Kizazi chenye elimu bora kitachochea uhifadhi, kutokomeza ujangili na kulinda rasilimali za Taifa

Kizazi chenye elimu bora kitachochea uhifadhi, kutokomeza ujangili na kulinda rasilimali za Taifa

Muktasari:

  • Jamii nyingi za Afrika zimekuwa zikirithisha tamaduni, elimu, biashara au kazi vizazi kwa vizazi. Urithi huu umekuwa pia ukifanyika Tanzania mfano mzuri ni jamii za wilaya ya Serengeti na Bunda zinazozunguka mapori ya akiba ya Ikorongo Grumeti na Ikona WMA mkoani Mara.

Jamii nyingi za Afrika zimekuwa zikirithisha tamaduni, elimu, biashara au kazi vizazi kwa vizazi. Urithi huu umekuwa pia ukifanyika Tanzania mfano mzuri ni jamii za wilaya ya Serengeti na Bunda zinazozunguka mapori ya akiba ya Ikorongo Grumeti na Ikona WMA mkoani Mara.

Asilimia 90 ya wakazi wa maeneo haya wamekuwa wakijishughulisha na kilimo na ufugaji kama njia kuu ya kujiingizia kipato na wamekuwa wakihusisha pia vizazi vyao. (Tafiti ya Kaya-Grumeti Fund mwaka 2016).

Kizazi chenye elimu bora kitachochea uhifadhi, kutokomeza ujangili na kulinda rasilimali za Taifa

Vilevile kutokana na vijiji hivi kuwa pembezoni mwa maeneo ya hifadhi za wanyamapori, baadhi ya watu wamekuwa wakijihusisha na ujangili wa wanyamapori na kuchangia kuharibu na kupoteza rasilimali za taifa.

Tunaamini kuwa tukiwawezesha vijana kupata elimu bora tutatengeneza jamii inayoelewa umuhimu na manufaa ya uhifadhi wa wanyamapori, itakayokuwa mstari wa mbele kutunza mazingira na kuunga mkono juhudi za Serikali na wadau wa maendeleo kwenye uhifadhi, kulinda wanyamapori, kutokomeza ujangili na kujivunia rasilimali zetu.

Shirika la Grumeti Fund ni wadau wa maendeleo mkoani Mara wanaofanya jitihada mbalimbali kuendeleza elimu mkoani humo.

Jinsi gani shirika la Grumeti fund linachangia elimu?

Meneja wa kitengo cha Maendeleo ya Jamii wa shirika hilo, Frida Mollel anasema, “Dhamira yetu ni kuwasaidia vijana kufikia viwango vya juu vya elimu kwa kutumia mkakati wetu wa UPLIFT (Unlocking Prosperous Livelihoods for Tomorrow) wenye lengo kuu la kuhakikisha tunatoa maarifa, zana na rasilimali zitakazowawezesha wanajamii kujihudumia wenyewe, familia zao na jamii nzima kwa ujumla.”

Ufadhili wa wanafunzi

Wasichana wamekuwa wakikumbwa na changamoto nyingi kwenye elimu ikiwamo mila na desturi potofu, kuwa na muda mchache wa kujisomea nyumbani kutokana na kazi za nyumbani pamoja na umbali wa shule. Mwanafunzi wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Issenye wilayani Serengeti, Leonia Chacha (16) (sio jina lake halisi) anasema, “Kuwa msichana kwenye familia ya mitala yenye watoto 9 si kuwa na ndoto ya kusoma. Baba yangu hakuwa na kipato cha kutusomesha wote.

Kizazi chenye elimu bora kitachochea uhifadhi, kutokomeza ujangili na kulinda rasilimali za Taifa

Nilijua ningeishia kwenye mimba au ndoa za utotoni kama wasi-chana wengine wa rika langu kwenye jamii yangu. Baada ya kupata ufadhili wa shirika la Grumeti Fund ndoto yangu ya elimu imetimia.”“Baada ya wazazi wangu kufariki nilijikuta nimeacha shule nikiwa darasa la pili na kuchunga mifugo ya mjomba wangu. Grumeti Fund imefufua ndoto yangu ya elimu iliyokuwa imekufa. Siamini nimeingia kidato cha nne mwaka huu naona naikaribia ndoto yangu ya kuwa rubani ili niisaidie familia yangu,” alisema mwanafunzi mwingine mnufaika, James Marwa (18) (sio jina lake halisi).

Kila mwaka shirika la Grumeti Fund hutoa nafasi 100 za ufadhili wa wanafunzi kwenye ngazi mbalimbali za elimu kuanzia elimu ya sekondari, vyuo vya stashahada, vyuo vya ufundi stadi, vyuo vya elimu ya juu nchini na kwenye Chuo cha Upishi cha Singita, ambacho ni mshirika mkubwa wa Grumeti Fund na ambacho hutumia mitaala ya hoteli za kimataifa kufundisha upishi.

