Kizimbani kwa kughushi hati ili apate mkopo wa Sh350 milioni

Tuesday April 13 2021
kortini pc
By Hadija Jumanne

Dar es Salaam. Mkazi wa Magomeni Mikumi mkoani Dar es Salaam, John Kyenkungu (65) amefikishwa katika mahakama ya hakimu mkazi Kisutu kujibu mashtaka mawili ya kughushi hati ya nyumba kwa lengo la kujipatia mkopo wa Sh350 milioni kutoka benki.


Mshtakiwa huyo amesomewa mashtaka hayo jana Jumatatu Aprili 12, 2021 na wakili wa Serikali, Adolf Lema mbele ya hakimu mkazi mwandamizi, Augustina Mmbando.


Wakili Lema amedai mshtakiwa anakabiliwa na kesi ya jinai na anadaiwa kutenda makosa yake mkoani humo.


Advertisement

Lema amedai katika shtaka la kwanza, Kyenkungu anadaiwa katika tarehe tofauti mwaka 2014 kwa nia ya kudanganya, alighushi hati ya mkopo ya mwaka 2014 kwa kusaini kuwa Said Nassoro amekubali kutumia hati ya nyumba yenye namba 25480 iliyopo kiwanja namba 516 kitalu B, eneo la Mikocheni Wilaya ya Kinondoni ili itumike kama dhamana ya kupata mkopo kutoka benki ya Equity kiasi cha Sh350 milioni.


Katika shtaka la pili Agosti 23, 2014 mshtakiwa huku akijua na kwa nia ya kudanganya alighushi barua ya Agosti 23, 2014 kwa kuonyesha kuwa Said Nassoro alikubali hati yake ya nyumba itumike kukopea Sh350 milioni katika benki hiyo, wakati akijua kuwa ni uongo.


Upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na upande wa mashtaka wameomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.


Mshtakiwa baada ya kusomewa mashtaka yake ameomba dhamana kwa kuwa mashtaka anayotuhumiwa nayo yanadhaminika.


Hakimu Mmbando alikubaliana na ombi la mshtakiwa na kutoa masharti ya dhamana ambayo  mshtakiwa alishindwa kuyatimiza na kurudishwa rumande huku kesi hiyo ikiahirishwa hadi Aprili 21, 2021 itakapotajwa tena.


Advertisement