mwakani na uchaguzi mkuu 2025 na kusisitiza yawe magoli ya uhakika.

Kutokana na agizo hilo, Waziri Mchengerwa alisema “mimi sina hofu nalo, kwani tafsiri ya Rais ni kwenda kufanya kazi, uchaguzi utakuwa mwepesi kama kila mmoja atafanya kazi usiku na mchana, Watanzania wanaona tumefanya nini.

“Kama kuna sehemu hatutafanya kazi, basi utakuwa ni mgumu, lakini kama tutafanya kazi, tutatatua kero za wananchi, miradi itatekelezwa utakuwa uchaguzi mwepesi sana na kama hatutafanya haya, basi utakuwa uchagizi mgumu."

Hata hivyo, akizungumza na Mwananchi, Katibu wa Organizesheni wa CCM Zanzibar, Issa Haji Ussi ‘Gavu’ alisema chama hicho hakijawahi kulalamikia uchaguzi, muda wote wanaamini mchakato huo unapofanyika unakuwa huru na haki.

“Tunaamini hivyo kwa sababu lolote litakalokuwa limetendwa kinyume cha Katiba na miongozo, sheria za nchi zinaelekeza anayehisi hakutendewa haki anajua nini cha kufanya kupata haki zake, ikiwemo kwenda mahakamani,” alisema Gavu.

Alisema CCM inaamini uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2024 utakuwa huru, haki, wazi na usawa huku akivitaka vyama vitakavyoshiriki kusimamia taratibu na kanuni za mchakato huo.

Misingi ya demokrasia

Akizungumzia uchaguzo huo, Ali Makame Issa alisema viongozi wa Serikali wanatakiwa kuwa na nia na dhamira njema ya kuendesha uchaguzi katika misingi ya kidemokrasia.

“Kumekuwa na malalamiko ya wananchi na vyama kuwa wanaosimamia uchaguzi wa Serikali za mitaa ni wateuliwa ambao wapo katika ngazi za halmashauri, jambo hilo limesababisha uzito mkubwa wa kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na haki.

“Viongozi wa vyama na wanaharakati wanatamani kuona hizi chaguzi zinasimamiwa na Tume huru ya uchaguzi ili kwenda uchaguzi utakaopunguza dosari, basi miongoni mwa mambo yanayotakiwa pia ni kuheshimu sheria zilizopo,” alisema.

Uvunjifu wa amani

Wananchi waliozungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, walisema endapo mambo yaliyojitokeza mwaka 2019 yatajitokeza tena mwakani, kuna hatari ya kusababisha uvunjifu wa amani.

Mkazi wa Bomang’ombe wilayani Hai mkoani Kilimanjaro, Simon Mnyampanda, alisema kilichotokea katika uchaguzi huo ni uhuni, kwani wengi waliogombea walienguliwa kwa kigezo cha “kutojua kusoma na kuandika.”

“Nina rafiki yangu ni daktari, mtumishi wa Serikali mstaafu, aligombea uenyekiti wa mtaa lakini akaenguliwa eti hajui kusoma. Alipopambana nao wakamwambia hajui Kiingereza. Akawaandikia Kiingereza haikusaidia,” alisema Mnyampanda.

Mnyampanda alisema baadhi ya fomu za wagombea zilichezewa kwa kuongezewa namba au herufi mbele na kutolea mfano mgombea aliyejaza amezaliwa tarehe 03.06.1980, fomu yake iliongezewa herufu na kusomeka tarehe 030.

Hellen Michael wa Dar es Salaam, pamoja na kukosa uelewa wa kina kuhusu uchaguzi huo, alisema anachokisikia zaidi ni malalamiko ya kukosekana haki kwa wagombea wa vyama vya upinzani.

“Mimi si mfuatiliaji wa mambo haya, nilishakata tamaa kila siku mnakwenda kumchagua mtu mnayeona sahihi, wao wanampa wanayemtaka wao, nikaachana na hivi vitu, lakini marekebisho yafanyike kwenye haki kwa wagombea wa vyama vyote,” alisema Hellen wa Kigamboni, Dar es Salaam.