Kizazi chenye elimu bora kitachochea uhifadhi, kutokomeza ujangili na kulinda rasilimali za Taifa

Vilevile shirika la Grumeti Fund huunganisha wanafunzi wafadhiliwa na washauri (mentors) ambao ni wafanyakazi wa shirika kwa ajili ya kuwasimamia na kuwaongoza ili waweze kufaulu masomo yao na kutimiza ndoto zao.

Kwa upande wa wasichana, shirika hufanya makongamano ya kuwawezesha kujitambua, kujua haki zao, kuwapa elimu ya afya pamoja na kuwapa taulo za kike zitakazowasaidia kuhudhuria darasani bila wasiwasi kila mwaka. Kupitia makongamano hayo ya uwezeshaji wasichana, wasichana zaidi ya 4900 wamefikiwa kuanzia mwaka 2017 mpaka mwaka 2020.Frida Mollel alifafanua kuwa, “Wanafunzi wanaomaliza masomo yao na kufaulu vizuri hupata nafasi ya kufanya mazoezi kwa vitendo na baadhi yao kuajiriwa na shirika na mshirika wake Singita kwenye vitengo mbalimbali kama utafiti, askari wa wanyamapori, upishi na kwenye hoteli za utalii.”“Ni faraja kubwa tunapoona wanafunzi wengi tuliowafadhili wakiwa wanafanya kazi kwenye mashirika na kampuni kubwa pamoja na taasisi mbalimbali za Serikali,” alisema Frida.

Uboreshaji wa miundombinu ya elimu

• Ujenzi wa madarasa na nyumba za walimu

Kutokana na umbali mrefu wanaotembea wanafunzi kufuata shule, shirika la Grumeti Fund lilifadhili ujenzi wa madarasa kwenye shule za msingi na sekondari Makundusi, nyumba 4 za walimu na kutoa madawati 240 ili kuboresha miundombinu ya shule. Hii iliongeza mahudhurio ya wanafunzi na ari ya wazazi kuandikisha watoto wao shuleni.

• Mafunzo ya lugha

Lugha ya Kiingereza ni changamoto kubwa wanayokutana nayo wanafunzi wa shule za msingi zinazotumia Kiswahili wanapoingia sekondari kwa kuwa ni lugha kuu ya kufundishia darasani. Shirika la Grumeti Fund linashirikiana na shirika la Concordia Language Villages la Marekani kufundisha wanafunzi wa shule za msingi lugha ya Kiingereza ya kuongea na kuandika. Wanafunzi zaidi ya 730 wamenufaika na mafunzo haya yalioonyesha kuleta matokeo makubwa kwa kuwaongezea wanafunzi uelewa, kupenda lugha ya Kiingereza na kuwaongezea kujiamini hivyo kumudu masomo yao.

• Uwezeshaji wa walimu

Ili kuendelea kuboresha elimu na ufaulu wa wanafunzi ni vyema kuongeza ujuzi kwa walimu. Kila mwaka, shirika la Grumeti Fund linatoa mafunzo ya ufundishaji kwa walimu wa shule za msingi za serikali zilizopo kwenye vijiji 21 vya wilaya ya Serengeti na Bunda ili kuwaongezea ujuzi wa kutumia nyenzo za ufundishaji zilizopo kwenye mazingira yao ili kuongeza uelewa wa wanafunzi kwenye masomo. Walimu 95 wa shule zote za msingi serikali zilizopo kwenye vijiji 21 vya wilaya ya Serengeti na Bunda wameshapata mafunzo hayo.

Elimu ya mazingira

Jamii za wilaya ya Serengeti na Bunda zimebarikiwa kuzungukwa na rasilimali kubwa ya mapori ya akiba ya Ikorongo Grumeti yenye wanyamapori wanaotumika kukuza uchumi wa Taifa kupitia shughuli za utalii.

Kupitia kituo cha elimu ya mazingira shirika la Grumeti Fund limekuwa likifundisha uhifadhi na utunzaji wa mazingira kwa wanafunzi wa sekondari kila mwaka ambao husambaza elimu hiyo kwa wenzao shuleni na kwenye jamii kupitia klabu za Malihai.

“Elimu ya mazingira imelenga kuwapa vijana hamasa ya kujivunia na kulinda mazingira ikiwemo wanyamapori, kutambua fursa zilizopo kwenye uhifadhi na kuzitumia kujiletea maendeleo kama ufugaji wa nyuki na upandaji wa miti na kuhamasika kusomea uhifadhi na utafiti wa wanyamapori kwenye elimu ya juu ili tuwe na wataalamu wengi zaidi watakaochangia maendeleo ya uhifadhi,” alisema Frida.

Grumeti Fund ni shirika lisilo la kiserikali linalojishughulisha na uhifadhi, kupambana na ujangili, kulinda mahusiano kati ya wanyamapori na jamii, kufanya utafiti na uvumbuzi wa mfumo wa ikolojia ya Serengeti na shughuli za maendeleo ya jamii hasa elimu, biashara na elimu ya mazingira kwenye vijiji 21 vya wilaya za Bunda na Serengeti mkoani Mara.