Mkazi wa Butimba jijini Mwanza, Abel Luhima alisema, “uchaguzi wa mwakani sidhani kama utakuwa wa haki...kwa usimamizi huu? Yaani uchaguzi unasimamiwa na Tamisemi ambayo waziri wake anateuliwa na Rais? Hivi wewe unaweza kumwangusha bosi wako? Hapana utajipendekeza ili umfurahishe na watamfurahisha kwa kuhakikisha wenyeviti wa chama chao wanashinda.”

Mkazi wa Mtwara mjini, Mwanahamisi Juma alisema," nadhani ni wakati sasa wa kila chama cha siasa kujitathini na kuangalia mapungufu na kuyarekebisha kama ni tume basi ifumuliwe yote na kufanyiwa ukarabati na kama ni katiba ifanyiwe marekebisho, tunahitaji viongozi ambao tutawachagua sisi wananchi, si wale watakaoteuliwa bila ridhaa yetu."

Mchungaji Ashery Kihombo wa Kanisa la KKKT alisema dalili njema zimeonekana kupitia kauli anazozitoa Rais Samia kwamba anataka demokrasia, ingawa kuna mashaka kwa wasaidizi wake.

Hata hivyo, alisema uhuru wa kujieleza, mikutano ya hadhara na maridhiano yaliyofanyika hivi karibuni yanatoa ishara nzuri kuwa mbele kutakuwa na ushindani wa haki.

Viongozi wa siasa

Baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa wamesema ili uchaguzi wa serikali za mitaa uwe huru na haki unapaswa kusimamiwa na chombo kingine, si Tamisemi.

“Ingawa wagombea huenguliwa katika chaguzi nyingi, lakini uchaguzi wa mwaka 2019 ulitia fora. Asilimia 90 wagombea wetu walienguliwa na hatuamini sababu ilikuwa kukosa sifa,” alisema Ado Shaibu, Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo.

Shaibu alisema kinachotakiwa ni usawa na uchaguzi ukisimamiwa na chombo huru na kwamba kila kitu kitakwenda vizuri.

Wakati Ado, akieleza hayo Katibu Mkuu wa CUF, Hamad Masoud alisema kitendo cha uchaguzi wa serikali za mitaa kusimamiwa na Tamisemi kunakuwa na upendeleo kwa baadhi ya wagombea na vyama vya siasa.

Masoud aliyewahi kuwa Waziri wa Miundombionu katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, alisema kama Serikali ipo tayari na inataka demokrasia katika chaguzi zijazo basi, makosa ya mwaka 2019 yasijirudie uchaguzi wa mwaka 2024.

Naye Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itikadi, Uenezi na Mambo ya Nje ya Chadema, John Mrema alisema kukosekana kwa Tume ya kusimamia uchaguzi ni miongoni mwa mambo yaliyosababisha dosari katika uchaguzi huo.

“Watu wanaosimamia uchaguzi ni wateuliwa wa Rais, hawa ndiyo wanaosababisha mchakato huu kutokuwa mzuri ikiwemo kuwaengua wagombea wetu,” alisema Mrema.

“Unakuta mgombea ni mwalimu mstaafu halafu anaambiwa hajui kusoma na kuandika na kuenguliwa. Haliingii akilini. Kwa lugha nyepesi uchaguzi wa Serikali za Mitaa unasimamiwa kutokea Ofisi ya Rais na hakuna haki,” alisema Mrema.

Mrema ambaye pia aligombea ubunge jimbo la Segerea, alisema kinachopaswa kufanyika ni kuwepo kwa Tume huru itakayosimamia mchakato huo bila upendeleo kwa upande wowote sambamba na kubadilishwa kwa sheria za uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Imeandika na Daniel Mjema na Florah Temba (Moshi), Juma Issihaka, Bakari Kiango (Dar), Mary Sanyiwa (Iringa), -Joseph Lyimo (Manyara), Bahati Mwatesa (Lindi), Lilian Lucas (Morogoro), Saada Amir (Mwanza), Florence Sanawa (Mtwara).